Abiria wakiwa ndani ya treni hiyo. |
Abiria wanaotumia usafiri wa treni kutoka kituo cha Stesheni kwenda Ubungo Jijini Dar es Salaam, wameanza kuonja ‘machungu’ ya usafiri huo, kutokana na idadi ya mabehewa kuwa ndogo, ikilinganishwa na abira wanaotaka kusafiri.
Mwandishi alishuhudia juzi na jana, abiria hao katika kituo cha Stesheni wakiwa wamejazana kupita kiasi katika mabehewa huku wengine wakigombea kuingia bila kuwa na matumaini yoyote ya kupata nafasi ya kusafiri.
Katika treni hiyo yenye mabehewa nane, imewalazimu watoa huduma wake, kuzuia matumizi ya behewa moja katika kituo hicho, kwa lengo la kutoa nafasi kwa abiria wengine wanaopandia kituo cha Kamata, kuweza kusafiri baada ya kuwepo kwa malalamiko kwamba treni hiyo huwa imeelemewa inapokuwa imetoka Stesheni.
Kwa mujibu wa wananchi mbalimbali waliozungumza na mwandishi, kuelemewa kwa treni hiyo kunasababishwa na foleni kubwa zinazojitokeza katika barabara mbalimbali za jijini Dar es Salaam hasa nyakati za asubuhi na jioni.
Alipotafutwa Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) yenye dhamana na usafiri huo, Midlady Maez alikiri tatizo hilo na kueleza kuwa hatua hiyo inatokana na kutokamilika kwa miundombinu ya reli nyingine, kama ilivyokuwa imeahidiwa wakati wa uzinduzi wa usafiri huo.
Alisema wakati unazinduliwa usafiri huo Oktoba 29 mwaka jana, walisema kuwa huduma ya treni hiyo ungetarajiwa kuwa wa treni mbili zenye behewa sita kila moja, ambazo zingetarajiwa kupishana eneo la Buguruni kwa Mnyamani, hivyo kutokana na miundombinu ya reli ya pili kutokuwa tayari ndio kumesababisha hali hiyo.
No comments:
Post a Comment