WANAJESHI WAWILI KORTINI KWA MAUAJI YA KUKUSUDIA YA DEREVA WA BAJAJI KAWE...

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Watu watatu wakiwamo wanajeshi wawili wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka ya kuua kwa kukusudia.

Wanajeshi hao wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ni MT 95735 Noah Lusivuni (25) mkazi wa Lugalo na MT 99170 Raphael Masha (29) mkazi wa Mabibo External na mlinzi Reverian Paul (40) mkazi wa Mbezi Beach.
Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Binge Mashabala.
Wakili wa Serikali, Leonard Challo, alidai mahakamani hapo kuwa washitakiwa walitenda kosa hilo Aprili 3 eneo la Kawe, Kinondoni.
Challo alidai kuwa washitakiwa hao kwa makusudi walimwua Yohana Mbelwa, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.
Washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote, kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji isipokuwa Mahakama Kuu pekee. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Aprili 29 itakapotajwa.
Katika hatua nyingine, askari Magereza namba B7947 WDR Brighton Sakaya (23) mkazi wa Kimara Stop Over, Kinondoni, alipandishwa kizimbani akikabiliwa na mashitaka ya kukutwa na dawa za kulevya.
Wakili wa Serikali, Hellen Moshi, alidai mbele ya Hakimu Mkazi Aloyce Katemana,  kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Aprili 7 katika gereza la Keko, Temeke.
Ilidaiwa kuwa mshitakiwa alikutwa na dawa za kulevya aina ya heroine gramu 20.23 zenye thamani ya Sh 910,350.
Mshitakiwa alikana mashitaka na kurudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
Masharti yalimtaka kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika ambao wanafanya kazi katika taasisi inayotambuliwa kisheria na kuwa na makazi ya kudumu, ambao wangesaini hati ya dhamana ya Sh milioni 1.5 kila mmoja. Kesi hiyo itatajwa tena Aprili 26.

No comments: