WANANCHI WALIA NA PETROLI, DIZELI, SIMU KWENYE BAJETI...

Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa.
Wananchi wa kada mbalimbali nchini wameendelea kutoa maoni yao kuhusu bajeti ya serikali iliyosomwa bungeni Alhamisi na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe, Shule ya Biashara, Paulo Kabelele alisema Bajeti inauma na kupuliza na italeta matokeo mazuri iwapo yote yaliyopangwa katika utekelezaji yanafikiwa kwa asilimia 100.
Alisema sekta ya usafiri imechukua uchumi na kwamba kupanda kwa petroli na dizeli kutaongeza gharama za maisha ambayo yategemea usafishaji wa bidhaa, abiria na nyinginezo.
“Ukipandisha bei petroli na dizeli tayari umeongeza gharama za maisha...kushusha mafuta ya taa si hoja sana kwani uchumi unaendeshwa na usafirishaji unaotegemea petrol na dizeli,” alisema Mhadhiri huyo.
Hata hivyo, alisema pamoja na Bajeti hiyo, suala kubwa ni kuwa kupanga ni kitu kingine na kutekeleza ni jambo lingine pia.
Hivyo alisema, iwapo utekelezaji wa Bajeti hiyo utafanyika kwa asilimia 100, matokeo ya kimaendeleo yataonekana  na kwamba kama haitatekelezwa kwa kiwango kinachohitajika, shughuli nyingi za kimaendeleo zilizopangwa kwenye wizara  hazitafikiwa kama ilivyokusudiwa.
Alitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kujipanga vilivyo kukusanya mapato kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo. 
“Hapa zinahitajika jitihada za makusudi kutoka TRA kwani kiwango ni kikubwa na wasipofikisha malengo hayo hata mgawo wa fedha kwenye wizara unakuwa ni wa chini, hivyo mipango yote iliyopangwa haitafikiwa,” alisema Mhadhiri huyo.
Pia alisema pamoja na wafadhili kuahidi kuchangia Bajeti, mara nyingi fedha hizo huchelewa kutolewa kwa wakati, kitendo kinachoweza kukamisha pia utekelezaji wa Bajeti
Hivyo katika maoni yake ya ujumla, alisema ili kufikiwa kwa malengo ya Bajeti hiyo, vipaumbele vielekezwe katika usimamiaji wa makusanyo ya mapato, matumizi sahihi ya mapato hayo na kwa maeneo yaliyolengwa, wafadhili nao walioahidi kuchangia Bajeti watoe fedha hizo kwa wakati na kwamba bila kutekelezwa hayo malengo yaliyowekwa hayatafikiwa.
Baadhi ya wasomi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ambao hawakupenda majina yao yatajwe, waliipongeza Bajeti hiyo, licha ya kusema kuwa ina kasoro nyingi zinazohitajika kusimamiwa vema wakati wa utekelezaji. Miongoni mwa maeneo hayo ni tozo la kodi ya matumizi ya M-pesa.
Walisema eneo hilo linatakiwa kuangaliwa katika utekelezaji wake hasa ikizingatiwa kuwa huduma za benki zitasambaa hadi vijijini ambapo huduma za mawakala wa kampuni za simu yamefanikiwa kufika.
Baadhi ya wananchi hasa wakulima walisema kupanda kwa mafuta kutaongeza gharama za uzalishaji mazao na hivyo kusababisha kupanda kwa bei.
Nao baadhi ya madereva wa bodaboda, wakizungumzia kuondolewa kwa kodi ya pikipiki na bajaji, walisema hatua hiyo itanufaisha wamiliki wa vyombo hivyo vya usafiri.
Baadhi wa madareva waliojitambulisha kwa majina ya Juma Hamisi na Petro Adrian, kwa nyakati tofauti walisema madereva wengi wa bodaboda hawana pikipiki wanazomiliki.
Hivyo, kuondolewa kwa ushuru huo watakaonufaika ni wamiliki, ambao ndio wenye pikipiki nyingi zinazotumika kusafirisha abiria mijini na vijijini.
“Matunda haya yananufaisha wamiliki wa usafiri huu, asilimia kubwa wenye kuwa na pikipiki mchana na usiku ni madereva, hawana hisa, wanalipwa ujira ... sasa unafuu huu unanufaisha wamiliki na wenzetu wachache wenye pikipiki zao au bajaji,” alisema hamis.
Hata hivyo, alisema iwapo serikali za wilaya na halmashauri zinawawezesha vijana kuunda vikundi vya ushirika vya usafiri na kuwakopesha mikopo ya kununua vyombo hivyo, kupitia utaratibu wa kuondolewa kwa kodi utaweza kunufaisha na wao kupitia vikundi hiyo.
Baadhi ya wakazi wa dodoma waliohojiwa, walisema bajeti kimsingi haijampa nafuu mwananchi wa kawaida kutokana na ongezeko la baadhi ya kodi hasa katika utumaji fedha kwa njia ya mtandao.
Mratibu wa mtandao wa asasi za kiraia Dodoma, Edward Mbogo alisema kimsingi Bajeti haitasaidia mtu wa hali ya chini kutokana na kuongezeka kwa kodi hasa katika masuala la kutuma fedha kwenye mtandao.
“Unapoweka kodi kwenye vitu muhimu gharama zinaongezeka,” alisema na kuongeza kuwa kuweka kodi kwenye masuala ya kuhamisha fedha kutaumiza watu wa hali ya chini ambao walishapata nafuu kuliko kwenda benki.
“Kuweka kodi kwenye kutuma fedha kwa njia ya  simu ni janga lingine, kwani watu wa kawaida wamekuwa wakisaidiana kwa fedha kidogo lakini unapotakiwa kulipa kodi katika kubeba mzigo huo watu wa chini uwezo wao ni mdogo,” alisema.
Mkazi wa Chinangali, Sospeter Msendekwa alisema Bajeti imelenga watu wenye nafasi zaidi kwani petroli inapopanda maana yake ni kupandisha bei ya kila kitu.
Alisema wakati wabunge wanajadili Bajeti hiyo waangalie vitu muhimu ambavyo vitasaidia wananchi.
Katibu Mkuu wa Kiislamu cha Dalai, Dodoma, Alhaj Rashid Bura alisema kupandisha bei ya mafuta ni kumbana mwananchi wa kawaida ambaye hana uhakika wa kipato.
Alisema mafuta yamekuwa yakitumika kwenye usafirishaji mazao, hali ambayo inaweza kusababisha kupanda bei kwa bidhaa za chakula.
Bura alitaka Serikali isiwe na vyanzo vya mapato vya aina moja ambapo kumekuwa na utegemezi wa mapato ya bia, sigara na vinywaji baridi, huku vyanzo vikubwa kama madini, utalii vikiachwa.
Kutoka Mwanza imeelezwa kuwa Bajeti inaumiza wafanyakazi licha ya kupunguziwa kodi ya asilimia moja na kupandisha bei ya mafuta.
Katibu wa Chodawu  wa Mkoa wa Mwanza, Athuman Zebedayo, alisema: “Hakuna jipya, kodi ya madini ilitakiwa ipande na wawekezaji kwenye mbuga za wanyama na watalii wanaotoka nje ya nchi nao waongezwe kodi badala ya wananchi kuendelea kubebeshwa mzigo.”
Alisema ilitarajiwa ingekuja na mapya na ubunifu lakini mambo yanaonekana kuwa yale yale ya kuumiza wafanyakazi na wakulima.
Aliongeza kuwa yawezekana pia Serikali ikapata shida ya kukusanya kodi kwa kuwa wanategemewa wafanyakazi zaidi kuliko wafanyabiashara. 
Adam Chagulani alisema ipo haja ya kubuni vyanzo vipya vya mapato badala ya kila siku kutegemea wanywaji na wavuta sigara.
Alisema Serikali inapaswa kuwezesha wakulima ili wakopesheke na kufanya kilimo kitumike ipasavyo katika kuchangia pato la Taifa kwani wananchi wana ardhi ambayo haijathaminishwa ili wapate hati.
Watu waliohojiwa Mbinga walitofautiana kuhusu ubora wa Bajeti hiyo wengine wakiiponda na wengine kuiunga mkono.
Waliofurahishwa walisema Serikali  imeonesha ukomavu kwa kusikia kilio cha wabunge kuongeza fedha za maendeleo.
Kauli hiyo ilielezwa na mtumishi wa umma, Geofrey Nghumbi ambaye hakupenda taasisi anayofanyia kazi ijulikane.
Nghumbi alisema anaona Serikali imeonesha kubana matumizi yasiyo ya lazima ili kutumia fedha nyingi inazokusanya kwa malengo iliyojipangia. Aidha, alisema inaonekana kumjali mfanyakazi hasa kwa kumpunguzia kodi ya mapato.
Katibu wa Mtandao wa Asasi Zisizo za Serikali wilayani Mbinga, Benedict Rwena, aliikosoa akisema inaonesha imemtupa mwananchi wa kawaida.
Alisema katika uchambuzi wake, Bajeti haileti matumaini kwa Mtanzania wa kawaida na badala yake imependelea wageni hasa wawekezaji wakubwa.
Alisema wananchi wataendelea kubanwa na mfumuko wa bei kutokana na kuongezeka kwa gharama za usafirishaji na hivyo chakula.
Martina Mgimba aliiomba Serikali kupunguza kodi ya mapato katika biashara ndogo ili kuendelea katika miradi yao. Aidha aliitaka kufikiria upya tozo kwenye simu kwa kutoza kampuni husika na si watumiaji wa huduma.

No comments: