Iddi Simba. |
Mwenyekiti
wa Bodi ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), Iddi Simba aliyekuwa
akikabiliwa na mashitaka ya kusababisha hasara katika shirika hilo, amefutiwa mashitaka
hayo na kusomewa mapya ya uhujumu uchumi.
Awali
Simba na wenzake, walikuwa wakikabiliwa na mashitaka ya kusababishia shirika
hilo hasara ya Sh bilioni 2.3, kwa kuuza hisa milioni 7.8 za shirika kwa
kampuni ya Simon Group, bila kufuata utaratibu wa mchakato wa zabuni.
Jana
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ilvin Mugeta, aliwaachia huru washitakiwa
hao, baada ya upande wa mashitaka, kuomba kufuta kesi ya jinai iliyokuwa
inawakabili, kabla ya kukamatwa tena na kusomewa mashitaka mapya.
Aidha,
Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Simon Group, Robert Kisena, ameunganishwa
katika mashitaka hayo, lakini jana hakufikishwa mahakamani kusomewa mashitaka
dhidi yake kwa kuwa bado hajakamatwa.
Awali
Wakili wa Serikali, Osward Tibabyekomya, alidai mahakamani hapo kuwa wakati
wanakusanya ushahidi katika kesi hiyo, walibaini kuwa ushahidi huo ni wa
mashitaka ya uhujumu uchumi ambayo wanataka kuyaongeza.
Hata
hivyo, alidai kuwa walibaini wakiongeza mashitaka hayo, wataharibu mwenendo wa
kesi hiyo ndio maana wanaiomba Mahakama wafute kesi hiyo na kufungua kesi ya
uhujumu uchumi, chini ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Mbali
na Simba ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara katika Serikali ya
Awamu ya Tatu, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mkurugenzi wa Bodi ya
Shirika hilo, Salim Mwaking’inda na Meneja Mkuu wa Shirika hilo, Victor
Milanzi.
Akiwasomea
mashitaka hayo, Wakili Awamu Mbagwa, alidai kuwa katika mashitaka yanayomkabili
Simba na Milanzi, kati ya Septemba 2009
na Januari 2010 Dar es Salaam, walipanga njama kwa nia ya kujihusisha na
vitendo vya rushwa katika ununuzi.
Alidai
kuwa katika siku hizo hizo, Simba na Milanzi, walipokea Sh milioni 320 kutoka
kwa Kisema, kama kishawishi cha kuiuzia kampuni hiyo hisa za Uda.
Mbagwa
alidai kuwa Simba, Milanzi na Mwaking’inda, wakiwa katika ofisi za Uda,
Kurasini, Temeke, Dar es Salaam, walitumia madaraka yao vibaya kwa kuuza hisa
milioni 7.8 za shirika hilo.
Mauzo
ya hisa hizo zilizokuwa zikimilikiwa na Serikali na Halmashauri ya Jiji la
Dar es Salaam, kwa kampuni ya Simon
Group, inadaiwa hayakufuata mchakato wa zabuni jambo ambalo ni kinyume na
sheria.
Katika
mashitaka mengine, inadaiwa kuwa kati ya Septemba 2009 na Februari 2011,
washitakiwa hao walitumia madaraka yao vibaya kwa kuuza hisa kwa Sh bilioni
1.1, bila kuwahusisha wamiliki wa hisa hizo jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Aidha
alidai kuwa, washitakiwa hao walisababisha hasara ya Sh bilioni 8.4, na si Sh
bilioni 2.3, iliyokuwepo katika mashitaka ya awali kwa shirika hilo.
Hasara
hiyo inadaiwa kutokana na kuuza hisa hizo kwa Sh bilioni 1.1, wakati kama
wangefuata mchakato wa zabuni, wangeuza hisa hizo kwa Sh bilioni 8.4.
Hata
hivyo, washitakiwa walikana mashitaka na kuachiwa kwa dhamana, baada ya Wakili
Alex Mgongolwa, kuomba wadhamini wa awali waendelee kuwadhamini washitakiwa
hao.
Hakimu
Mugeta alikubaliana na ombi hilo kwa kuwa walifutiwa kesi hiyo asubuhi, hivyo
wadhamini hao wataendelea kuwadhamini na watahamisha nyaraka za dhamana
zilizokuwa katika kesi ya awali.
Wadhamini hao wametakiwa kufika mahakamani Mei
20 na wasipofika, washitakiwa watatakiwa kuwa na wadhamini wengine. Upelelezi
wa kesi hiyo umekamilika.
No comments:
Post a Comment