WATU 13 WAFA KWA KUFUNIKWA NA KIFUSI KATIKA MGODI ARUSHA...

Hali ilivyokuwa eneo la tukio jana.
Watu 13 wamekufa papo hapo huku zaidi ya 20 wakisadikiwa kufunikwa na kifusi wakati wakichimba mchanga kwenye machimbo yaliyoko Moshono nje kidogo ya hapa.

Tukio hilo ambalo limegubikwa na simanzi na vilio kwa ndugu, jamaa na wananchi wa eneo hilo, lilitokea jana  saa 5 asubuhi.
Marehemu hao na watu wengine walikuwa katika machimbo hayo wakichimba na kupakia mchanga huo aina ya  moramu hiyo kwenye magari ya watu binafsi kwa lengo la kuiuza kwa ajili ya ujenzi wa nyumba na kumwagwa barabarani kuondoa utelezi. 
Pamoja na vifo hivyo magari mawili aina ya Mitsubishi Fuso na Scania yaliharibiwa baada ya kufukiwa na kifusi hicho kilichoporomoka umbali wa meta 50 kutoka usawa wa bahari.
Jana kikosi cha uokoaji cha  Jeshi la Ulinzi la  Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kiliopoa miili minane.
Baadhi ya miili ilitambulika kuwa ya Alex Maliaki, Gerald Hamis, Sauli Rafael ‘Mbu’, Barick Loselian, Kababuu Lowasale, Mwenda Kibobori, Japhet Mjivaine na Gerald Masai.
Taarifa za mashuhuda zilibainisha kwamba chanzo cha kuporomoka kwa kifusi hicho ni mvua kubwa zinazoendelea kunyesha jijini hapa zikisababisha kukatika kwa ngema baada ya kuzidiwa na maji ya mvua.
Mkuu wa Mkoa Magesa Mulongo alilazimika kukatisha safari yake wakati  akielekea Dar es Salaam, baada ya kupata taarifa hiyo ya msiba.
Katika tukio hilo, viongozi wa vyama na Serikali walifika eneo la tukio akiwamo Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Meya wa Jiji Gaudence  Lyimo.
Akizungumzia tukio hilo akiwa Moshono, Mulongo alisema hadi jana watu 13 walithibitishwa kupoteza maisha. 
Aliongeza kuwa yeye na kundi la waokoaji wako eneo la tukio wakijitahidi kuokoa na kuopoa baadhi ya watu ambao inadaiwa bado wamefukiwa na kifusi hicho.
“Nilikuwa njiani kwenda Dar es Salaam, lakini baada ya taarifa hii imebidi nigeuze na kuja hapa kushirikiana na viongozi wengine kusimamia shughuli ya uokoaji,” alisema Mkuu wa Mkoa.
Mulongo alitaka wananchi wa Arusha kujihadhari na mvua inayoendelea kunyesha mfululizo ili kuepuka maafa mengine.
Alisema Serikali inapenda wananchi wake, lakini haiko tayari kuona watu wanapata maafa ambayo yanaepukika kama ya Mto wa Mbu kwani wananchi wale walishaambiwa kuhama mabondeni.

Comments

Popular Posts