MABAKI YA BOMU LILILORUSHWA KANISANI ARUSHA KUCHUNGUZWA...

Mabaki ya bomu hilo lililoua watu watatu na kujeruhi zaidi ya 70.
Bomu lililorushwa katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti Arusha litachunguzwa kubaini aina yake na lilikotengenezwa.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ameagiza vipande vya chuma vitakavyotolewa katika miili ya majeruhi wa mlipuko wa bomu hilo vichunguzwe.
Ameagiza vipande hivyo, vikabidhiwe kwa wataalamu wa mabomu kubaini kama lilikuwa bomu la kutengeneza kienyeji au la kiwandani.
Alitoa agizo jana alipotembelea majeruhi katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, Arusha akifuatana na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck ole Medeye na baadhi ya wabunge wa viti maalumu wa CCM.
Alitaka madaktari watakaofanya upasuaji kwa majeruhi hao, kukabidhi vipande hivyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo ambaye atavikabidhi kwa wataalamu wa mabomu, ili wavichunguze. 
Akitoa taarifa ya ziara yake Arusha, Pinda  alisema: “Pale Mount Meru, madaktari wanaendelea na upasuaji leo (jana) na kesho (leo), kutoa vyuma kwenye miili ya majeruhi.
“Tumewaagiza kwamba vyuma hivyo wasivitupe, wavikabidhi kwa vyombo vya Dola kwa sababu tunataka kujua kama bomu lile lilikuwa la kienyeji au kiwandani, kwa maana ya kijeshi. Tunataka kujua chimbuko lake, ndiyo maana tumewaambia wasivitupe,” alisema Pinda.
Waziri Mkuu alisema uchunguzi kuhusu shambulio hilo bado unaendelea na wanashikilia watu wanane;  wanne wenye asili ya Arabuni, na Watanzania watatu akiwamo aliyetuhumiwa kurusha bomu hilo, Victor Ambrose na mwenzake ambaye hakumtaja jina.
“Hawa raia wanne wa kigeni tunawashikilia ili kujiridhisha kama wanahusika na tukio hilo, kwa sababu waliingia siku moja kabla ya tukio na baada ya tukio, waliondoka nchini, wakakamatwa wakati mipaka imefungwa.
“Tumeanza kuzungumza nao ili kufanya uchunguzi kujua ushiriki wao, tusingewezeka kujiridhisha hivi hivi, ndiyo maana tumeona tuwahoji kama wanahusika,” alisema Pinda.
Waziri Mkuu alisihi baadhi ya watu wanaotumia tukio hilo kujipatia umaarufu wa kisiasa, badala ya kusaidiana na Serikali kutafuta chanzo cha tatizo.
"Mimi kwa upande wangu ni mtu wa mwisho sana kuingiza siasa katika masuala mazito kama haya, tunapaswa kulaani tukio hili zito na si tuingize siasa au kulaumiana.
“Tukio lile ni kubwa, ni kitendo kibaya, si kitendo cha kushabikia kisiasa. Kimehuzunisha watu wote, tunapaswa kushirikiana wote. Lakini kule (Arusha) kuna watu wachache wanazungumzia visiasa visivyo na tija,” alisema.
Aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alipongeza vyombo vya habari kwa kutangaza tukio hilo bila kupotosha na kupongeza Serikali na Polisi kwa kufanya uchunguzi kwa haraka na kuomba waendelee ili ukweli ubainike na uwekwe wazi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alikabidhi msaada wa Wizara, wa dawa na vifaa vya kuhudumia majeruhi, wenye thamani ya Sh milioni 23.3 na kuahidi kukutana na wadau wa utalii wakiwamo wafanyabaishara, ili waone msaada gani zaidi watatoa kwa wagonjwa hao.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, alisema majeruhi walikuwa 66, kati yao watatu walifariki dunia na 24 kuruhusiwa baada ya kupata nafuu na 41 bado wapo hospitalini kwa matibabu zaidi.
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), lililaani tukio hilo ambapo Shekhe Mkuu wa Tanzania, Issa bin Shaaban Simba, katika taarifa yake iliyotumwa kwa vyombo vya habari, ilisema tukio hilo ni  la kusikitisha, kukera na kufadhaisha.
“Bakwata inalaani kitendo hicho cha kikatili na inaviomba vyombo vya Dola kufanya jitihada kuhakikisha wahusika wanakamatwa na wanachukuliwa hatua, kwani msiba huu ni wetu sote, Wakristo na Watanzania wote,” alisema Mufti Simba.
Chama cha Wananchi (CUF), nacho kililaani tukio hilo lililolenga watu wasio na hatia.
Akizungumza na wananchi katika maeneo tofauti mkoani Singida, Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad, alikitaja kitendo hicho kuwa ni cha kinyama na kisichotarajiwa.
Alisema Tanzania ina historia ya kuwa nchi ya amani na  vitendo kama hivyo vinaitia doa na kuiharibia sifa yake kitaifa na kimataifa.
Alitaka wananchi kuacha kushutumiana na kuiachia Serikali ifanye uchunguzi wa kina, ili kubaini wahusika na kuwachukulia hatua za kisheria.

No comments: