MZIMU WA MAUAJI YA ALBINO WAMNYIMA USINGIZI PINDA...

Waziri Mkuu Mizengo Pinda akilia bungeni wakati alipokuwa akizungumzia suala la mauaji ya albino.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema ni aibu kwa nchi kuendelea kushuhudia vitendo vya kuuawa na kukatwa viungo kwa watu wenye albinism.

Pamoja na kauli hiyo ya Waziri Mkuu, Chama cha wenye Albinism Tanzania (TAS) kimeomba makachero wa taasisi ya FBI kutoka Marekani waombwe kuja nchini kuchunguza wanaowaua au kuwakata viungo.
Pinda alitoa kauli hiyo wakati akifungua semina kwa wabunge kuhusu changamoto zinazowakabili watu hao wenye albinism, kwa lengo la kuwapa uelewa mpana wabunge hao. Semina hiyo imeandaliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) chini ya mradi wa kuwajengea uwezo wabunge.
“Hili la fikra za kishirikina dhidi ya albino ndipo kwenye aibu ya nchi…kwa nini ukipata kiungo chake mambo yakunyookee? Ukatili huu ulianza mwaka 2007 hadi sasa na hakuna aliyetajirika maana tungewaona mabilionea wengi,” alikemea Pinda ambaye amewahi kulia bungeni kutokana na mauaji ya albino.
Pinda, ambaye anaishi na watoto watatu albino nyumbani kwake na kusomesha wengine wawili, lakini mmoja wao amefariki hivi karibuni kwa saratani ya ngozi, alisema ushirikina dhidi ya wenye albinism msingi wake ni elimu ndogo kwa watu pamoja na watu hao kuwa na imani ndogo ya dini.
“Mimi kati ya watoto wangu wawili ninaowasomesha mmoja alianza kichunusi tukaona ni kawaida, lakini baadaye ikabadilika na kuwa chunusi ngumu ndipo mimi na mama yake tukampeleka Ocean Road (Taasisi ya Saratani ya Ocean Road) na ikabainika ni kansa ya ngozi, akapatiwa tiba lakini tulikuwa tumechelewa akafariki dunia,” alisema.
Naye Spika Anne Makinda aliwataka wabunge kuangalia namna ya kutatua matatizo ya wenye albinism bila kutegemea fedha za wafadhili.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Chama cha wenye Albinism Tanzania (TAS), Ernest Kimaya alisema, “Zanzibar tumeona mchungaji kauawa lakini picha ilipatikana na mtuhumiwa wa mauaji kapatikana, tunaomba wabunge mtusaidie kupata usaidizi wa kimataifa watumike FBI na mauaji yataondoka”.
Alisema huu ni mwaka wa saba wanapigania Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kutambua idadi ya watoto wenye albinism kuanzia shule za msingi ili wanapopelekewa mitihani waweze kuongezewa muda na maandishi kuwa makubwa.
“Suala la mauaji limetufanya turudi nyuma kimaendeleo kwa hofu ya kuuawa kwani kama mtu alikuwa anakwenda shamba haendi. Hata hivyo hali hiyo sasa kidogo imetulia na tunaendelea kupambana na mzizi wa mauaji haya,” alisema Kimaya.
Wakichangia katika semina hiyo, Mbunge wa Busega, Dk  Titus Kamani (CCM) alisema halmashauri ziweke mazingira maalumu kuwahudumia wenye albinism kwa kusambaza dawa za kuwahudumia.
Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM) aliomba wa wabunge wawachangie angalau Sh 70,000 katika posho yao ya siku moja ya kikao kwa ajili ya vipindi vya redio na televisheni vya kutoa elimu ya kuzuia mauaji ya wenye albinism. Hata hivyo, Spika Anne Makinda baada ya kuwahoji na kukubali alisema watakatwa moja kwa moja posho hizo. Hii ina maana kwamba, kama posho ya kikao ya Sh 70,000 itakatwa kwa wabunge wote 350 kwa siku moja, kiasi cha Sh milioni 24.5 kitapatikana.
Naye Mpanda Mjini, Said Amour Arfi (Chadema) alisema kuwekwe utaratibu wa wenye albinism wanaohitaji tiba Hospitali ya Bugando na Ocean Road kuwezeshwa kufika huko badala ya kusubiri kibali kutoka kwa Katibu Tawala wa Wilaya ili wachangishe fedha za kuwafikisha kwenye hospitali hizo.
Mbunge wa Kisarawe, Selemani Jaffo (CCM) alitaka wabunge katika bajeti ya mwaka wa fedha 2013/2014 itakapoletwa bungeni kuhakikisha kodi inaondolewa kwenye vifaa vya walemavu wote na dawa za kuwakinga wenye albinism na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road iangaliwe kwa karibu ili kuwahudumia vizuri.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy (CCM) alisema, “Dar es Salaam kumejaa vibao vya waganga wa jadi kuanzia uwanja wa ndege hadi unafika Manzese, serikali iving’oe vibao vyote kwani wao ndo wanaoshawishi mauaji haya.”

No comments: