SHIVJI AONYA BUNGE LIKIPITISHA SERIKALI TATU HAKUNA MUUNGANO...

Profesa Issa Shivji.
Gwiji wa masuala ya sheria za katiba nchini, Profesa Issa Shivji amewataka vijana kujiepusha na wanasiasa wenye uchu wa madaraka ambao kwa sasa wanang'ang'ania muungano wa serikali tatu ili kukidhi matakwa yao.

Akiwasilisha mada yake katika kongamano la vijana jijini Dar es Salaam jana, Profesa Shivji ambaye alisema kwamba yeye ni muumini wa muungano wa serikali mbili, alisema kama Bunge Maalumu la Katiba litapitisha rasimu ya serikali tatu, hakutakuwa na muungano.
"Kama mtaendelea kutaka utambulisho wa Tanganyika, tutauzika Muungano na utaifa wetu, kwa kufanya hivyo tutakuwa tumetekeleza matakwa ya wanasiasa wachache wenye uchu wa madaraka," alihadharisha Profesa Shivji.
Alisema rasimu ya katiba ya sasa inatishia kuwagawa wananchi wa Tanzania Bara na Visiwani, hali ambayo inaviza ukuaji mzuri wa muungano kwani kila upande unaona kwamba unaonewa kwa kunyimwa haki zake.
Mtaalamu huyo wa sheria za katiba alisema pamoja na kuamini kwamba Tume ya Mabadiliko ya Katiba (CRC) ilikuwa na nia njema, suala la serikali tatu  litasababisha mparaganyiko zaidi, badala ya utulivu uliokusudiwa.
Kongamano hilo ambalo limeitishwa wakati taifa linajipanga kusherehekea miaka 50 ya Muungano, limekusanya vijana zaidi ya 300 kutoka vyuo vya elimu ya juu Tanzania Bara na Visiwani na linajadili masuala ya muungano.
Profesa Shivji alisema kwamba pamoja na kuwa kuna mambo mengi ambayo anadhani yanatakiwa kufanyiwa marekebisho ili kuimarisha muungano, yeye hakubaliani na mfumo wa serikali tatu kwani hautasaidia kuondoa matatizo na kuimarisha muungano bali kuuvunja.
Alisema watu hawapaswi kufikiria idadi ya serikali ili kuufanya muungano ushamiri, lakini wanapaswa kuangalia demokrasia, kwa kuja na muundo ambao utaangalia changamoto na mahitaji ya muungano bila kuuvuruga na kuuweka katika hatari ya kuvunjika.
Naye Profesa Gaudens Mpangala akiwasilisha mada yake kuhusu wajibu wa vijana katika kuimarisha muungano, aliwataka vijana kuuchambua muungano kama unavyozungumzwa na wanasiasa kwa kuangalia manufaa na ubaya wake.
Akifungua kongamano hilo, Mkurugenzi anayeshughulikia maendeleo ya vijana Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, James Kajugusi, alisema kwamba wameitisha kongamano hilo ili kuwapa vionjo muhimu vijana kuhusu muungano, kwani wana wajibu maalumu wa kuuimarisha.

No comments: