UHURU KENYATTA AAPISHWA, ODINGA ASUSIA NA KUTIMKIA AFRIKA KUSINI...

Uhuru Kenyatta akiapa kuwa Rais wa nne wa Kenya mapema jana. Kulia ni mkewe, Margaret.
Rais  wa Kenya, Uhuru Kenyatta, ameapishwa rasmi jana nchini humo na kuwatangazia wa Kenya kuwa ndani ya siku 100 atakazokuwa ofisini, atatekeleza sehemu ya ahadi alizotoa.

Akihutubia taifa la Kenya na mazungumzo yake kurushwa moja kwa moja na runinga, Rais Kenyata alisema, kubwa atakalosimamia ni amani, umoja na mshikamano wa wananchi wake.
Rais Kenyatta alisema ndani ya siku hizo, atahahikisha suala la kuwatoza fedha wazazi na wananchi wa nchi hiyo kwa ajili ya matibabu, linakoma katika zahanati zote za umma.
"Hiyo ni kwa sababu zahanati za umma ni za Wakenya kwa hiyo, nimejipanga kuhakikisha huduma zinatolewa bure. Kwa maana hiyo ninafuta malipo yaliyokuwa yakitozwa kwa wazazi na watu wengine, ili wayapate bure," alisema Rais Kenyatta.
Aidha, alitangaza neema kwa wanawake na vijana wa nchini humo , kuwa fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya uchaguzi wa marudio, Sh bilioni 6 za Kenya, sasa    zitaingizwa kwenye miradi yao ya maendeleo, bila kubagua eneo wanakotoka nchini humo au kiongozi waliyempigia kura.
Hakuwasahau wanafunzi wa shule za Serikali,  ambapo alisema kila mmoja wao atapewa kompyuta ya mkononi (laptop), ikiwa ni mkakati wa uongozi huo kuhakikisha hawabaki nyuma kimaendeleo.
Katika sherehe hizo, ambazo Rais Jakaya Kikwete aliwawakilisha Watanzania na kupamba na nyimbo mbalimbali, ikiwemo Wimbo wa Afrika Mashariki na Wimbo wa Taifa la Tanzania, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alizungumza kwa niaba ya wakuu wenzake wa nchi.
Katika hotuba yake, Museveni aliwasifu Wakenya kwa kupiga kura kuikataa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Aliibeza mahakama hiyo na kusema imekuwa ikitumika kuwaondoa viongozi wa Afrika, isiyowahitaji madarakani, na kuwaweka viongozi wanaowataka.
Naye Rais mstaafu wa Kenya, Mwai Kibaki, aliwashukuru wananchi wa nchi hiyo na kuwaeleza kuwa walikuwa msaada mkubwa kwake katika utekelezaji wa majukumu yake kama Rais.
Alisema, mafanikio yote yaliyopo Kenya sasa ni mchango wa wananchi hao hivyo wanapaswa kujivunia.

Lakini wakati Uhuru akiapishwa, taarifa zilizopatikana baadaye zilisema kwamba aliyekuwa mpinzani wake karibu, Raila Odinga na timu yake halisusia sherehe hizo na kutimkia Afrika Kusini kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kwenda kujipumzisha akili baada ya mchakato mzito wa kinyang'anyiro cha urais.
Vyanzo vimeeleza kwamba Raila na wenzake wamekuwa wakitumbua maraha nchini humo kana kwamba hawajui nini kinachoendelea nchini mwao.
Vyanzo hivyo vimesema kwamba uamuzi huo unadhihirisha kwamba bado Odinga ana kinyongo dhidi ya ushindi alioupata Kenyatta, hali inayotishia amani na utulivu wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

No comments: