KESI YA WILFRED RWAKATARE KUUNGURUMA TENA LEO...

Wilfred Rwakatare akiingia mahakamani Kisutu kusikiliza kesi dhidi yake.
Uamuzi wa ombi la marejeo ya mwenendo wa kesi ya ugaidi inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Rwakatare, utatolewa leo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Ombi hilo, liliwasilishwa Machi 22, baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kuwafutia mashitaka Lwakatare na mwenzake Ludovick Joseph, kisha wakakamatwa na kusomewa upya mashitaka hayo.
Jaji Lawrence Kaduri atatoa uamuzi huo leo, baada ya kupitia hoja za mawakili wa pande zote mbili.
Katika ombi lao, mawakili wa Lwakatare wanaiomba Mahakama Kuu ifanye marejeo na kuchunguza mwenendo wa kesi hizo mbili, ili ijiridhishe juu ya usahihi na uhalali wa mwenendo katika kesi namba 37 ya mwaka huu, iliyofutwa na namba sita iliyofunguliwa upya.
Wanaomba marejeo au kutengua hati ya DPP iliyowafutia mashitaka, kabla ya kuwafungulia tena kwa kuwa kitendo alichofanya DPP ni kinyume na misingi ya sheria inayomwongoza.
Wanadai kwa mujibu wa sheria hiyo, DPP alitakiwa kufuta mashitaka kwa haja ya kulinda haki, kuzuia matumizi mabaya ya mfumo wa Mahakama, maslahi ya umma na kudhibiti mashitaka, lakini aliwasilisha hati hiyo kwa nia mbaya.
Wanaomba Mahakama iamuru Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, itoe uamuzi wa ombi la dhamana uliotakiwa kutolewa katika kesi iliyofutwa, pia ifanye marejeo na au kutengua mwenendo wa kesi mpya iliyofunguliwa, iamuru kuwa utaratibu uliotumika kutoa hati ya kufuta mashitaka dhidi ya washitakiwa, ulikuwa kinyume cha sheria au haukuwa sahihi.
Hata hivyo, upande wa mashitaka, ulidai kuwa kesi hiyo ipo katika hatua za awali na mashitaka yanayowakabili yanaweza kufanyiwa mabadiliko, kama kuwashitaki chini ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu au kuwaachia huru.
Pia walikiri kuwa sheria haijaeleza maana ya ugaidi na kufafanua, kwamba kuteka nyara ni kosa la ugaidi, lakini linaweza kushitakiwa chini ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Kutokana na hali hiyo, mawakili hao walisema baada ya upelelezi, wataangalia ushahidi watakaopata kama utathibitisha kosa hilo la ugaidi kwa Lwakatare, basi ataendelea kushitakiwa kwa Sheria ya Ugaidi na kuwa DPP alifuta mashitaka hayo kwa kufuata utaratibu wa sheria.

No comments: