BUNGE LAUNDA KAMATI KUCHUNGUZA YA MTWARA...

Spika Anne Makinda.
Spika Anne Makinda ameunda Kamati Maalumu ya Bunge kwenda kuzungumza na wananchi wa Mtwara kuhusu sakata la ujengwaji wa bomba la gesi asilia kutoka mkoani humo hadi Dar es Salaam.

Akihitimisha mjadala wa hotuba ya Bajeti  ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka ujao wa fedha bungeni mjini hapa jana, Makinda alisema kamati hiyo itakwenda Mtwara baada ya hali ya amani na utulivu kutengemaa.
Akitumia kanuni ya 5 ya Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la mwaka 2013, Spika Makinda alisema uamuzi wa kuundwa kwa kamati hiyo ulifikiwa katika kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bunge iliyokutana baada ya kuzuka kwa vurugu hizo Mei 22.
Vurugu hizo zilizuka muda mfupi baada ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuwasilisha bungeni hotuba yake hiyo ya bajeti na kusisitiza azma ya Serikali ya kujenga bomba hilo ili kusukuma mbele maendeleo ya Mtwara na Taifa.
“Kamati hii itakapofika Mtwara itakutana na wananchi wa kawaida, vikundi mbalimbali, taasisi na watu binafsi ili kusikiliza maoni na ushauri wao kuhusua suala hilo la ujenzi wa bomba la gesi.
“Napenda kuchukua nafasi hii kuwaomba wananchi wa Mtwara kuwa wawazi, watulivu, wawe na amani, utulivu, upendo na wasiwe na wasifanye ubaguzi wa aina yoyote watakapokutana na Kamati hii,” alisema Spika Makinda.
Alisema Kamati hiyo itafanya kazi hiyo chini ya hadidu rejea za kuchunguza chanzo cha vurugu hizo, kufuatilia hatua zilizochukuliwa na Serikali kushughulikia mgogoro huo, kukutana na wadau wa sakata hilo na kuchunguza mambo mengine yenye uhusiano na mgogoro huo.
Akitaja wabunge wanaounda Kamati hiyo, Spika Makinda alisema Kamati itakuwa chini ya Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage (CCM). Wajumbe ni  Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Arfi (Chadema), Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ramo Makani (CCM) na Cecilia Paresso (Viti Maalumu – Chadema).
Wengine ni Mbunge wa Kasulu Vijijini, Agripina Buyogera (NCCR – Mageuzi), Mbunge wa Kisarawe, Suleiman Jaffo (CCM), Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba (CCM), Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), Mbunge wa Igunga, Peter Kafumu (CCM),  Hilda Ngoye (Viti Maalumu – CCM), Rukia Kasimu Ahmed (Viti Maalumu – CUF), Mbunge wa Magomeni, Muhammad Chombo (CUF) na Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Kisangi (CCM).
Katika hatua nyingine, mjadala huo jana ulitawaliwa kwa kiasi kikubwa na shinikizo kutoka kwa wabunge wakitaka Serikali kuruhusu kukatwa kwa tozo ya Sh 100 kutoka kwenye mafuta na muda wa hewani wa simu za mikononi ili fedha zitakazopatikana zipelekwe kwa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kusaidia kusambaza umeme vijijini.
Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (NCCR – Mageuzi) na Mbunge wa Viti Maalumu, Devotha Likokola (CCM) waliiomba Serikali kufanya uamuzi mgumu ili kuruhusu tozo hiyo kukatwa na kusaidia umeme vijijini. Makadirio ya Wizara hiyo yalipitishwa na Bunge.

No comments: