WABUNGE SASA KUANZA KUPITIA RASIMU YA KATIBA, KANUNI ZAWEKWA KIPORO...

Wajumbe wa Bunge la Katiba.
Bunge Maalumu la Katiba linaendelea na kikao chake na miongoni mwa shughuli zinazotarajiwa kufanywa  kuanzia leo, ni kurekebisha baadhi ya kanuni za uendeshaji wake na kuanza kujadiliwa kwa ibara zilizopo ndani ya rasimu ya Katiba.

Pamoja na  kazi hiyo ya kufanyia marekebisho kanuni za Bunge, Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo Maalumu la Katiba, Samia  Suluhu Hassan akiahirisha kikao cha Bunge  juzi, alisema leo Bunge  litaanza kazi ya kupitia rasimu ya Katiba  kwa kuanza na Sura ya Kwanza na Sura ya Sita.
Sura ya Kwanza inazungumzia muundo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na  ya Sita inazungumzia masuala ya Muungano.
Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, mjadala kuhusu Kamati ya Bunge utafanyika kwa muda usiozidi siku mbili na baada ya mjadala, kila Kamati itaandaa taarifa kuhusu mambo yaliyoafikiwa na wajumbe walio wengi kwa ajili ya kuwasilishwa kwenye Bunge Maalumu.
Kanuni hizo zinasema endapo kutakuwa na wajumbe ambao hawakuunga mkono maoni ya wajumbe walio wengi katika Kamati, wajumbe hao wanaweza kuandaa maoni yanayohusu maeneo ambayo hawakukubaliana nayo na yatajumuishwa kwenye taarifa ya Kamati.
Baada ya Kamati kuandaa taarifa yake, Mwenyekiti wa Kamati inayohusika atamjulisha Mwenyekiti kwa maandishi kuwa Kamati imekamilisha kazi yake.
Kwa mujibu wa kanuni, keshokutwa wenyeviti wa Kamati 12 za Bunge hilo Maalumu la Katiba sasa wanatarajia kuwasilisha taarifa za kile walichojadiliana katika sura namba moja na sita za rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalumu.
Baada ya jaribio la awali kutaka baadhi ya kanuni kurekebishwa kugonga mwamba  wiki iliyopita,  sasa azimio lenye lengo hilo litawasilishwa leo.
Jaribio la awali lilishindikana baada ya wabunge  wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kupinga mpango wa kutaka kanuni hizo kurekebishwa wakati hazijaanza kutumika, wakisema ni mbinu za kutaka kuwadhoofisha.
Walitaka kanuni  za 37 na 38 pekee ambazo ziliwekwa kiporo ndizo zijadiliwe.
Ukawa kupitia kwa Mwanasheria wao, Tundu Lissu, ulipinga jaribio hilo hata kabla ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge hilo, Pandu Ameir Kificho kusoma azimio hilo ndani ya bunge wiki iliyopita, huku Lissu akiita karatasi iliyokuwa na mapendekezo hayo kuwa ni 'takataka'.
Kutokana na mzozo huo, Mwenyekiti wa Bunge hilo Samuel Sitta alilazimika kuagiza Kamati  ya Kanuni kuahirisha uwasilishaji wa Azimio la Marekebisho hayo ya kanuni wamalize kwanza utata ulioibuliwa na Ukawa; ambao ulisababisha kikao cha Bunge kuahirishwa kutokana na vurugu.
Taarifa zilizomfikia mwandishi, zilisema baada ya kutafakari kwa kina na kupitia kwa Kamati ya Maridhiano, Ukawa wamekubali kufanyiwa marekebisho kwa baadhi ya kanuni baada ya kuonekana kuwa baadhi zinawabana wabunge katika ushiriki wao kwenye vikao vya Bunge na hata kwenye vikao vya Kamati.
Alhamisi iliyopita Mwenyekiti Sitta alitangazia wajumbe kwamba kwa vile marekebisho ya kanuni yalikwama, sasa  Kamati zitaendesha mijadala kwa kutumia kanuni zile zile za Bunge Maalumu.
Agizo hilo la Sitta lilionekana kuwa mwiba kwa wabunge wengi,  ambapo kanuni ya 32 inawabana kuvaa  mavazi rasmi, mjumbe kusimama anapotaka kutoa hoja hata kama wako wachache na vikao vya kamati vitalazimika kuanza saa tatu asubuhi hadi saba mchana na baadaye saa 10 jioni hadi saa mbili usiku, kama ilivyo kwa vikao vya Bunge, jambo ambalo limeonekana kuwa ni mwiba mkali.
Hata hivyo inadaiwa baadhi ya kanuni zilizotakiwa awali kuwasilishwa kwa marekebisho, hazitakuwepo kutokana na makubaliano yaliyofikiwa ikiwemo kanuni inayohusu uamuzi kupitishwa kwa theluthi mbili  za pande zote mbili za Muungano ili utaratibu wa kutumika uwe wa wingi wa kura.
Kanuni nyingine ambayo pia ilikuwa ifanyiwe marekebisho na baada ya mashauriano hayo itabaki kama ilivyo, ni ya 32(1) ambayo inasema kila Kamati itajadili rasimu ya Katiba kwa wakati mmoja kwa kuzingatia mgawanyo wa sura mbili za rasimu kwa mujibu wa ratiba itakayopangwa na Kamati ya Uongozi.
Hatua hiyo inaondoa mpango aliotangaza Mwenyekiti Sitta wiki iliyopita kwamba Kamati zitabadili kanuni hiyo ziweze kujadili kanuni tatu tatu au nne nne, suala ambalo lilipingwa na Ukawa ukidai msingi wake unalenga katika kujadili sura nyingi kwa pamoja jambo litakaloondoa umakini.

No comments: