BOMU KANISANI LAUA WATATU, LAJERUHI ZAIDI YA WAUMINI 70 ARUSHA...

Baadhi ya majeruhi wa bomu hilo wakipatiwa huduma eneo la tukio jana.
Watu karibu 70 wamejeruhiwa na watatu kufa, wakati kitu kinachodhaniwa kuwa bomu la kutupa kwa mkono, kiliporushwa kanisani na mtu asiyejulikana wakati misa ikiendelea.

Kitu hicho kilirushwa jana saa 4.45 asubuhi wakati waumini wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Arusha, wakiwa wamejumuika katika misa ya uzinduzi wa Kanisa la Mtakatifu Joseph, Parokia ya Olasiti.
Mlipuko huo ulitokea wakati Balozi wa Vatican nchini na Mwakilishi wa Papa Francis, Askofu Francisco Padilla, akiongoza misa hiyo kwa kushirikiana na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Arusha, Josephat Lebulu.
Akizungumzia tukio hilo, mpiga tarumbeta wa kanisa hilo, Clemence Mahimbo, alidai jana waumini wa makanisa yote ya kikatoliki Jimbo Kuu la Arusha, walihimizwa kwenda kusali katika kanisa hilo kutokana na shughuli hiyo ya uzinduzi.
Mahimbo alidai mara baada ya Askofu Padilla kunyunyiza maji ya baraka ndani ya kanisa hilo, akiongozwa na Askofu Lebulu, walikuwa wakitoka nje ya kanisa, lakini kabla ya kufika, kitu kinachodhaniwa kuwa bomu kilirushwa kutoka nje ya ukuta wa Kanisa. 
Alidai kitu hicho kililipuka katikati ya waumini waliokuwa wametangulia kutoka nje ya Kanisa, kumsubiri Askofu Padilla amalizie kunyunyiza maji ya baraka katika Kanisa.
 Kwa mujibu wa madai ya Mahimbo, baada ya mlipuko huo, Balozi Padilla na Askofu Lebulu walisitisha kazi ya kunyunyiza maji ya baraka ndani ya Kanisa na kuanza kuhangaika kuwaokoa majeruhi. 
Aidha, misa zote za pili katika makanisa yote ya Jimbo Kuu la Arusha, zilisitishwa, kutoa nafasi kwa waumini na mapadri, kwenda eneo la tukio kusaidia majeruhi.
Muumini mwingine aliyeomba kutotajwa jina lake, alidai aliyetupa bomu hilo, alikuwa amelihifadhi katika mfuko wa rambo na alikuwa akirandaranda nje ya kanisa hilo mara kwa mara. 
Mtoa habari huyo alidai waumini wengi na wasimamizi wa Kanisa kutoka sehemu mbalimbali jimboni Arusha, walikuwa ndani ya uwanja wa Kanisa, na nje ya ukuta wa Kanisa hakukuwa na muumini wala msimamizi wa Kanisa.
‘’Huyu jamaa aliyetupa bomu ndani ametumia udhaifu wa waumini wa Kanisa na wasimamizi kuwa ndani ya ukuta wa Kanisa, huku nje kukikosekana ulinzi wowote,” alidai.
Kwa mujibu wa taarifa za Polisi, waumini watatu  wamefa, na kituo kimoja cha redio kilimtaja kwa jina moja la Regina mmoja wa waliokufa.
Mwandishi alifika katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, na kukuta tayari miili ya waumini hao imehifadhiwa katika chumba cha maiti.
Baadhi ya majeruhi wamepata ulemavu baada ya kukatika viungo vya mikono na miguu na wamelazwa katika hospitali hiyo ya Mount Meru na Hospitali ya Mtakatifu Elizabeth ya jijini Arusha.
Majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Elisabeth, ni pamoja na Joan Temba (29), mkazi wa Majengo, Neema Kihisu (18), mkazi wa Metevezi, Regina Fredrick (23), mkazi wa Ilboru, Joram Kisera (38) mkazi wa Unga Ltd,  Vovert John (20), mkazi wa Sakina, Gloria Tesha (21), Unga Ltd na Saimoni Andrew (18) mkazi wa Kwa Mrombo.
Wengine wanaotoka eneo la Olasiti ni Inocent Charles (46), Rioba Oswar (36), Fatuma Haji (42), Rose Pius (39), Fikiri Keya (40), John  James (12), Anna Kesy (54), na Anna Edward (54).
Majeruhi 10 kati ya 30 waliolazwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, ni  Kasesa Mbaga, Philemoni Geleza, Neema Daudi, Beata Cornel, Debora Joackimu, Elizabeth Sauli, Editha Ndowo, Regina Daniel na Yasitha Msafiri.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema tukio hilo ni baya na ni la kigaidi na mtu mmoja anashikiliwa na Polisi kutokana na tukio hilo.
Alisema mtu huyo alirusha kitu kinachodhaniwa kuwa bomu kwa mkono, ingawa kulikuwa na ulinzi na watu waliojeruhiwa na wamepelekwa hospitali.
Msemaji wa Polisi Makao Makuu, Advera Senso,  alisema Mkuu wa Polisi, IGP Said Mwema ameshafika eneo la tukio na kuwataka wananchi watulie na kutoa ushirikiano kwa wakati wa uchunguzi.
Akizungumza katika eneo la tukio, IGP Mwema alisema watahakikisha wahusika wanachukuliwa hatua.

No comments: