ZITTO AWASILISHA MUSWADA BINAFSI KUFUTA SHERIA YA MAGAZETI...

Kabwe Zitto.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto amewasilisha kwa Katibu wa Bunge muswada binafsi kufuta Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, Zitto alisema ameamua kutumia njia za kawaida za kuwasilisha muswada na kuepuka njia ya dharura ili kujenga mazingira ya wadau wa habari kushiriki vya kutosha katika mabadiliko yanayotakiwa.
"Njia ya dharura ni ya haraka, lakini huziba fursa za kupata maoni ya wadau ambao kimsingi ndio wenye sheria yenyewe haswa, hivyo nimepeleka muswada leo ili uchapwe kwenye gazeti la Serikali (GN) kwa mujibu wa kanuni za Bunge, kisha usomwe kwa mara ya kwanza," alisema Zitto.
Aidha alisema juhudi za kutaka kufuta sheria imefanywa na wadau wa tasnia ya habari kwa muda mrefu sana na wakati umefika kuwasaidia kwa manufaa ya taifa.
"Kwa muda mrefu tumewaangusha wanahabari kwa kutosukuma vya kutosha mabadiliko waliyokuwa wanayapigania. Hata hivyo, kuna msemo wa kihindi 'asubuhi huanza pale unapoamka'. Sasa tuchukue hatua za kufuta sheria hii kandamizi," alisema Zitto.
Alisema yeye kama Mbunge anashawishi kwa sababu taratibu za kuandika sheria zinataka ama Serikali, Kamati ya Bunge au Mbunge kuwasilisha muswada.

No comments: