SABUNI YA UNGA YA KLIN YAPIGWA MARUFUKU KWA KUKOSA UBORA...

Baadhi ya pakiti za sabuni ya Klin.
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeagiza kuondolewa sokoni kwa sabuni ya unga iitwayo Klin, kwa sababu haina viwango vya ubora vinavyotakiwa.

Aidha, limeutaka umma ufahamu kuwa kiwanda kinachozalisha sabuni hiyo, Klin Soaps and Detergent Limited cha Dar es Salaam kilikwishazuiwa kuzalisha bidhaa hiyo tangu Juni 2012, kutokana na kushindwa kutekeleza matakwa ya leseni ya viwango vya ubora, hivyo kutonunua sabuni zake.
Mkaguzi wa ubora wa bidhaa wa TBS, Gervas Kaisi alisema Dar es Salaam jana kuwa maduka makubwa yanayofahamika kama Supermarkets ndio yanayo nunua na kusambaza zaidi sabuni hiyo wakati uzalishwaji, usambazaji na uuzwaji wake ulikwisha pigwa marufuku.
"Kiwanda hicho hata hakijulikani kilipo kwa sasa kwa sababu wahusika wana shughuli ya kuhama hama kutoka eneo moja kwenda jingine, ili kukwepa ukaguzi wa shirika letu. Hii ni hatari kwa kuwa walipojificha hawajajificha bure bali wanaendelea kuzalisha sabuni hizo zisizo na viwango na hivyo kuweka afya za watumiaji katika hatari,"Kaisi alisema.
Kwa mujibu wake, Shirika la Viwango lilikipa kiwanda hicho leseni ya ubora mwaka 2010 baada ya wazalishaji wa sabuni hiyo kutimiza masharti ya awali ya ubora, lakini, baada ya hapo hawakuwa wakipatikana tena kwa simu wala kwa kufikiwa kutokana na ukweli kwamba wamekuwa wakijificha kwa kuhamahama.
"...kutokana na hilo, wamekuwa wakizalisha kwa kufuata utaratibu wanaoujua wao na viwango vya ubora wanavyoviamini wao, hilo ni kosa kwa sababu TBS ndio yenye kueleza kama viwango vilivyotakiwa vinafuatwa au la".
" Tumebaini kuwa licha ya kuwafungia wanaendelea kutumia nembo yetu kurubuni wanunuzi. Udanganyifu huo tuliubaini mapema tukaanza taratibu mbalimbali za kuwazuia wasiendelee, ikiwa ni pamoja na kuwaandikia barua kadhaa ambazo hata hivyo hazijajibiwa hadi leo," Kaisi alisema.
Alifafanua kuwa awali kiwanda hicho kilikuwa Tegeta nje kidogo ya Dar es Salaam na kwamba kutokana na uzalishaji wa ujanja ujanja unaokwepa ukaguzi wa ubora wamekuwa wakihama hama na kufanya anuani yao isijulikane.
"Kutukimbia ni kosa la kwanza, la pili ni la kuzalisha sabuni ya mche wanayodai wanaitoa bure kwa anayenunua kilogramu 1000 ya sabuni ya unga ya Klin, bila kuwa na ruhusa yetu na kosa la tatu ni kuingiza kinyemela sokoni bidhaa inayozalishwa kiholela mitani bila kujali afya ya mteja".
Kufuatia ukiukwaji huo, Kaisi alisema, "Hata bila uwepo wao katika eneo hili ambalo ndilo tunalolitambua katika mkataba wetu (Tegeta), tunautangazia umma kuwa kiwanda chao kimefungwa na atakayeendelea kuuza sabuni hiyo akikamatwa atawajibishwa kisheria." 
Katika hatua nyingine, TBS imewaomba wananchi watoe taarifa endapo watafahamu mahali uzalishaji wa sabuni hiyo unapoendeshwa ili waweze kuuzuia kwa faida ya afya ya watumiaji.
Kaisi aliongeza kuwa endapo wahusika watajitokeza, hatua zinazostahili zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwakagua upya huko walipoanzisha makazi mapya ya kiuzalishaji, pamoja na kuwataka waombe upya leseni ya ubora.

No comments: