MGOMO WA DALADALA WALETA USUMBUFU KIGOMA

Mgomo mkubwa wa daladala umefanyika mjini Kigoma jana baada ya wamiliki na wafanyakazi wa mabasi hayo kupinga Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) kukamata wafanyakazi wa mabasi hayo wasio na sare rasmi.
Hali hiyo imesababisha adha na usumbufu mkubwa kwa wakazi wa manispaa ya Kigoma Ujiji na vitongoji vyake.
Wakizungumza na waandishi wa habari, Katibu Msaidizi wa Chama cha wamiliki wa mabasi ya daladala Kigoma (KIBOA), Hussein Kalyango  na  Mjumbe wa kamati ya utendaji ya chama hicho, Shadrack Evarist na mmiliki wa daladala, walisema kuwa walishakutana KIBOA na SUMATRA na kukubaliana kusogeza mbele tarehe ya kuanza kwa sare mpya iliyopaswa zianze kuvaliwa Aprili 10 mwaka huu, lakini wameshangaa ukaguzi kuanza ghafla.
Walisema katika mazungumzo yao walikubaliana kwamba wale ambao wameshalipia kiasi cha Sh 56,000 kwa KIBOA waliochukua zabuni ya kutengeneza sare lakini SUMATRA wamekataa kukubaliana na hali hiyo na kutaka sare hizo zianze kuvaliwa leo.
Akizungumzia mgomo huo na madai hayo ya wamiliki wa mabasi ya daladala, Meneja wa SUMATRA mkoa Kigoma, Adam Mamilo alisema waliwapa wamiliki wa mabasi ya daladala miezi mitatu kuhakikisha wanakuwa na sare mpya za suti.
Hata hivyo, muda mfupi wakati mgomo huo ukiendelea Kamanda wa Polisi Mkoa Kigoma, Fraisser Kashai alieleza kuwa amepata maagizo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa Kigoma, Issa Machibya kwamba atakutana nao leo na hivyo wasitishe mgomo na kuendelea na utoaji huduma hadi hapo watakapokaa na kupata suluu ya madai yao.

No comments: