BOMU KANISANI LAKATISHA ZIARA YA RAIS KIKWETE KUWAIT...

Rais Jakaya Kikwete.
Mshituko uliosababishwa na ugaidi wa bomu kurushwa kwa waumini katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya  Olasiti jijini Arusha, umemlazimu Rais Jakaya Kikwete, kukatisha ziara yake nchini Kuwait, na kurejea nyumbani haraka.

Rais Kikwete aliyekuwa aondoke leo kurejea nyumbani, amelazimika kukatiza ziara hiyo na kuondoka Kuwait City jana, ili kuwa karibu na wafiwa pamoja na wale waliojeruhiwa katika shambulio hilo la kigaidi.
Aidha, ameendelea kusisitiza kufanyike uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo la kusikitisha, kufadhaisha na kuudhi, huku akiahidi kamwe Serikali haitasalimu amri kwa watu au kikundi kinachojihusisha na matukio ya kigaidi nchini Tanzania.
Alisema hayo jana mchana kwenye Kasri la Bayan la Mtawala wa Dola ya Kuwait jijini hapa kabla ya kuanza safari ya kurejea nyumbani, wakati alipokuwa anazungumza na wajumbe aliofuatana nao katika ziara hiyo ya kwanza kwa Rais wa Tanzania nchini Kuwait.
Jana asubuhi, Rais aliyekuwa amalize ziara yake usiku , aliahirisha baadhi ya shughuli katika ziara hiyo, kwa kuchagua baadhi na kurejea nchini.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu aliyepo Kuwait City, Rais Kikwete alitarajiwa kuwasili nchini jana usiku na kwenda Arusha kuwajulia hali wafiwa na majeruhi.
Miongoni mwa shughuli ambazo hazikufanyika kutokana na uamuzi huo wa Rais, ni ziara ya kutembelea Kampuni ya Mafuta ya Kuwait, katika  eneo la Ahmadi mjini Kuwait.
Aidha, Rais pia alisitisha kuhudhuria dhifa ya chakula cha jioni, ambacho alikuwa ameandaliwa na Waziri Mkuu wa Kuwait, Shekhe Jaber Al Mubarak Al Hamad Al Sabah.
Akizungumzia kilichotokea Arusha, Rais Kikwete alisisitiza kuwa, kamwe hatakubali kuona baadhi ya watu
wakichezea amani ya Tanzania na kwamba, pamoja na umasikini, nguvu kubwa itapelekwa kuwasaka wahusika wa matukio ya kigaidi.
“Tutawasaka popote walipo na kupambana nao bila huruma.  Aidha, tutakabiliana na aina yoyote ya uhalifu nchini, iwe ni ugaidi au aina yoyote ya uhalifu wa namna hiyo au wa namna nyingine, uwe na chimbuko lake ndani ya nchi ama nje ya nchi yetu.
"Kamwe hatutakubali kuwaacha wavuruge amani na usalama wa Tanzania na watu wake," alisema Rais ambaye anaamini kuwa Serikali, kwa msaada na ushirikiano wa wananchi, watu hao watapatikana na kuadabishwa ipasavyo.
Pamoja na kuahidi kukabiliana na matukio ya aina hiyo, amewataka Watanzania kuwa watulivu, huku akisema matukio ya kigaidi kamwe hayana ratiba, bali uchunguzi ndio utakaobaini wahusika ambao alisema watachukuliwa hatua kali.
Alitoa mfano wa mlipuko wa Boston, Marekani kuwa haukupangwa, lakini baada ya kutokea kwa tatizo, uchunguzi wa kina ulifanyika na kubaini wahusika.
“Na hata hapa kwetu, tunafuatilia kwa karibu. Nimeagiza uchunguzi wa kina. Ni jambo ambalo halitufurahishi hata kidogo,” alisema Rais Kikwete, ambaye pia ametoa rambirambi kwa wafiwa na waliojeruhiwa katika tukio hilo.
Alisema anaungana na wafiwa, katika msiba na machungu. Rais pia anawaombea walioumia katika tukio hilo, wapate nafuu ya haraka na waendelee na shughuli zao za ujenzi wa taifa.
Ametoa pia pole kwa viongozi na waumini wa Kanisa Katoliki kwa tukio hilo la kusikitisha, ambalo lilivuruga ibada na shughuli yao muhimu ya uzinduzi wa Kanisa lao juzi Jumapili.
Shughuli alizofanya jana asubuhi kabla ya kuanza safari ya kurejea nchini, ni pamoja na kukutana wa baadhi ya watendaji wa Serikali ya Kuwait, wakiwemo wakuu wa mashirika na taasisi mbalimbali za maendeleo Kuwait.
Baadaye alisema ingawa alikuwa na muda mfupi nchini Kuwait, ziara yake imekuwa na mafanikio makubwa.
Baadhi ya ratiba zilizokuwa katika ziara yake rasmi ya kiserikali ya siku mbili nchini hapa, alizikabidhi kwa mawaziri aliofuatana nao, wakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Miongoni mwa ratiba ambazo amezifuta ni ziara katika Kampuni ya Mafuta ya Taifa ya Kuwait iliyopo katika eneo la Al Ahmadi.
Kuwait ni nchi ya sita duniani kwa kuzalisha mafuta mengi, ikiwa inatoa asilimia saba ya mafuta yote duniani na ikiwa na kiasi cha utajiri wa mafuta unaokadiriwa kufikia mapipa bilioni 104 katika eneo lake na lile la bahari kuu, ambako inagawana utajiri huo na nchi jirani ya Saudi Arabia.
Pia Rais hakuhudhuria dhifa ya chakula cha jioni, ambacho alikuwa ameandaliwa na Waziri Mkuu wa Kuwait, Shekhe Jaber Al Mubarak Al Hamad Al Sabah.
Akizungumza baada ya kuwatembelea majeruhi jana, waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema watakaoshindikana kupatiwa matibabu katika hospitali za nchini, watapelekwa nje ya nchi.
Aliwataka majeruhi waliotibiwa na kuruhusiwa, wakisikia maumivu, wasisite kwenda hospitalini kucheki afya zao.
Kuhusu watu watatu waliokufa, Pinda alisema Serikali itagharamia shughuli za mazishi kwa kushirikiana na familia za wafiwa.
Wakati huo huo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha, Josephat Lebulu, aliyenusurika katika tukio hilo la ugaidi, aliwataka Watanzania wajiulize kwanini watu wanauawa kama mbwa, na hao wanaofanya matukio hayo wanapata faida gani.
Akizungumza na waandishi wa habari eneo la Burka ambapo alinusurika yeye pamoja na Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Askofu Francisco Padilla na waumini wengine kujeruhiwa.
Askofu Lebulu alisema walikuwa wanaanza ibada na hawakujua kilichotokea isipokuwa alipogeuka yeye na Balozi Padilla, waliona watu wakiwa wamelala chini, huku wengine wakilia na kuumia sehemu mbalimbali.
"Hii inasikitisha na Watanzania tujiulize kwanini hivi sasa watu wanauawa kama mbwa na kwanini matukio haya yanajitokeza? Lakini pia mhusika aliyelipua bomu ndiye anayejua alikuwa akimlenga nani, kama si mimi ni Balozi na kama si Balozi, basi huyo mhusika ndio anajua.
“Nasikia uchungu sana kwani sijui mtoto yule na mama yule wapo hai au la, maana hali zao zilikuwa mbaya sana kwa kweli inauma sana,” alisema kwa uchungu Askofu Lebulu.
Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa, ambaye aliambatana na Makamu wa Rais kutoka mkoani Shinyanga, alisema amesikitishwa na tukio hilo.
Alisema tukio hilo sio la kawaida, na limewashitua watu wengi wanaopenda amani, lakini amewaomba waendelee kuwa watulivu, wakati suala hili linapoendelea kufanyiwa uchunguzi.
"Wakristo tuendelee kuhubiri amani, kuombea amani kwa sababu Mungu wetu ni wa amani," alisema Askofu Malasusa.
Aidha Balozi Padilla pamoja na Askofu Lebulu na
viongozi mbalimbali wa Kanisa Katoliki,  walifika Hospitali ya Mount Meru, kwa ajili ya kuwaombea waathirika wa mabomu hayo, na kuwapa pole.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alifika hospitalini hapo kuwapa pole majeruhi waliopata madhara mbalimbali, akiongozana na viongozi mbalimbali wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).
Nyalandu pamoja na Tanapa wametoa msaada wa mablangeti 50 yenye thamani ya Sh milioni 2.3, huku akiongeza kuwa Wizara kupitia Tanapa wameahidi kutoa Sh milioni 16.2, kwa ajili ya kununulia dawa pamoja na vifaa mbalimbali vya kuhudumia wagonjwa hao.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mount Meru, Dk Mariam Murktadha, aliishukuru wizara kwa msaada huo pamoja na wadau mbalimbali wanaojitokeza kuchangia damu na vifaa mbalimbali ili kuokoa maisha ya waathirika hao.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana, kimetaka watakaobainika kuhusika na tukio hilo, wachukuliwe hatua kali iwe fundisho na izuie matukio ya aina hiyo.
Aidha kimetaka Watanzania kushikamana na wenye taarifa juu ya watu wanaotuhumiwa kufanya shambulio hilo, wasaidie kuzitoa ili hatua zichukuliwe.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Makao Makuu ya chama hicho mjini Dodoma, Kinana aliitaka Serikali kufanya juhudi na kutumia taaluma za kila aina,
kunasa mtandao mzima wa uhalifu na kuchukua hatua stahiki.
Mwenyekiti wa  CHADEMA, ametuma salamu za pole
na rambirambi kwa waumini wa Kanisa Katoliki nchini na Watanzania wote kwa ujumla, kutokana na mlipuko huo. 
Mwenyekiti Mbowe ametoa salamu hizo alipozungumza kwa njia ya simu na Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Padri Antony Makundi, jioni ya Jumapili, baada ya kupata taarifa za tukio hilo.

No comments: