MLIBERIA ALIYEKAMATWA NA HEROIN ANYIMWA DHAMANA

Raia wa Liberia, Deocntee Togbah (28) anayekabiliwa na mashitaka ya kuingiza dawa za kulevya aina ya heroin, zenye thamani ya Sh milioni 38, amenyimwa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hakimu Mkazi Waliarwande Lema alimnyima dhamana mshitakiwa huyo, kwa kuwa mashitaka yanayomkabili hayana dhamana na Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Kesi imefunguliwa katika Mahakama hiyo kwa hatua za awali na upelelezi ukikamilika, itahamishiwa Mahakama Kuu kuanza kusikilizwa.
Togbah anatuhumiwa Aprili 25, mwaka huu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere,  aliingiza  gramu 862.3 za dawa hizo za kulevya zenye thamani ya Sh milioni 38.803.
Upande wa mashitaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa ili wakamilishe upelelezi.
Mshitakiwa hakuruhusiwa kujibu mashitaka yake na kurudishwa rumande hadi Mei 12, mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena.

No comments: