MAWAZIRI NA WABUNGE WACHUNGUZWA KWA DAWA ZA KULEVYA....

Kamishna Godfrey Nzowa.
Jeshi la Polisi, Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, linazifanyia uchunguzi wa kina taarifa zinazotolewa na wadau mbalimbali za baadhi ya watu wakiwemo mawaziri, wabunge na  wafanyabiashara  kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Katika hatua nyingine, jeshi hilo limesema limechukua hatua mbalimbali katika kudhibiti kushamiri kwa biashara hiyo nchini, ambapo kiasi cha dawa zilizokamatwa kuanzia Januari hadi Julai mwaka huu, ni kidogo ikilinganishwa na cha mwaka jana.
Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya cha Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi (ACP), Godfrey Nzowa, alisema Dar es Salaam jana kwamba jeshi hilo limeongeza mbinu na mikakati ya kudhibiti biashara ya dawa za kulevya na kuonya kuwa wahusika wote watakamatwa na kupambana na mkono wa sheria.“Wapo baadhi ambao tayari tumewahoji na uchunguzi unaendelea. Ninachokiomba kwa wananchi ni kuwa wasitoe siri kwa kutumia mitandao ya kijamii, watume siri hizo kwetu moja kwa moja, maana taarifa zinapotoka kwenye mtandao wahusika wanapoteza ushahidi haraka,” alisema Nzowa ambaye katika kuthibitisha hilo alisema jeshi hilo tayari limemhoji Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan (CCM) kwa tuhuma za kujihusisha na biashara hizo.
Kamishna huyo wa Polisi alisema taarifa za kuwepo kwa wabunge, mawaziri na wafanyabiashara wakubwa wanaojihusisha na dawa za kulevya, zimekuwa zikifikia jeshi hilo kupitia vyanzo mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii na kwamba hazipuuzwi bali zinafanyiwa kazi kwa  nguvu kubwa.
Kuhusu Mbunge Azzan ambaye katika siku za hivi karibuni zimekuwepo taarifa za kudaiwa kujihusisha na biashara ya dawa hizo, Kamishna Nzowa alisema kwa kifupi; “Idd Azzan tumeshamhoji na uchunguzi unaendelea.”
Akizungumzia mafanikio  ya mwaka huu, Nzowa alisema kuanzia Januari hadi Julai, Polisi wamekamata kilo 32 za heroin, kilo 4 za kokeini, kilo 9,999 za bangi, kilo 6,628 za mirungi na kilo 11 za dawa mpya za kulevya aina ya ephedrine, zilizokuwa zikisafirishwa kwenda Afrika Kusini.
 Alisema katika  tukio la heroin watuhumiwa 44, kokeine watuhumiwa 18, bangi watuhumiwa 1,478, mirungi watuhumiwa 532 na ephedrine mtuhumiwa mmoja walikamatwa wakiwemo Wanaigeria watatu na wote wamefikishwa mahakamani kujibu mashitaka.
“Tunawashukuru wananchi wa mikoa mbalimbali ambao ndio waliotupa ushirikiano uliowezesha kuwakamata wahusika hawa wa dawa za kulevya ambazo ziliingizwa kupitia katika viwanja vyetu vya ndege na baharini,” alisema Nzowa.
Alisema vipo viashiria  vinavyoonesha kudhibitiwa kwa biashara hiyo moja ikiwa ni kupungua kwa kiasi ukilinganisha na takwimu za mwaka jana zilipokamatwa kilo 260 za heroin na 151 za kokeini, lakini pia kupanda ghafla kwa bei ya dawa hizo  kufikia Sh milioni 50 na milioni 55 kwa kilo moja.
Alisema vita dhidi ya dawa hizo si ya Tanzania pekee, bali dunia nzima ambapo viongozi wa mataifa mbalimbali ya ndani na nje ya Afrika wamekuwa wakikutana mara kwa mara kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na biashara hiyo ambayo inawahusisha watu wenye uwezo mkubwa sana wa kifedha.
“Sasa hivi tupo katika mikakati ya kuifanya sheria inayohusiana na dawa za kulevya kuwa inayojitegemea badala ya kuchanganywa na sheria nyingine, lakini pia tunataka kuweka adhabu kali kwa nchi zote ili mtu anapokamatwa katika nchi yoyote anakumbana na adhabu kali na si katika nchi nyingine adhabu kuwa ndogo.”
Alisema jeshi hilo limegundua pia kuwepo mbinu mpya za usafirishaji wa dawa hizo kwa kubadili vifungashio kutoka katika gundi ya karatasi (selotepu) ya awali na sasa kuwekwa katika  vifungashio  vinavyoonesha kuwa ni kahawa halisi, sukari na hata  kuzibadili dawa hizo kutoka katika unga na kuwa vimiminika.
“Mbinu zote hizi tumezibaini na kila kitu tunachokigundua tumekuwa tukielezana kimataifa kwani mkakati wa sasa ni kuhakikisha kuwa dawa hizi hazifiki kwa mtumiaji wa mwisho, zikamatwe zikiwa bado mikononi mwao bila kujali ni katika nchi gani.
“Kama vile Watanzania wanavyokamatwa kwenye nchi nyingine ndivyo sisi pia tunavyowakamata wafanyabiashara hawa haramu kutoka nchi za Pakistan, Iran na Brazil  hapa,” alisema.

No comments: