WALIMU WAJAWAZITO WAOMBA LIKIZO YA UZAZI IANZE MAPEMA...

Walimu wajawazito, wameomba likizo ya uzazi ianze mapema wakiwa na ujauzito wa miezi saba, kwa kuwa wakati huo, wengi wao hushindwa kumudu kuandika ubaoni.

Walitoa ombi hilo hivi karibuni kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya, katika kikao kilichokutanisha walimu wa kike kutoka shule za msingi, vyuo vya Serikali na binafsi.
Malengo ya kikao hicho ilikuwa kujadili changamoto zinazowakabili walimu wa kike katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Mwalimu  Betilda Siyame wa Shule ya Msingi Chanji mjini hapa, alisema Serikali inapaswa kuanza kuwapa likizo ya  uzazi  walimu wajawazito wanapofikisha miezi saba.
Alisema wakati huo, matumbo ya walimu wengi huwa makubwa kiasi cha kushindwa hata kuandika ubaoni, kwa kuwa kabla hawajafikisha mkono kuandika, tumbo linagusa ubao na kushindwa kuandika.
"Mkuu wa Mkoa na wewe ni mwanamke mwenzetu, unajua vizuri tabu tunazopata tukiwa  na ujauzito kuanzia miezi minane au tisa, kwa kweli tunapata tabu sana na watoto wetu hawa wa kizazi kipya, baadhi wamekuwa wakitucheka tunavyohangaika.
"Hivyo tunaiomba Serikali ituruhusu kuanza likizo  ya uzazi mapema hata tukiwa na ujauzito wenye umri wa miezi saba  hivi, ili tupumzike tunapata shida sana mama," alisema Mwalimu  Betilda.
Mkuu wa Mkoa Manyanya alisema suala hilo la kuomba muda zaidi wa likizo ya uzazi, ni vizuri lijadiliwe katika maoni ya Katiba na likichukuliwa, litakuwa limepata majibu ya kudumu na halitakuwa kero tena.
Alitaka wawasilishe maoni kwa wajumbe wa mabaraza ya Katiba  ya wilaya, ili  yaboreshe uundwaji wa Katiba mpya nchini.
Mwalimu mwingine, Theresia Suwi alisema changamoto nyingine inayokabili walimu hao ni mishahara midogo, inayosababisha wajiingize kwenye mikopo iliyo na riba kubwa, hali inayosababisha kunyang'anywa kadi za benki na vitambulisho vya kazi mpaka wanapolipa deni.
Alisema baadhi ya walimu wamekuwa wakiishi kwa kujificha, wakikimbia madeni hayo, huku wengine wakiacha hata kufika kazini wakihofia wanaowadai, kwa kuwa wanawafuata hadi kazini hali inayochangia kutowajibika na kudidimiza kiwango cha elimu mkoani humo.

No comments: