Abdallah Zombe akiwa mahakamani. |
Mahakama ya Rufaa jana ilitupilia mbali rufaa ya kupinga kuachiwa huru kwa Zombe na wenzake wanane.
Mahakama hiyo ilitoa uamuzi huo, kutokana na kasoro zilizo kwenye taarifa ya kusudio la kukata rufaa hiyo iliyowasilishwa na DPP.
Katika rufaa hiyo, DPP alikuwa anapinga hukumu iliyotolewa Agosti 17, 2009 katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, akidai Jaji Salim Massati, alikosea kuwaachia huru washitakiwa hao waliokuwa wanakabiliwa na mashitaka ya mauaji.
Kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa, jopo la majaji Edward Rutakangwa, Bathuel Mmila na Mbarouk Mbarouk, waligundua kasoro katika taarifa ya kusudio la kukata rufaa na mawakili wa Zombe kuomba rufaa hiyo itupwe.
Akisoma uamuzi huo, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Elizabeth Mkwizu, alisema Mahakama inatupa rufaa hiyo chini ya kanuni ya 61 (1) ya Sheria za Mahakama za Rufaa, kwa kuwa rufaa hiyo haikuwasilishwa kama inavyotakiwa kisheria.
Alisema katika taarifa hiyo, DPP alidai wanapinga hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iliyotolewa na Jaji Massati wa Mahakama ya Rufaa, jambo linaloonesha hukumu ilitolewa katika Mahakama ya Rufaa.
Mkwizu alisema Mahakama ya Rufaa hairuhusiwi kikatiba kusikiliza mashauri yaliyotolewa uamuzi katika Mahakama hiyo, isipokuwa kutoka Mahakama za chini na pia Jaji wa Mahakama hiyo haruhusiwi kusikiliza kesi mahakama za chini.
Alifafanua, kwamba endapo Jaji atateuliwa kuwa wa Mahakama ya Rufaa, ataendelea kusikiliza na kutoa uamuzi wa mashauri aliyokuwa akisikiliza kwa wadhifa wa Jaji Kiongozi au wa Mahakama hiyo.
Alisema kutokana na kasoro zilizokuwa kwenye kusudio la kukata rufaa, Mahakama imeona hakuna rufaa iliyowasilishwa mbele yake, na hawawezi kuruhusu wakata rufaa wafanye marekebisho kwa kitu ambacho hakiko mahakamani.
Hata hivyo, alisema wakata rufaa wana haki ya kuomba kurudisha rufaa hiyo kwa kutumia sheria ya ukomo wa muda.
Akizungumza nje ya Mahakama, Zombe alisema:“Sheria si kulazimisha, si hisia bali ni ushahidi.” Aliitaka Serikali kuacha tabia ya kubambikia watu kesi, kwa sababu nchi inaendeshwa kwa misingi ya sheria.
Kwa upande wake, mshitakiwa Christopher Bageni, alisema hajaridhika kwa kuwa rufaa hiyo imetupwa kwa kosa dogo, lakini alipenda isikilizwe, ili Mahakama ithibitishe kuwa hawana hatia.
Mbali na Zombe, washitakiwa wengine walikuwa ni ASP Christopher Bageni, ASP Ahmed Makelle, Konstebo Noel Leonard, Konstebo Jane Andrew, Koplo Nyangerela Moris, Konstebo Emmanuel Mabula, Koplo Felix Sedrick, Michael Shonza, Koplo Abeneth Salo, Koplo Rashid Lema (aliyefariki kabla ya kujitetea), Koplo Rajabu Bakari na Koplo Festus Gwabisabi.
Walidaiwa kuwa Januari 14, 2006 eneo la Mabwepande waliwaua Sabinus Chigumbi na ndugu yake Ephrahim Chigumbi, Mathius Lunkombe na Juma Ndugu.
Agosti 17, 2009 Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliwaachia huru baada ya kuridhika kuwa washitakiwa hawakuwa na hatia ya mashitaka yaliyokuwa yakiwakabili. Katika uamuzi huo, Jaji Massati alisema alibaini walioshitakiwa, si walioua, bali wauaji hawakuwa mahakamani.
Wakati huo huo, hatma ya Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Shekhe Issa Ponda na wafuasi wake 49, itajulikana leo wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, itakapotoa hukumu katika kesi ya uchochezi na wizi wa mali zenye thamani ya Sh milioni 59 inayowakabili.
Hukumu hiyo itatolewa na Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa, baada ya kupitia majumuisho ya hoja na ushahidi wa pande zote mbili, uliowasilishwa kwa njia ya maandishi.
Shekhe Ponda na wenzake wanakabiliwa na mashitaka ya uchochezi, kuingia kwa nguvu na kujimilikisha isivyo halali kiwanja cha Chang’ombe Markazi kinachomilikiwa na kampuni ya Agritanza na wizi wa mali zenye thamani hiyo.
1 comment:
naachia muuaji ee
Post a Comment