MABAKI YA ALIYEUAWA NA KUNYOFOLEWA VIUNGO YAFUKULIWA...

Mabaki ya mwili wa mwanamume mmoja aliyeuawa na kuchukuliwa baadhi ya viungo vyake zikiwemo sehemu za siri na kuchunwa ngozi yaliyokuwa yamezikwa yamefukuliwa tena na kuchukuliwa na ndugu zake baada ya kutambuliwa.
Ofisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoani Mara, Jaffar Mohammed alisema kwa njia ya simu kutoka mjini Musoma kuwa mabaki hayo yalifukuliwa juzi na kuchukuliwa vipimo kwa ajili ya uchunguzi zaidi na kisha kukabidhiwa kwa ndugu zake baada ya kumtambua kwamba ni ndugu yao.
Mohamed alisema kuwa mwanamume huyo aliuawa na kuchukuliwa baadhi ya viungo vyake ikiwa ni pamoja na miguu yote miwili, pamoja na sehemu za siri na kuchunwa ngozi na wauaji hao wakayatelekeza mabaki ya mwili huo kandokando ya mlima Kurwirwi ulioko kijijini hapo.
“Mwanamume huyo aliuawa na kuchukuliwa baadhi ya viungo vyake, mabaki ya mwili wake yalizikwa na wananchi katika eneo hilo kwa sababu alikuwa hajatambuliwa.... lakini jana (juzi) ndugu zake walijitokeza na tukatoa kibali cha kufukua mabaki hayo na kutambuliwa na ndugu zake, tulichukua baadhi ya vipimo,” alisema.
Kamanda huyo alisema kuwa tukio la kuuawa mwanamume huyo lilitokea Machi 31 mwaka huu, majira ya saa 7:30 usiku katika kitongoji cha Mwibara Kijiji na Kata ya Igundu wilayani Bunda.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Igundu Deus Kuliga alisema kuwa mwanamume huyo ametambuliwa kwa jina la Sagini Lutenga mkazi wa Kijiji cha Katoro wilayani Geita na kwamba alikuwa akifanya kazi ya kuchunga ng’ombe mali ya Diwani mstaafu wa Kata ya Igundu aliyetambuliwa kwa jina la Machumu Malima.
Kuliga alisema kuwa mabaki ya mwili wa mwanamume huyo yaligunduliwa na wapita njia na kwamba yalizikwa katika eneo hilo na juzi yalifukuliwa na kupelekwa kijijini kwao wilayani Geita kwa ajili ya maziko.
Kamanda Mohammed alisema kwa kufuatia tukio hilo Polisi inamshikilia Diwani Malima, pamoja na mwananchi mmoja aliyetambuliwa kwa jina Agnes Nyamwero, mkazi wa kata hiyo na kuongeza  kuwa upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea na vipimo vimepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.

No comments: