UDINI WAVURUGA MCHAKATO WA KATIBA MPYA...

Jaji Joseph Warioba.
Udini na siasa za uanaharakati vinaonekana kuanza kutafuna na kuathiri utamaduni wa Watanzania na mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya.

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari, kuhusu sintofamu iliyoibuka katika uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ya kata.
Jaji Warioba alisema sehemu kubwa ya matatizo yaliyojitokeza, yalisababishwa na na misukumo na misimamo ya kisiasa na kidini.
“Watanzania tumekuwa na utamaduni wa kutobaguana kwa misingi yoyote ikiwamo ya dini na ukabila, lakini sasa mambo hayako hivyo.
“Katika baadhi ya maeneo, mikutano ya uchaguzi ngazi za vijiji, mitaa na shehia ilishindwa kufanyika, kutokana na mivutano ya kisiasa na kidini iliyosababishwa na baadhi ya wananchi kufungamanisha uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ya Katiba ya wilaya na masuala ya kisiasa na kidini,” alisema Jaji Warioba.
Kutokana na changamoto hiyo, Warioba alisema Tume, itachukua uamuzi mgumu katika kuandaa rasimu ya Katiba itakayoweka mbele maslahi ya Taifa na kamwe haitapokea shinikizo kutoka taasisi, asasi, makundi au vyama vya siasa.
Alihadharisha kuwa kama kuna wajumbe wanakwenda kwenye mabaraza hayo, kwa kutumwa na vyama vya siasa au dini zao, Tume itazingatia hoja za msingi zinazoisaidia nchi na si wingi wao. 
Tume ilihadharisha Watanzania kuwa kila kundi liking’ang’ania mapendekezo yake yawekwe kwenye Katiba hiyo, kuna uwezekano Tanzania isipate Katiba mpya katika muda  uliotajwa katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ni mwakani.
Kwa hali hiyo, Warioba alitaka wananchi nao kuchukua uamuzi mgumu, kukubaliana na mapendekezo ya Tume na si kung’ang’ania misimamo ya vyama na dini zao.
“Kila mtu akitaka jambo lake ndilo lichukuliwe hatutafanikiwa, hatuwezi kukwepa kufanya uamuzi mgumu katika uandaaji wa Katiba ya nchi,” alisema.
Akifafanua kuhusu uamuzi mgumu watakaofanya, Jaji Warioba alitoa mfano: “Kuna wananchi wanataka Muungano uvunjwe, wengine wanataka serikali mbili, tatu, nne (Serikali ya Muungano, ya Tanzania Bara, ya Unguja na ya Pemba) na wengine wanataka Serikali moja… kuna wanaotaka Muungano wa Mkataba.
“Lakini wananchi wengine wanataka madaraka ya Rais yapunguzwe, wengine wanapinga hilo na wengine wanataka Rais aondolewe kinga. Pia kuna wengine wanataka muundo wa majimbo, wengine hawataki… ni lazima tufanye uamuzi mgumu katika rasimu tutakayoandaa,” alisema.
Jaji Warioba aliomba wananchi wajadili rasimu ya Katiba na kutoa maoni yao katika mabaraza ya Katiba yatakayokutana kuanzia Juni.
Alisisitiza kuwa Tume itashawishi wajumbe hao kukubaliana na mambo ya msingi yaliyopendekezwa nayo  na kuachana na misimamo ya makundi yao.
Kuhusu malalamiko kuwa baadhi ya vyama vimevuruga mabaraza hayo kwa kuchagua wanachama wao wengi, Jaji Warioba alisema katika kuandaa rasimu, Tume haitapokea shinikizo kutoka taasisi, asasi, makundi au vyama vya siasa.
“Tume haitengenezi Katiba ya vikundi au vyama, tunaandaa Katiba ya nchi,” alisema Jaji Warioba na kuongeza: “Hao waliojazana kwenye mabaraza wanadhani wanakuja kupiga kura, hapana …Tume inazingatia uzito wa hoja zilizotolewa na wananchi na si idadi ya watu waliotoa maoni.”
Alihadharisha wananchi watakaokwenda kutoa maoni yao katika mabaraza ya kata, kutokubali kutumiwa na makundi, asasi, taasisi na vyama wakati wa kujadili na kutoa maoni katika mabaraza ya Katiba ya wilaya. 
Warioba alitaja changamoto nyingine zilizojitokeza, kuwa ni pamoja na baadhi ya wananchi kujiingiza katika vitendo vya rushwa katika uchaguzi huo, ili wapendekezwe kuwa wajumbe wa mabaraza hayo. 
“Tumepokea pia malalamiko ya vitendo vya rushwa,” alisema Mwenyekiti huyo na kuongeza kuwa vitendo hivyo ni kinyume cha sheria na kuongeza kuwa taasisi zenye mamlaka ya kupambana na vitendo hivyo, zinapaswa kushughulikia malalamiko hayo.
Alipoulizwa ni hatua gani Tume itachukua kwa uchaguzi ambao ulitawaliwa na rushwa, alisema Tume haishughuliki na watu waliopokea rushwa bali wenye jukumu ni vyombo vya Dola.
Kuhusu madai ya baadhi ya wanasiasa hususan wa Chadema, kutishia kususia mchakato wa Katiba kutokana na uchaguzi wa mabaraza hayo kuvurugwa, Mwenyekiti alijibu: “Sitaki kujiingiza kwenye malumbano ya kisiasa, sisi tunakwenda kwa wananchi kupata maoni kuhusu rasimu ya Katiba.”
Jaji Warioba katika mazungumzo hayo, alisema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba imetoa fursa ya kuundwa kwa mabaraza ya aina mbili; mabaraza yatakayosimamiwa na kuendeshwa na Tume katika muda na tarehe itakayopangwa.
Aina ya pili, kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, ni mabaraza ya Katiba ya asasi, taasisi na makundi mbalimbali yenye malengo yanayofanana. Mabaraza hayo yatajiunda, yatajisimamia na kujiendesha na kuwasilisha maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba ndani ya muda utakaopangwa na Tume.
“Kazi kubwa ya mabaraza hayo ya Katiba ni kupitia, kujadili na kutolea maoni rasimu ya Katiba itakayokuwa imeandaliwa na Tume kutokana na maoni yaliyokusanywa na wananchi,” alisema Jaji Warioba.
Aliziomba taasisi, makundi, asasi na vyama kutumia fursa hiyo ya kisheria kuunda mabaraza na kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba itakayotolewa.
Pia alisisitiza kuwa mabaraza hayo hayatapiga kura, kwani hatua ya kupiga kura iko kwenye Bunge la Katiba na si vinginevyo.
“Kwa sasa vyama viwaache wananchi watoe maoni yao, muda wa makundi upo nao watasema yao,” alisema Mwenyekiti huyo.
Kuhusu ushiriki wa walemavu katika mabaraza ya Katiba, Jaji Warioba alisema Tume yake inatarajia kuunda mabaraza ya Katiba ya wenye ulemavu, ili kuwapa fursa  kutoa maoni kuhusu rasimu ya Katiba.
Hatua hiyo ya Tume inatokana na Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) na Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (UWAZA) kwa Tume kuunda mabaraza maalumu ya kundi hilo.
Mabaraza hayo yatakayoundwa Bara na Zanzibar  yatashirikisha wananchi kutoka ngazi ya chini ya wilaya hadi Taifa.
“Tunaelewa kuwa watu wenye ulemavu ni karibu asilimia 10 ya Watanzania wote na mchakato huu hauwezi kuwatenga katika ngazi yoyote,” alisema Jaji Warioba.
Jaji Warioba  alisema katika uchaguzi wa mabaraza ya mitaa, vijiji, vitongoji na shehia, tathmini ya Tume yake inaonesha sehemu kuwa ya viongozi na watendaji katika ngazi zote walizingatia mwongozo uliotolewa na Tume na kuwa maeneo mengi wananchi walichaguana kwa amani na utulivu.
Alitoa mfano kuwa katika shehia 323 (asilimia 96.4) kati ya shehia 335 Zanzibar zimekamilisha mchakato huo na kata 3,331 (asilimia 99.8) kati ya 3,339  Bara, nazo zimekamilisha mchakato wa kupata wajumbe wa mabaraza ya Katiba ya wilaya kwa kuzingatia utaratibu uliotolewa kwa mujibu wa mwongozo.
Hatua inayofuata kwa mujibu wa Jaji Warioba, Tume inaendelea kupokea majina kutoka kwa mamlaka za Serikali za Mitaa ya wote waliopendekezwa kutoka katika kata na shehia, na kazi hiyo inatarajiwa kukamilika leo.

No comments: