TOTOO ZE BINGWA AAMUA KUJIWEKA KANDO KILI MUSIC AWARDS

Tuzo za muziki Tanzania 'Kili Music Awards' zimepata pigo jingine baada ya mwanamuziki mashuhuri wa dansi na rapa, Totoo Ze Bingwa kutangaza kujiondoa kwenye tuzo hizo.
Katika taarifa yake aliyoisambaza kwenye ukurasa wake wa Facebook, Totoo amesema haoni haja tena ya kushirikishwa kwenye tuzo hizo baada ya kutoambulia chochote kwa kipindi cha miaka mitano aliyoshirikishwa.
Totoo ambaye ni kiongozi wa bendi ya Malaika amewaomba radhi mashabiki wake kwa uamuzi wake huo na kuwataka wamuelewe kwanini kafikia uamuzi huo.
Ujumbe wake ulisomeka hivi: "Najaribu kujiuliza ni kwa nini nashirikishwa kili music awards cpati jibu haki ya mungu kwa heshima ya mashabiki wangu naomba kama kutakua na uwezekano nisishirikishwe tena mara 5 ni miaka mitano nimechoka kuzalilishwa."
Kwa kipindi kirefu sasa kumekuwa na mlolongo wa wasanii wa muziki wa aina mbalimbali ambao wamekuwa wakilalamikia Tuzo hizo na baadhi yao kutangaza kuomba wasishirikishwe katika kinyang'anyiro hicho kwa madai ya kutotendewa haki ama kuandaliwa washindi kabla ya onesho hilo.
Mbali na hilo, madai yao yameonekana kuwa na uzito hasa kwa kuzingatia jinsi shindano lenyewe linavyoendeshwa na hata wakati mwingine mshiriki mmoja kushinda tuzo zaidi ya tano.
Katika shindano la mwaka huu, msanii wa bongofleva, Naseeb Diamond alijizolea tuzo saba katika 'category' zote saba alizoshirikishwa.

No comments: