WAASI RDC WAONYWA WAKITIA MGUU TANZANIA WATAKIONA CHAMOTO...

Baadhi ya askari wa kundi la waasi la M23 wakirandaranda nchini DRC.
Waasi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wanaojiita M23 wameonywa wasithubutu kuingia nchini kishari kwani wakifanya hivyo cha moto watakiona.
Lakini wanapaswa pia kujua kwamba kamwe Tanzania haitatishwa na kauli zao kwani nchi iko imara dhidi ya adui yeyote.

Onyo hilo lilitolewa jana bungeni mjini hapa na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.  
Waziri Membe alitaka waasi hao waache kutumia jina la Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuifundisha Tanzania dhana ya wema ni nini.
Pamoja na kuwaagiza kuacha kutishia Watanzania, Waziri Membe aliwataka kuacha kubaka na kuua wananchi wa Kongo vinginevyo Tanzania kwa kusaidiana na mataifa mengine chini ya uongozi wa Umoja wa Mataifa (UN) itaingia nchini humo kulinda wananchi.
Alisema ghasia zinazofanyika Kongo ‘zinazaa’ wakimbizi na kusema ni wajibu wa Tanzania ikishirikiana na mataifa mengine kulinda uhai wa wananchi wa Kongo.
Waziri Membe alisema hayo alipochangia makadirio ya matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) iliyopitishwa na Bunge jana huku akisaidia kujibu hoja za wapinzani kuhusu M23 na usalama wa mpaka wa Ziwa Nyasa.
Waziri wa Ulinzi na JKT, Shamsi Vuai Nahodha katika hotuba yake alisema mipaka ya nchi kwa ujumla iko shwari ingawa upinzani ulihoji kauli ya M23 na kujitoa kwa Malawi katika mazungumzo ya mgogoro wa mpaka.
Wizara ya Ulinzi na JKT jana ilipitishiwa na Bunge jumla ya Sh trilioni 1.1  ambazo kati yake  Sh bilioni 857.4 ni kwa matumizi ya kawaida na Sh bilioni 245.6 kwa matumizi ya maendeleo.
Membe alisema Tanzania imepata baraka zote za kutoa kikosi cha Jeshi kwenda Kongo kuungana na majeshi mengine kulinda amani nchini humo, hivyo vitisho vilivyotolewa hivi karibuni havina msingi.
“Muda umefika wa kwenda kusaidia majirani zetu ili kuhakikisha Wakongo wanaishi kwa amani na kufanya shughuli zao na hakuna wa kututisha na kuzuia majeshi yetu kwenda Kongo,” alisema Waziri Membe.
Membe alisema amepokea barua kutoka kikundi hicho kikitishia kuwa endapo Tanzania itatoa askari kwenda nchini humo watauawa kwa mauaji ya halaiki.
“Nimepokea barua imetumwa kwangu ikiwa na anuani ya Mungu, inadai imetoka kwa Mungu, lakini lugha ndiyo hiyo hiyo tunayoisoma kila siku, huku ikimnukuu marehemu Baba wa Taifa kuwa binadamu wote ni sawa,” alisema.
“Nadhani walitaka kutumia jina la Mungu ili Serikali itishike na kushindwa kufanya majukumu yake. M23 wametutisha kama alivyotutisha Kanali Bakari wa Comoro kuwa vijana wetu wakienda pale watakuwa chakula cha mamba.
“Vijana walikwenda na badala ya kuwa chakula cha mamba wao wakala samaki na siku ya tatu Kanali Bakari alikimbia akivalia baibui na kuiacha nchi… vitisho vya M23 ni vya mtu ambaye amekata tamaa,” alisema.
“Hawa watu hawawezi kutumia jina la Baba  yetu wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kutufundisha sisi juu ya wema ni nini, huku wakiendelea kuua watu na kubaka huku wakidhalilisha wazee wao, huko ni kukufuru  ni lazima tutakwenda kukomesha hilo,’’ alisisitiza huku akiwa na uso wa hasira.
Membe alisema endapo Jeshi laTanzania litakwenda nchini humo kisha kuguswa na kikundi hicho, Tanzania itajibu mapigo.
Waziri huyo alisema endapo kikundi hicho hakipendi Jeshi la Tanzania kwenda nchini humo, ni lazima wafanye mambo kadhaa ikiwamo kurudi katika mazungumzo ya Uganda, kuacha kuua raia wasio na hatia na kubaka na kujisalimisha kwa hiari.
“Sisi tupo tayari kutokwenda, lakini lazima wafanye yafuatayo: Warudi kwa Rais  Museveni (Yoweri wa Uganda) na kuendelea na mazungumzo;  kujisalimisha kama walivyofanya baadhi yao hivi karibuni na kutoendelea kubaka na kudhalilisha wazee wao bila sababu.
“M23 wanaua, wamebaka, M23 wamedhalilisha wazee na akinamama, M23 wameleta wimbi la wakimbizi 230,000 hasa 30,000 wanaoingia Tanzania; kama wangethamini kauli ya mwalimu wasingefanya hayo, wamefanya hivyo hadi kusababisha kiongozi wao, Bosco Ntaganda, kujisalimisha na sasa yupo The Hague kujibu mashitaka ya uhaini hawawezi kutufundisha ubinadamu wala amani,” alisema kwa hasira.
Waziri Membe alisema nia ya Jeshi la Tanzania kwenda Kongo ni kufanya kazi tatu tu, ikiwamo ya kunyang’anya silaha kikundi hicho, kuwabana wasijipanue kama wanavyotaka sasa na pia kuhakikisha kuwa wanajisalimisha na vizuri wajiunge na Jeshi la Serikali.
Kwa upande wa usalama wa wanajeshi watakaokwenda DRC na kukaa pamoja na wa kutoka Malawi, hasa kwa kuzingatia mgogoro uliopo kuhusu mpaka wa Ziwa Nyasa,  Membe alisema taarifa zilizopo sasa vikosi vya Tanzania na Malawi vimetengwa umbali wa kilometa 100.
Alisema hali hiyo pia itaimarishwa zaidi na hadhari iliyowekwa, kwani usalama kwa askari wa Tanzania ni wa kutosha kwani vikosi hivyo vyote vitaongozwa na Mtanzania.
Alisema kutokana na uwepo wa umbali huo hakuna tatizo la mmoja kutisha mwingine na wote watakuwa wakifanya majukumu yao yaliyoorodheshwa na Baraza la UN kwa Azimio namba 2098.
Akizungumzia tatizo la mpaka huo, Waziri Membe alisema uko salama na kuwatoa Watanzania wasiwasi.
Alisema Serikali ya Malawi imerudi kwenye mazungumzo, Tanzania inatarajia kwenda  Msumbiji mapema mwishoni mwa mwezi huu.
Alisema hata hivyo, Tanzania haitasita kuendelea na hatua nyingine endapo itashauriwa kufanya hivyo na jopo la marais wastaafu, ambao wanasikiliza tatizo hilo wakiongozwa na Rais mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chisano.
Hata hivyo, alisema Serikali ina kila ushahidi wa kushinda kesi hiyo, kwani ina vielelezo vyote kuhusu mipaka ya Ziwa hilo.

No comments: