Samuel Sitta. |
Kaimu Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta jana aliepusha hatari ya kuzuiwa kwa bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi bungeni.
Hatua hiyo ilikuja baada ya wabunge kuichachamalia Serikali wakiitaka kuongeza fedha kwenye bajeti hiyo kwa kutokubaliana na kutengwa kwa Sh bilioni 47 kwa ajili ya shughuli za wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha.
Tangu juzi baada ya Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo alipowasilisha hotuba hiyo bungeni, wabunge waliopata nafasi ya kuchangia walililamikia kiasi hicho cha fedha wakisema ni kidogo.
Wabunge hao walisema Serikali kuendelea kupunguza fedha zinazoelekezwa kwenye wizara hiyo mwaka hadi mwaka kunatia shaka, kwamba haithamini wafugaji na wavuvi nchini na hivyo walitishia kukwamisha bajeti hiyo kama Serikali haitaongeza fedha.
Mbunge wa Mji Mkongwe, Mohamed Ibrahim Sanya (CUF) ndiye alikuwa ‘mwiba’ alipong’ang’ana kushikilia shilingi kutoka kwenye mshahara wa Waziri Mathayo, huku akisema atahakikisha Waziri anarejea Dar es Salaam kwa miguu.
Pamoja na Sanya, wabunge wengine waliolalamika ni wanaotoka jamii ya wafugaji, Mbunge wa Ngorongoro, Kaika Telele (CCM) na wa Longido, Lekule Laizer (CCM) ambao walisema ingawa wafugaji ni watu muhimu, lakini Serikali imekuwa haiwajali na kuwafanya waishi kwa shida ndani ya nchi yao.
Telele alisema bajeti kwa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikipunguzwa kwa wastani wa Sh bilioni 15 kila mwaka na katika kipindi cha miaka mitano kiasi kilichopunguzwa ni zaidi ya Sh bilioni 160, hatua aliyosema inakwamisha utendaji kazi wa wizara hiyo.
Kutokana na hasira za wabunge, Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama jana wakati wa majumuisho, alimwomba Waziri Sitta aliyekuwa akikaimu nafasi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyeko safarini, kutoa kauli ya Serikali juu ya maombi ya wabunge wengi ya kutaka wizara hiyo kuongezwa fedha ili wabunge wasikwamishe mshahara wa Waziri.
Sitta aliliambia Bunge kwamba kutokana na malalamiko ya wabunge Serikali imesikia na kukubali kuongeza fedha katika bajeti hiyo.
“Kutokana na malalamiko yenu wabunge kuanzia jana tumekuwa tunahangaika kutafuta fedha ili kuongeza kwenye bajeti. Labda niwaambie kilichojificha nyuma ya pazia … kwa vile Rais yuko Tokyo (Japan), Waziri Mkuu yuko Dar es Salaam na Waziri wa Fedha yuko nje ya nchi pia, nilimwomba Naibu Waziri Mkuya (Saada), ambaye alihangaika kutafuta fedha hizo na kufanikiwa kupata Sh bilioni 20.
“Lakini hizi Sh bilioni 20 hazitoshi, tulitaka tutafute kiasi chote cha fedha kilichoombwa kuongezwa na wabunge (Sh bilioni 40), lakini kwa vile hawa viongozi wote hawapo ambao wangeweza kutusaidia kujua tujibane wapi ili fedha hizo zipatikane, tutaendelea kulifanyia kazi suala hilo ili fedha zaidi zipatikane, na zitaonekana kwenye bajeti ya Wizara ya Fedha,” alisema Sitta.
Majibu hayo ya Waziri Sitta yalionekana kuridhisha wabunge ambao waliamua kupitisha bajeti hiyo huku Waziri Mathayo akimshukuru Sitta kwa jitihada zake.
No comments:
Post a Comment