WANASIASA WAIPA WAKATI MGUMU TUME YA MABADILIKO YA KATIBA...

Jaji Joseph Warioba.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amewaambia wanasiasa wajadili  rasimu iliyotolewa badala ya kujadili Tume au wajumbe wake.

Jaji Warioba alisema jana Tume yake imekuwa ikifanya kazi katika mazingira magumu kutokana na kauli za wanasiasa ingawa amesema wanafarijika na kauli za kutia moyo wanazozipata kutoka kwa wananchi wa kawaida.
Warioba ambaye amesema haamini kuwa kauli za viongozi hao wa kisiasa ndiyo misimamo ya vyama vyao, alisema “Nadhani wangezungumzia rasimu wangetusaidia sana, badala ya kuzungumzia Tume na watu.”
Jaji Warioba alikuwa akitoa ufafanuzi kuhusu kauli mbalimbali zilizotolewa na baadhi ya wanasiasa zikituhumu Tume kuingilia uhuru wa wananchi wa kutoa maoni kuhusu Katiba mpya katika mikutano ya Mabaraza ya Katiba ya Wilaya iliyomalizika hivi karibuni.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana , Jaji  Warioba alisema  siku zote Tume yake imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na kuwataka wanasiasa hao kujadili rasimu iliyotolewa badala ya Tume au wajumbe wake.
“Moja ya kazi za kisheria za Tume ni kutoa elimu kwa umma, na ni kazi ya wakati wote,” alisema Jaji Warioba wakati akijibu swali la waandishi waliofika ofisini kwake kutaka ufafanuzi wa kauli ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo.
 Bulembo amenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari juzi na jana akiwa mkoani Tanga akisema Tume ya Warioba imeacha kutekeleza majukumu yake na kuingilia uhuru wa wananchi wa kutoa maoni.
Kwa mujibu wa Warioba,  katika mikutano ya Mabaraza ya Katiba ya Wilaya, wananchi ambao walikuwa ni wajumbe wa Mabaraza hayo walikuwa na fursa ya kuuliza maswali na Wajumbe wa Tume walitoa elimu kuhusu hoja na maswali yaliyoulizwa kwa mujibu wa sheria.
“Sasa anaona ( Bulembo) kuwa kutoa elimu ni dhambi,” alisema Jaji Warioba aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri Mkuu.
Jaji Warioba pia  alikumbusha kauli yake: “Nilisema mwishoni mwa mwezi uliopita, wanasiasa wamekuwa wakitoa matamshi yaliyoifanya kazi ya Tume kuwa ngumu katika mikutano ya Mabaraza ya Katiba,” alisema na kuongeza:
“Matamshi mengine yalilenga Tume na wakati mwingine yalinilenga mimi binafsi au wajumbe wa Tume badala ya kuzungumzia rasimu,” alisema Mwenyekiti huyo anayeongoza  tume hiyo yenye wajumbe 32.
Kwa mujibu wake, Tume yake siku zote imekubali kukosolewa kwa kuamini kuwa kukosolewa ni jambo la kawaida, lakini akaongeza kuwa ni vema wananchi na wanasiasa wakajadili Rasimu ya Katiba iliyotolewa badala ya watu au Tume.

No comments: