WASSIRA ACHEKESHA WAOMBOLEZAJI KWENYE MSIBA WA RC TUPPA...

Stephen Wassira.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira alisababisha kicheko kwa waombolezaji katika maziko ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Gabriel Tuppa baada ya kulalamikia masharti yanayoambatana na safari ya kwenda peponi.

Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya wabunge wa mkoa wa Mara katika Ibada ya Maziko iliyofanyika nyumbani kwa marehemu Tuppa, Kilosa mjini, Morogoro, Wassira alisema watu wote waliohudhuria hapo wanataka kwenda peponi lakini tatizo ni masharti yanayoambatana na safari hiyo.
"Baba Askofu Mkude (Telesphor), ukiuliza nani anataka kwenda peponi, wote hapa watanyoosha mikono, lakini tatizo ni masharti yanayoambatana na safari ya kwenda huko. Kila mtu anaona ugumu wa hayo masharti ukiwemo wewe Baba Askofu," alisema Wassira huku umati uliokuwepo ukiangua vicheko.
Alisema kifo hakizoeleki wala hakizuiliki na kwamba hakuna anayeweza kuchakachua siri ya Mungu kuhusu uhai wa maisha ya wanadamu. Wassira pia alitumia fursa hiyo kuwaombea wafiwa wapate faraja katika kipindi hicho kigumu.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, jana jioni akizungumza na waombolezaji wakati wa ibada hiyo, alisema amemfahamu Tuppa tangu mwaka 1993 alipoteuliwa kuwa mkuu wa wilaya kwa mara ya kwanza.
"Tuppa alikuwa mtumishi Serikalini kwa muda wa miaka 42 na katika muda wote huo, miaka 21 ya utumishi wake alikuwa akihudumia wananchi kama Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa. Alikuwa mtu mwema, aliyejali watu na wala hakuwa na tamaa za hovyo hovyo," alisema Waziri Mkuu na kuongeza.
"Kumpoteza mume na baba ni mtihani mkubwa lakini mkimtumaini Mwenyezi Mungu mtafaulu," alisema Waziri Mkuu na kuwasihi mjane wa marehemu Tuppa pamoja na watoto wasisononeke wanapopatwa na jambo na wasisite kumuona Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, yeye binafsi au Rais Jakaya Kikwete, kwa msaada zaidi.
Awali, katika Ibada ya Misa, Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro, Telesphor Mkude aliwataka watu waliohudhuria maziko hayo kufanya toba kama njia ya kuleta mabadiliko kwenye maisha yao.
"Ninawaomba kila mmoja mahali hapa afanye toba, awe mkweli, asifanye uchakachuaji... kila mtu kwa imani yake aache mabaya na atende mema kama ndugu yetu John Tuppa ambaye alijitoa na kufanya zaidi kwa ajili ya wengine.
"Je, mnawaongozaje watu katika ofisi zenu katika ngazi mbalimbali, iwe ni wizarani, mkoani, wilayani hadi kwa mtendaji wa kijiji? Je, unawafanyaje watu katika biashara unayofanya? Je, unawadhalilisha kwa kuwauzia vitu vibovu? Je, unawauzia dawa za kulevya?" alihoji Askofu Mkude.
Aliwataka watu kila mmoja kwa imani yake kuendelea kuombea mchakato wa Katiba ipatikane Katiba bora zaidi.
"Tuna wajibu kama wacha Mungu tuwaombee wajumbe wa Bunge Maalumu ili kazi ile ifanyike sawa na mapenzi ya Mungu. Tusipowaombea watafanya vitu vya ajabu," alisisitiza.
Maziko hayo yalihudhuriwa pia na Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal, baadhi ya mawaziri, wabunge wa Mara na Morogoro, wakuu wa mikoa mbalimbali, viongozi wa dini na viongozi wa vyama vya siasa.
Tuppa alizaliwa Januari mosi, 1950. Amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya za Chunya, Mwanga, Bukoba, Muleba na Dodoma kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara mwaka 2011. Ameacha mjane, watoto watano na wajukuu watano.

No comments: