BASI LAPOROMOKA KWENYE KORONGO KINA CHA FUTI 260 NA KUUA ABIRIA 19...


Takribani watu 19 - wakiwamo watoto wadogo wawili - wamekufa wakati basi lililokuwa likisafiri kutoka mji mkuu wa Lima, nchini Peru kwenda jimbo la kijijini kusini mwa nchi hiyo lilipojibamiza kwenye mwamba mwishoni mwa wiki.
Watoto wawili, wenye umri wa mwaka mmoja na miaka mitatu, pamoja na watu wazima 17, walikufa wakati basi hilo liliposerereka kwenye mwamba na zaidi ya futi 260 chini katika mteremko mkali huko Huancavelica, kusini mwa Peru. Watu wengine 25 walijeruhiwa, kwa mujibu wa maofisa.
Basi hilo lilikuwa limebeba abiria 55 wakati lilipoanguka kina cha futi 260, kwa mujibu wa ripoti. Dereva wa basi hilo alipelekwa hospitali baada ya kupata majeraha, imeripotiwa, hali yake haijafahamika.
Ajali hiyo ilitokea majira ya Saa 10:20 alfajiri ya Jumapili katika jamii ya wakulima kwenye wilaya ya Acoria ya mkoa wa Huancavelica takribani kilomita 246 (maili 152) kusini mwa Lima. Basi hilo lilikuwa limebakiza saa moja kufikia mwisho wa safari yake, kwa mujibu wa ripoti.
Abiria mmojawapo aliyenusurika amesema ajali hiyo imechangiwa na mwendokasi huku dereva akiongeza mwendo kwenye barabara nyembamba, yenye upepo mkali, kwa mujibu wa ripoti.
Video kutoka eneo la tukio imeonesha wananchi kadhaa wa eneo hilo wakikimbilia kwenye basi hilo, wakaligeuza juu upande wa kulia na kuanza kuwavuta abiria kutoka kwenye mabaki ya basi hilo.
Miili kadhaa imeweza kuonekana ikiondolewa kutoka kwenye eneo hilo lililovurugika, mingi kati ya hiyo ikiwa imelala chini na kufunikwa kwa mablanketi kando ya mteremko mkali.
Walionusurika walionekana wakilia, baadhi wakimshukuru Mungu kwa kuwanusuru, wengi wakitaka ndugu zao wafahamu bado wako hai.
Hali ya watu 25 waliojeruhiwa, kwa mujibu wa ripoti, haijafahamika, wengi wamehamishwa kwa ndege kwenda kwenye hospitali mbalimbali za mjini humo.
Ajali mbaya za basi zimekuwa zikitokea mara kwa mara nchini Peru, ambako uhamasishaji wa usalama barabarani ni dhaifu. Takwimu za Serikali zinasema watu 5,435 walikufa na 13,520 walijeruhiwa katika ajali za basi kati ya Septemba 2008 na Desemba 2012.

No comments: