AJIANDAA KUZUIA SIKU 60 ZA NYONGEZA BUNGE LA KATIBA



Mjadala wa Bunge Maalumu la Katiba, umeanza kuibuka upya wakati Bunge la Bajeti likienda ukingoni ambapo Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Tanzania Bara, Mwigulu Nchemba ameibuka na hoja ya kupinga nyongeza ya siku 60 za Bunge hilo.
Akihutubia wakazi wa Manispaa ya Iringa na vitongoji vyake katika mkutano uliopewa jina la Ondoa Msigwa Iringa Mjini, Mwigulu alisema atapinga kwa nguvu zake zote Bunge hilo kukutana kwa siku nyingine 60.
Wakati Mwigulu akipinga kuendelea kwa Bunge hilo, mjumbe wa Bunge hilo na Mbunge Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), ametuma ujumbe kwa wajumbe wenzake waliojiundia kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kuwa ili kumuenzi mama yake mzazi Shida Salum, aliyefariki dunia juzi na kuzikwa jana, wawaletee Watanzania Katiba mpya.
Mwigulu, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, alisema sababu ya hatua hiyo ni mtazamo wake kuwa bunge hilo likiendelea kama lilivyofanyika katika awamu ya kwanza, itakuwa sawa na kutumia vibaya fedha za walipa kodi.
Aliahidi kumshauri Spika wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta, amuandikie barua Rais Jakaya Kikwete, ili avunje Bunge hilo, endapo wajumbe wake watashindwa kutumia wiki mbili za mwanzo kujadili mambo ya msingi katika rasimu hiyo.
Kwa mujibu wa Mwigulu, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, nchi imepoteza fedha nyingi katika awamu ya kwanza ya mjadala wa Katiba katika Bunge hilo, kwani kwa zaidi ya siku 40 walikuwa wakilumbana kuhusu kanuni na muundo wa Serikali.
Alisema kuliko kuendelea kupoteza fedha, kwa kuwalipa wabunge wanaolumbana kwa mambo yanayojadilika, ni bora fedha hizo zikapelekwa katika sekta zingine za maendeleo.
Akizungumzia muonekano wa Bunge hilo uliofikia hatua za baadhi ya wajumbe kuwakashifu waasisi wa Taifa, Mwigulu alisema: “Natamani siku moja niongoze Taifa hili, ili niwafundishe watu kuwa na adabu.”
Alisema katika mazingira ya kawaida inawezekana watoto wakatukanana, lakini litakuwa jambo la ukosefu wa adabu kama mtoto atamtukana baba yake.
“Hawa watu wanaojiita Ukawa hawana adabu, wanapaswa kufundishwa adabu, ni jambo la kushangaa wanapoachwa tu wawatukane waasisi wa Taifa hili,” alisema.
Jana katika maziko ya Shida, ambaye pia alikuwa mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wa kuteuliwa na Rais, Zitto aliwataka wajumbe wenzake kumuenzi mama yake kupitia viongozi wao, Mwenyekiti wa Kamati namba nane,  Job Ndugai na Mwakilishi wa Ukawa, Profesa Ibrahimu Lipumba.
Alitoa ujumbe huo nyumbani kwa marehemu mama yake, mtaa wa Kisangani Mwanga, muda mfupi kabla ya kwenda makaburi ya Rubengela mjini Kigoma ambako mwili wa Shida Salum ulizikwa.
Zitto alisema kama kweli viongozi hao wanataka kumuenzi mama yake, wamalize tofauti zao na kulifanya Bunge Maalumu la Katiba, kuendelea na shughuli yake ya kuwaletea Watanzania Katiba itakayowafaa kwa muda mrefu.
Alisema kuwa mama yake alikuwa mjumbe wa Bunge hilo  baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, nafasi ambayo ingempa fursa ya kuandika historia ya kuwa mmoja wa wajumbe wa Bunge hilo, katika kuandika Katiba mpya ya Tanzania. 
Hata hivyo, alisema kwa kuwa mama yake aliugua na Mwenyezi Mungu kwa kudra zake akamuondoa katika nafasi ya kuandika historia hiyo, kilichobaki ni viongozi na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kufikia maridhiano na kuandika Katiba hiyo. 
Zitto alisema amejitahidi kwa kadri ya uwezo wake kumsaidia mama yake kupata matibabu ambayo yangerudisha afya yake, na kumpa fursa ya kushiriki katika shughuli zake za kawaida, lakini Mungu alipitisha uamuzi wake ambao hakuna wa kumpinga. 
Naye Ndugai, ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyeongoza wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye maziko hayo, alisema Shida alikuwa mtetezi wa Watanzania wa hali ya chini. 
Alisema yaliyotokea ni mapenzi ya Mungu na kuitaka familia  wasihuzunike kiasi cha kupitiliza, badala yake wakae pamoja na kuweka familia pamoja na kusonga mbele katika utekelezaji wa majukumu yao ya Taifa. 
Naye Profesa Lipumba, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, alisema kuwa Shida alisimama kuwapigania watu wenye ulemavu mchango ambao alikusudia kuutoa kwenye Bunge Maalumu la Katiba. 
Hata hivyo Lipumba alionya kuwa kama kweli watu wana nia ya kumuenzi Shida, hawana budi kusikiliza maoni ya wananchi walio wengi katika kuipata Katiba mpya, badala ya watu wachache kutaka kuichakachua. 
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila alisema Mkoa wa Kigoma, umekuwa na vyama mbalimbali vya siasa vyenye wabunge lakini mama yake Zitto, alikuwa mstari wa mbele kuwaunganisha kuwa wamoja kwa ajili ya maslahi ya Mkoa wa Kigoma na watu wake. 
Katika maziko hayo Chadema, iliwakilishwa na Mbunge wa   Nyamagana, Ezekiel Wenje, ambaye alisema kuwa Shida  alikuwa kiongozi aliyesimamia anachokiamini wakati wa vikao vya Kamati Kuu na mikutano mbalimbali ya Chadema. 
Maziko hayo pia yalihudhuriwa na Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi, James Mbatia, Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM), Mbunge wa Kasulu mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), Mbunge wa Nkasi, Ally Kesi (CCM), Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage (CCM), Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa (CCM). 
Mkoa wa Kigoma uliwakilishwa na Mkuu wa Mkoa, Issa Machibya na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa, Dk Walid Aman Kabourou, ambapo Mkuu wa Mkoa alisema kuwa amefarijika kuona mamia ya watu kutoka pande mbalimbali za nchi, wakihudhuria maziko ya Shida jambo linaloonesha kwamba alikuwa mtu aliyeishi na watu na kuwa msaada mkubwa kwao.

No comments: