LWAKATARE SASA ALALA URAIANI BAADA YA KUPATIWA DHAMANA...

Wilfred Lwakatare (wa pili kulia) akiongea na waandishi nje ya mahakama jana.
Hatimaye Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa  Chadema, Wilfred Lwakatare anayekabiliwa na mashitaka ya kupanga njama za kudhuru kwa sumu, ameachiwa kwa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Lwakatare aliachiwa jana na Hakimu Mkazi Aloyce Katemana baada ya Mahakama kukubali ombi lake la dhamana, huku mshitakiwa mwenzake  Ludovick Joseph akirudishwa rumande hadi Juni 24.
Aliachiwa saa 8 mchana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni kusaini hati ya Sh milioni 10, kuwa na wadhamini wawili wanaofanya kazi katika taasisi inayotambulika ambao walisaini hati hiyo.
Aidha, aliwasilisha hati yake ya kusafiria na haruhusiwi kusafiri nje ya mkoa bila kibali cha Mahakama,  Joseph alirudishwa rumande kwa kushindwa kutimiza masharti hayo.
Uamuzi huo ulizua nderemo na shangwe kwa wafuasi wa Chadema waliokuwa kwenye eneo la Mahakama wakiwa na mabango, huku wakitoa kauli yao ya “People’s Power (Nguvu ya umma)” .
“Lwakatare ameshinda Mungu amempigania…,”  ndiyo baadhi ya maneno yaliyoandikwa kwenye baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na wafuasi wa Chadema walioandamana baada ya Lwakatare kuachiwa na kutoka eneo la Mahakama.
Kesi hiyo ilitajwa saa 2 asubuhi kwa ajili ya uamuzi na baada ya kusomewa masharti ya dhamana, upande wa mashitaka ulidai barua za wadhamini wa Lwakatare hazina picha, pia waliomba wakazihakiki. Hakimu Katemana aliahirisha shauri hilo hadi saa 8 mchana.
Awali akisoma uamuzi wa maombi ya dhamana, Hakimu Katemana alisema maombi hayo yaliwasilishwa Mei 13 mbele ya Hakimu Mkazi Sundi Fimbo ambaye aliyasikiliza bila kutoa uamuzi.
Alisema washitakiwa walikuwa wanakabiliwa na mashitaka manne, yakiwamo ya ugaidi ambayo hayana dhamana, lakini  Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliwafutia mashitaka hayo na kubaki mashitaka ya jinai yenye dhamana.
“Kwa kuwa mashitaka yanayowakabili washitakiwa kwa sasa yana dhamana, Mahakama ina mamlaka ya kutoa dhamana endapo watatimiza masharti yaliyotolewa,” alisema.
Awali, Lwakatare na Joseph, walikuwa wakikabiliwa na kesi ya ugaidi katika Mahakama hiyo,  Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) aliwafutia mashitaka yote na kisha kuwakamata na kuwashitaki tena kwa makosa hayo hayo.
Lwakatare hakuridhika na uamuzi huo na kuwasilisha ombi la kutaka Mahakama Kuu ifanye marejeo ya mwenendo wa kesi ya ugaidi, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Mei 8 Jaji Lawrence Kaduri wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam alifuta mashitaka ya ugaidi kwa kuwa hati ya mashitaka iliyofunguliwa na DPP, haikueleza uhalisia wa tuhuma na uhusika wa watuhumiwa katika kufanya ugaidi.
Hata hivyo, DPP aliwasilisha maombi ya marejeo katika Mahakama ya Rufaa akiomba iitishe majalada ya kesi hiyo na kuchunguza uhalali wa uamuzi wa kuwafutia mashitaka hayo kwa madai kuwa haukuwa sahihi na kufuta uamuzi huo. Lwakatare naye aliwasilisha pingamizi la awali kupinga ombi la DPP.
Washitakiwa hao wanadaiwa kupanga njama ya kutenda kosa la jinai la kutumia sumu kumdhuru Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi Dennis Msacky, ambapo wanadaiwa kulitenda Desemba 28 mwaka jana eneo la King’ongo, Kinondoni, Dar es Salaam.

No comments: