Baadhi ya waombolezaji wakishiriki mazishi ya watu watatu waliouawa kwenye shambulio la bomu kanisani mjini Arusha Jumapili iliyopita. |
Wakristo wametakiwa kutolipiza kisasi juu ya maovu yaliyofanywa na kikundi cha watu kwa kurusha bomu kanisani na kusababisha vifo vya watu watatu na wengine 66 kujeruhiwa.
Tukio hilo lilitokea Jumapili wakati wa uzinduzi wa kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi lililoko Olasiti jijini Arusha.
Mwito huo ulitolewa jana na Kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo wakati wa maziko ya wananchi hao; Regina Saning'o (50), James Gabriel (16) mwanafunzi wa kidato cha tatu sekondari ya Arusha Day na Patricia Assey (10) mwanafunzi wa darasa la tatu shule ya msingi Elerai.
Alisema madhumuni ya kurusha bomu hilo wanayajua warushaji, ila kikubwa kwa Wakristo ni kukumbuka maneno ya Biblia ya Paulo na Sila na kusamehe.
"Si vizuri sisi Wakristo kulipa ovu kwa ovu, bali tulipe ovu kwa jema, kama Maandiko yasemavyo, ila tusikate tamaa ya kumwomba Kristo," aliasa Pengo.
Alisema vifo hivyo vinapaswa kupokewa, kwa sababu waumini hao walitoa uhai wao kwa ajili ya kumtangaza Kristo.
Alitaka kujua kutoka kwa waumini kama kati yao atajitokeza aliyerusha bomu na kujitaja watafanyaje; wote waliitika kuwa watasamehe na kusema hilo ndilo kuu kwao.
Aidha, aliwataka waumini kuliombea Taifa hata kama watauawa kwa ajili ya imani yao, kwa sababu hilo ni jambo jema.
Pengo alisema kuna mifano mingi kama wa Zanzibar kuhusu mauaji ya Padri, lakini hayo yote ni ishara kuwa Taifa linaondokewa na amani.
"Tunaomba hili lisisambaratishe imani yetu kamwe, bali tuendelee kudumu katika imani yetu kwa kuliombea Taifa hii," alisema.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na maaskofu zaidi ya saba kutoka Kanisa Katoliki mikoa mbalimbali nchini na madhehebu ya dini nyingine.
Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Askofu wa Jimbo la Iringa, Tarcisius Ngalalekumtwa, alisema vifo hivyo ni mwanzo wa imani ya Kikristo na watu waendelee kuwa nayo.
Alisema siku za karibuni mambo maovu yamekithiri hasa dhidi ya Ukristo; kuchomwa moto makanisa, mauaji ya viongozi wa dini na hatimaye kurushwa bomu kanisani.
Askofu Ngalalekumtwa alisema mwenye macho haambiwi tazama, “kwani kumekuwa na DVD, CD, vipeperushi vya kila aina na mihadhara ya kuchochea chuki dhidi ya Ukristo, lakini hatua za dhati hazichukuliwi.
"Katika miaka mitatu hali ya usalama nchini imetoweka na hili linafanywa na mihadhara ya dini, ila hakuna hatua," alisema.
Alidai kuwapo baadhi ya Waislamu wanaoendesha vikao vya siri na kueneza chuki na cha mwisho walikaa Oktoba 16 mwaka juzi na kuazimia kuua ili kutokomeza Ukristo.
"Sisi tunaendelea kulaani kundi hili dogo la Waislamu wanaotaka kuharibu amani yetu na tutaendelea kulaani," alisema.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Alex Malasusa alisema watu wengi wamehuzunishwa na tukio hilo la kinyama na marehemu wataurithi ufalme wa mbinguni.
"Lakini kubwa, Taifa limepata doa kutokana na tukio hili na amani iliyopo sasa imetoweka, inasikitisha sana," alisema.
Askofu Malasusa alisema kubwa zaidi ni kushinda mabaya kwa wema na Wakristo wasiwe waoga bali tukio hilo liwaimarishe.
"Mimi binafsi natamani sana mauti yanikute kanisani, maana nitakuwa nimeifia dini yangu, hivyo kwa hili hawa ni mashuhuda wa imani tosha na inapendeza mbele ya Kristo," alisema.
Aidha, aliomba wenye mamlaka ya kulinda amani na kuitunza wafanye hivyo na vinginevyo watapata shida siku ya mwisho.
Upande wa Mwenyekiti wa Umoja wa Madhehebu ya Kikristo Arusha, Askofu Stanley Hotay, alisema mharibifu au mwizi siku zote hatoi taarifa anapokuja na wala hahitaji kusindikizwa, hivyo ni vema watu wakawa macho.
Askofu Hotay aliomba watu wasiligawe Kanisa kwa misingi ya itikadi za vyama, kwa sababu waumini wao ni wa vyama mbalimbali, hivyo ni vema wakawa kitu kimoja.
Lakini pia alihadharisha waandishi wa habari wawe makini na kuepuka kununuliwa, kwa sababu nao hawako salama.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alitaka viongozi wa dini kutokatishwa tamaa na vitendo hivyo na kuwataka waendelee kueneza kazi ya Bwana.
Alisema anayefikiri kuua kiongozi wa dini au mwumini anaua dini ya Ukristo au Uislamu, anajidanganya kabisa.
"Hatuwezi kuua dini hizi kubwa kwa kuua mtu au watu fulani ni kujidanganya utakuwa umeua mtu tu," alisema.
Pia alitoa mwito kwa watu kuwa watulivu wakati huu hasa watakapoona kamatakamata imezidi ya watu, lengo ni kupata ukweli.
Aidha, kupitia Kitengo cha Maafa Ofisi yake, Waziri Mkuu alitoa rambirambi ya Sh milioni 100 na aliwasilisha Sh milioni mbili za wajumbe wa mkutano wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT) wanaokutana hapa na aliwakabidhi viongozi wa Kanisa kwa lengo la kusaidia shughuli mbalimbali.
Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Josephat Lebulu, alihitimisha kwa kutaka waumini wasikate tamaa kwa tukio hilo.
Alitaka watu wasiogope na wazidi kumtangaza Kristo huku akiwashukuru viongozi wa Serikali, Bunge, madaktari na watu mbalimbali kwa ushirikiano walioonesha katika wakati huu mgumu.
"Lakini mimi kama baba, nasema mambo haya yafike mwisho na tuseme sasa imetosha, hivyo tuendelee kuomba," alimalizia huku akilia na kusababisha Kanisa zima kuangua kilio.
No comments:
Post a Comment