MHADHIRI WA UDSM AUAWA KWA KUPIGWA RISASI...

Eneo la Magomeni, Dar es Salaam ambako mhadhiri huyo anasemekana alivamiwa na kupigwa risasi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Uhandisi  (COeT)  cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Patrick Rweyongeza (32), ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiofahamika. Aliuawa juzi jioni eneo la Magomeni, Dar es Salaam wakati akienda Kariakoo.

Kwa mujibu wa Ofisa Uhusiano wa UDSM, Jackson Isdory, Rweyongeza inasadikiwa alikuwa akienda Kariakoo kusimamia mradi unaoendeshwa na Taasisi ya Bico, iliyo chini ya CoET.
"Inaonesha majambazi hao walimvizia wakati akitoka Benki ya NBC Tawi la Ubungo ambako alikwenda kuchukua fedha kwa ajili ya kulipa vibarua kwenye mradi,” alisema Isdory wakati akizungumza na mwandishi.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alithibitisha kuwepo tukio hilo na kusema hakuna aliyekamatwa.
"Mhandisi Rweyongeza inadaiwa alikufa wakati akifikishwa Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokimbizwa kutokana na majeraha ya risasi,” Kamanda Wambura alisema.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, watu waliomvamia na kumpiga risasi, walikuwa kwenye pikipiki. Mhadhiri huyo alikuwa ndani ya gari  aina ya Toyota Opa lenye namba za usajili  T 170 BZG.
Rweyongeza alimaliza Shahada ya Uzamili ya Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Glasgow, Uingereza baada ya kuhitimu Shahada ya Kwanza ya Uhandisi katika  Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2007.
Msiba wa mhadhiri huyo upo eneo la Boko Mbweni na mwili wake unasafirishwa leo kwenda nyumbani kwao mkoani Kagera kwa maziko.

No comments: