SPIKA SASA KUDHIBITI WABUNGE KWA KUTUMIA POLISI...

Spika Anne Makinda.
Baada ya kikao cha juzi cha Bunge kukithiri matusi ya wabunge, hali hiyo imemkera Spika Anne Makinda ametangaza kutumia polisi wa Bunge, kukamata na kumtoa nje mbunge atakayetukana wakati wa kuchangia hoja.

Makinda hakuwapo katika kikao cha juzi, kilichotawaliwa na matusi kutoka kwa wabunge, kikiongozwa na Naibu wake, Job Ndugai.
 “Kwa bahati mbaya jana sijui wabunge mlikumbwa na kitu gani, badala ya kujadili hoja mlitumia muda mwingi kutoa matusi. Mnaonekana mmevaa suti nzuri; lakini mnatoa lugha za matusi vinywani mwenu. Kauli mlizotoa jana (juzi) hazifanani na mlivyovaa kiheshima.
“Baada ya yale matusi yenu ya jana, nimepokea ujumbe wa maneno mwananchi akiniambia; ‘kwa hali ilivyo bungeni kwenu, sitakaa tena na watoto sebuleni kuangalia Bunge, nitakuwa naangalia chumbani,” alisema Makinda akinukuu ujumbe wa maneno aliotumiwa.
Makinda alihoji: “Hivi tumeanzisha vyama vingi vije vishindane hapa kwa matusi? Hii ni aibu...ni aibu kubwa kwenu, naombeni mjiheshimu na kuanzia sasa atakayetoa matusi, nitamwita polisi amchukue na hii ni kwa wabunge wa vyama vyote.
“Utakata rufaa baadaye, lakini tayari umeshachukuliwa na polisi. Hatuwezi kuvumilia suala hili liendelee kutokea humu bungeni na kama mnataka kutukanana tutawatengea chumba maalumu mkatukanane hadi mchoke,” alisema Makinda.
Hatua hiyo ya Makinda, inatokana na wabunge juzi wakati wanajadili hotuba ya Waziri Mkuu, kutoleana lugha chafu. Wabunge wa vyama vya CCM, CUF na Chadema, walishiriki kutoa lugha hizo.
Wabunge ambao wanatuhumiwa kutoa matusi juzi kwa upande wa CCM, ni wa Kondoa Kusini Juma Nkamia, ambaye alimwita Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Chadema), kuwa ni mbwa na hawezi kuzungumza naye bali na mwenye mbwa.
Mbunge huyo pia alimwita Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), kuwa si mtu makini, hivyo hawezi kutilia maanani hoja zake.
Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, alitoa lugha za matusi na za kuudhi, wakati akichangia aliposema kuwa ndani ya Bunge kuna wabunge wana mimba zisizotarajiwa.
Kauli hiyo, ilikemewa na Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah (CCM), kuwa kauli hiyo ni ya udhalilishaji wanawake.
Kwa upande wa wabunge wa Chadema, wanaotuhumiwa kutoa lugha za matusi ni wa Nyamagana, Ezekiah Wenje na Peter Msigwa wa Iringa Mjini ambao mchango wao ulifanya Bunge wakati wa jioni uache kujadili hoja ya msingi ya Waziri Mkuu, badala yake wabunge wengi waliosimama walijibu mapigo.
Katika mchango wake, Wenje alisema Serikali ya CCM haina uwezo, legelege na imekosa meno katika kushughulikia masuala ya msingi. Lakini kauli aliyotumia kuwa the Government is impotent, incompetent  ilitafasiriwa na wabunge hao kuwa ameiita Serikali kuwa haina nguvu za kiume.
Kwa upande wake, Msigwa, alitumia Biblia kutukana viongozi wa Serikali kuwa ni wapumbavu na kwamba utendaji wanaofanya ni sawa na kuruhusu akili ndogo kutawala akili kubwa.
Alinukuu Kitabu cha Mithali 27:22 kinachosema kuwa ‘mpumbavu ukimchukua, ukimchanganya na ngano kwenye kinu atabaki na upumbavu wake.’
Michango ya wabunge hao ililalamikiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, ambaye alisema michango ya Msigwa na Wenje ni matusi ya dhahiri.
Mbunge wa Konde, Khatibu Saidi Haji, wakati akichangia, alionesha kuchukizwa na hotuba ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe ya kuhoji idadi ya Wazanzibari katika Tume ya Kurekebisha Katiba.
Mbunge huyo katika mchango wake alisema; “Mbowe kaja hapa anajambajamba tu,” kauli ambayo ililalamikiwa na Wenje kuwa ni matusi na kuonya kuwa kauli hizo za ajabu ni hatari katika ustawi wa mijadala ya Bunge.
Khatibu pia alimshambulia Msigwa, kwa kudai kuwa Zanzibar kuna udini na akamweleza kuwa Zanzibar ina desturi zake, hivyo mtu yeyote anayekwenda huko, ni lazima azifuate.
“Wewe Msigwa hivi kweli wewe ni mchungaji wa watu au mchungaji wa nguruwe?” Alihoji.
Kauli hiyo ilimkera Msigwa, ambaye aliomba Mwongozo wa Spika, kuhusu hoja ya mbunge huyo na kusema tatizo la Wazanzibari hawataki kuguswa na kuhoji baadhi ya mambo wanayofanya, likiwamo la kulazimisha watu wanaoishi Zanzibar wafunge, wakati nchini wanakaa watu wa dini tofauti.
“Tatizo la ninyi Wazanzibari hamtaki kuguswa, na mimi nawaambia kamwe hamuwezi kuigeuza Tanzania kuwa nchi ya Kiislamu,” alisema Msigwa.
Mbunge wa Magomeni Muhammad Amour Chombo (CCM) akionesha kukasirishwa na kauli ya Wenje iliyotafasiriwa kuwa ameiita Serikali kuwa haina nguvu za kiume, alisema; “Sawa Serikali yetu haina nguvu za kiume, lakini niseme kuwa wewe Wenje ni sawa na mfano wa uzi wa kuulainisha kabla ya kuingizwa kwenye tundu la sindano”.
Usemi huo ulishangiliwa na wabunge wa CCM, jambo ambalo linaashiria kuwa lilikuwa ni tusi kwa mbunge huyo wa Nyamagana.
Chombo pia alimshambulia Msigwa kuwa si mchungaji wa kweli wa watu na akaungana na Khatib kuwa yawezekana ni mchungaji wa nguruwe.

No comments: