Maalim Seif Sharif Hamad. |
Wakati Rasimu ya Katiba mpya ikitarajiwa kuzinduliwa leo, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ameonesha dhahiri kutoridhishwa na Muungano na kusema wakati umefika sasa kwa Wazanzibari kudai haki ya kuwa na Dola kamili.
Aidha, Maalim Seif amesema Tume ya Maridhiano ya Zanzibar imependekeza mambo 10 ambayo Zanzibar inataka yaondolewe katika orodha ya Muungano ikiwamo Zanzibar kuwa na uraia wake pamoja na mambo ya fedha na sarafu.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa wafuasi wa CUF Kibanda Maiti mjini hapa jana, alisema Zanzibar ilikuwa Dola kamili Afrika Mashariki hata kabla ya Dola za Tanganyika pamoja na nchi nyingine licha ya kuwa na kiti katika Umoja wa Mataifa (UN) Desemba 16, 1963.
Alisema muundo wa sasa wa Muungano umekuwa ukiidhoofisha Zanzibar kiasi cha Muungano huo kuonekana kukosa tija kwa upande mmoja.
Akifafanua, alitoa masharti na akisema Katiba mpya inapaswa iwe na marekebisho makubwa katika mambo ya Muungano, ikiwa ni pamoja na suala la uraia na jina lenyewe la Muungano.
Maalim alisema Zanzibar sasa inataka kuwa na uraia wake kamili ambapo itakuwa na uwezo wa kutoa hati zake za kusafiria.
“Zanzibar itakuwa na hati zake za kusafiria ambapo mambo ya Uhamiaji hayatakuwa ya Muungano tena…Tanganyika watakuwa na hati zao Zanzibar na zake,” alisema.
Aidha, alipinga jina la muundo wa Muungano wa sasa kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusema Zanzibar inataka jina la Muungano liwe Muungano wa Jamhuri za Tanzania.
Alisema mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa sasa yanatakiwa yawe chini ya milki ya Zanzibar ambapo itakuwa na sifa za kutambuliwa kimataifa na kujiunga na mashirika ya kimataifa.
“Kabla ya Muungano, Zanzibar ilikuwa na ofisi za kibalozi katika nchi mbali mbali ikiwamo Marekani, Uingereza na Misri,” alisema.
Aliongeza kuwa anataka kuiona bendera ya Zanzibar ikipepea New York kwenye makao makuu ya UN pamoja na Jumuiya ya Madola na Umoja wa Afrika (AU) jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Maalim aliiponda bendera ya sasa ya Zanzibar akisema haipendezi, kwa kuwa bado inaonekana kuwa na sura ya bendera ya Muungano.
Aidha, alisema Zanzibar inatakiwa kuwa na sarafu, Benki Kuu yake na kuwa na uwezo wa kuamua masuala ya uchumi na fedha na mambo ya mikopo.
“Zanzibar hatufaidiki na fursa za fedha ikiwamo mikopo inayotolewa na taasisi za fedha bila ya idhini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano,” alisisitiza Maalim.
Alisema Zanzibar ni waanzilishi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), lakini akadai kuwa kwa bahati mbaya hivi sasa imekuwa ikiambiwa kwamba haikuhusika.
Kuhusu Polisi alitaka katika muundo mpya wa Muungano Zanzibar inapaswa kuwa na Jeshi lake hilo huku pia akitaka suala la mafuta na gesi na Baraza la Mitihani viondolewe kwenye orodha ya mambo ya Muungano.
Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF alitaka vyama vya siasa visiwe na sura ya Muungano na suala hilo nalo liondolewe katika orodha ya mambo ya Muungano kwani wakati zilipounganishwa nchi mbili vyama hivyo havikuwapo na mambo hayo yalikuja mwaka 1977 wakati kilipozaliwa chama kipya cha siasa cha CCM baada ya muungano wa TANU na ASP.
Alisema Rasimu ya Katiba mpya inatazamiwa kuzinduliwa kesho itapimwa na wananchi wa Zanzibar kwa matukio hayo muhimu ya mabadiliko ya Katiba.
Aliongeza kuwa Zanzibar itaendelea kudai mabadiliko hayo makubwa ya Katiba pamoja na mambo ya Muungano hadi dakika za mwisho.
Wakati hayo yakijiri, hivi karibuni Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi alisema Wazanzibari ndio wanaofaidika na Muungano kwa kufanya kazi zao za maendeleo na uchumi Bara bila usumbufu.
Akasema chokochoko zinazoibuliwa na baadhi ya wanasiasa kwa kudai kwamba Muungano haujasaidia Wazanzibari ni mbaya na madhara yake ni makubwa kwao.
Alisema ndiyo maana CCM imekuwa ikisisitiza kwamba itaendeleza sera ya Muungano wa Serikali mbili ambao umebainika kuwa na tija kwa wananchi wa pande mbili hizi.
Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Vuai Ali Vuai akaikana Tume anayoiegemea Maalim Seif katika hoja zake, ambayo inaongozwa na mwanasiasa mkongwe, Hassan Nassoro Moyo, akisema CCM haina taarifa ya kuwapo kwake kwani imejiunda bila baraka za chama hicho.
No comments:
Post a Comment