ALIYEUAWA NA MAJAMBAZI KATIKA UPORAJI ARUSHA ATAMBULIWA


Aliyekuwa katika tukio la uporaji wa Sh milioni 20 kutoka kwa mtumishi wa duka la kubadilishia fedha za kigeni la Northern Bureau de Change,  ametambuliwa kuwa ni mwalimu mstaafu wa jijini  Arusha, Benedict Mmasi. 
Mmasi ambaye mkewe ni Diwani wa Viti Maalumu, Liliani Mmasi (CCM), aliuawa juzi. 
Alipigwa risasi baada ya kutoka kusali katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mjini Kati na kwenda kununua magazeti eneo ambako uporaji ulifanyika. 
Alipoona mama akipiga kelele kuomba msaada, Mmasi  alikwenda kusaidia lakini kabla ya kufika alipigwa risasi  ubavuni na kufa papo hapo . Ilikuwa saa 3.30 asubuhi katika Mtaa wa Maeda katikati ya Jiji la Arusha. Majambazi hao walikuwa kwenye pikipiki na walikimbia kupitia barabara ya Old Moshi. 
Kwa mujibu wa kaka wa marehemu, Adamu Mmasi  kifo cha mdogo wake kimeacha pengo kubwa kwa familia. Ameacha  mke,  Liliani na watoto watatu; wawili wakiwa wa kike. 
Kaka huyo wa marehemu alisema ndugu yake kabla ya kujishughulisha na biashara ya kununua, kuuza na kuchimba madini, alifundisha shule kadhaa jijini hapa. 
Maziko yatafanyika keshokutwa nyumbani kwake Mashono jijini hapa.

No comments: