KIGOGO WA POLISI AHUSISHWA WIZI WA SHABA YA SHILINGI MILIONI 800...

Shaba.
Ofisa mwandamizi wa Jeshi la Polisi nchini, anahusishwa na wizi wa shehena ya shaba yenye thamani ya Sh milioni 800 iliyokuwa ikitoka nje ya nchi kwenda bandari ya Dar es Salaam.

Kuhusika kwa askari huyo (jina tunalo) kunatokana na kuonekana akitumia gari ambalo baadaye lilikamatwa na Polisi likiwa eneo ambako shaba hiyo ilikuwa imefichwa baada ya kuibwa.
Afande huyo mwenye cheo cha Mrakibu wa Polisi anadaiwa kushirikiana na askari mwenzake mwenye cheo cha chini cha Koplo Mpelelezi.
Wawili hao kabla ya kufanyika wizi huo Aprili 5 walionekana wakiwa na gari hilo aina ya Noah namba T 785 BTM lililokamatwa baadaye kwenye yadi iliyoko eneo la Bank Club, Mtoni Kwa Aziz Ally, kulikohifadhiwa shaba hizo za wizi.
Tukio hilo pia lilihusisha askari mwingine mwenye cheo cha sajini ambaye inadaiwa alishiriki akitumia gari la Polisi aina ya Toyota Land Cruiser (namba tunazo).
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, taarifa iliyofika katika kituo cha Polisi Chang’ombe, ilisema shaba hiyo iliibwa kutoka lori la kampuni ya Dhandho lenye namba T 758 BKZ na tela namba T 117 BMF aina ya Isuzu lililokuwa na shehena hiyo likitoka Zambia.
Taarifa ilisema uongozi wa Dhandho ulibaini gari hilo kutoonekana katika mitambo katika ofisi ya Kinyerezi, Dar es Salaam na baadaye gari likaonekana Yombo Kilakala na baada ya muda, likawa limefika Mtoni Kwa Aziz Ally, ndipo wakaingiwa na hofu kuwa huenda limetekwa na watu wabaya.
“Ndipo walipoona umuhimu wa kutoa taarifa Polisi kwa msaada zaidi…mara moja polisi walifika kwenye yadi hiyo na kukuta tayari mzigo umefunguliwa na baadhi ya vipande vya shaba vimeondolewa.
“Walikutwa watu wengi ambao mara walipoona askari, waliruka ukuta ili kutoroka na polisi kutilia shaka mwenendo huo na kuchukua hatua za kuwafuatilia na kukamata watu sita,” kilisema chanzo hicho.
Majina ya raia waliokamatwa bila kuhusisha polisi tunayo na wamefunguliwa jalada la kesi namba CHA/IR/2545/2013.
Katika ukamataji huo wa Polisi, gari lingine aina ya Toyota Canter namba T 668 AMF lenye uzito wa tani tatu likiwa tayari limepakia mabando matatu ya shaba hiyo.
Upekuzi wa Polisi ulibaini jumla ya vipande 416 vya shaba vikiwa katika nyumba ya Erick na ikabainika pia kuwa yadi ulimofanyiwa wizi huo inamilikiwa na mtu aliyetambuliwa kwa jina moja la Rama vilimokutwa vipande 185 vya madini hayo.
Hata hivyo Rama hajakamatwa, lakini gari lake aina ya Noah lililotajwa kutumiwa na askari wa Polisi likiendeshwa na mtu anayeitwa Babu Ally, lilichukuliwa na Polisi.
Kana kwamba hiyo haitoshi, Aprili 6, Jeshi  la Polisi kituo cha Chang’ombe lilipata taarifa za kuwapo shaba nyingine eneo hilo hilo safari hii katika nyumba inayomilikiwa na mwanamke, ambaye jina lake kamili halikupatikana mara moja.
Hata polisi walipofika nyumbani kwa mama huyo kwa upekuzi hawakumkuta, lakini walifanikiwa kukuta vipande 222 vya shaba.
Kwa mujibu wa mtoa habari, magari yote matatu yanashikiliwa kituoni Chang’ombe sambamba na washukiwa hao huku vipande vyote 638 vya shaba vikiwa vimeokolewa na Polisi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alikiri Polisi kukamata vipande 650 vya shaba vyenye thamani ya dola za Marekani 167,000.
Alisema vipande hivyo vya shaba, vilikuwa vimeibwa wakati vikisafirishwa kutoka Kongo kupitia Bandari ya Dar es Salaam kwenda Uswisi.
Kova alisema shaba hiyo ilikamatwa baada ya kupewa taarifa na Meneja wa Kampuni ya Dhandho, kuhusu lori aina ya Isuzu kutoweka na vipande vya shaba.
Alidai uchunguzi wa awali, ulibaini kuwa lori hilo liliingizwa katika yadi bubu ya Ramadhan Yusuph, katika kiwanja namba 33, kinachomilikiwa na mama mjane, Agnes Jumaa, mkazi wa Mtoni kwa Aziz Ally, ambayo ilifunguliwa Februari mwaka huu.
Alitaja magari yaliyohusika katika tukio hilo, kuwa ni  lori hilo lililokuwa likiendeshwa na Goodluck Makundi, ambaye bado anatafutwa, baada ya kukimbia polisi na gari nyingine ni Toyota Canter, namba T 668 AMH, lililokutwa na vipande 231 vya shaba kutoka katika lori.
Alitaja gari lingine lililohusika kuwa ni Noah namba T 785 BMT linalosadikiwa kutumika katika matukio kadhaa ya kihalifu, linalodaiwa kumilikiwa na Ramadhan Yusuph.
Kutokana na wizi huo, alisema watu saba ambao majina yao yamehifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi, wamekamatwa na kuhojiwa, na uchunguzi wa awali umebaini kwamba kulikuwa na njama za wizi wa vipande hivyo kati ya Makundi na Yusuph.
Katika hatua nyingine, Kova alisema wanashikilia watu wanne, kwa tuhuma za kuhusika na uvunjaji wa mashine ya kutolea fedha ya NMB, Tabata, Kimanga kwa kutumia mitungi ya gesi.
Alisema katika mashine hiyo, kulikuwa na zaidi ya Sh milioni 150, lakini watuhumiwa ambao majina yao yamehifadhiwa kwa uchunguzi hawakuiba.
Kamanda Kova pia alisema wanashikiliwa watu watano, kwa tuhuma za kupatikana wakiwa na meno hayo yanayokadiriwa kuwa na uzito wa kilo 31 yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 30.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti wakiwa na meno manane na vipande 19 vya meno hayo katika matukio tofauti.
Alitaja waliokamatwa kuwa ni Seif Nassor, mkazi wa Buguruni ambaye alikamatwa na vipande 10, Said Rashid mkazi wa Mbagala na Ahmad Issa, mkazi wa Tunduru, ambao walikamatwa na meno manane na vipande viwili. Wengine ni Bakari Hassan na Masoud Juma wote wakazi wa Makabe ambao walikamatwa wakiwa na vipande saba.
Katika hatua nyingine, Kova alisema wanamshikilia Kondo Shomari, mkazi wa Buguruni Mnyamani, kwa tuhuma za kupatikana na ngozi nne za chui kinyume cha sheria.
Pia alisema wanashikilia Alidudu Ndumulan, mkazi wa Magomeni na Goodluck Raphael, mkazi wa Buza, kwa tuhuma za kupatikana na noti bandia 71 za Sh 10,000 walizokuwa wakizitoa kwa wakala wa Tigo-Pesa.
“Mbali na watuhumiwa hao, pia tumekamata bastola mbili katika matukio tofauti ambapo moja aina ya Glock 17 namba LZB iliyosajiliwa kwa namba TZ CAR 98189 ikiwa na risasi 12. Tuliikamata Mabibo na nyingine aina ya Serena namba 6828 na risasi 21, ilikamatwa Kipunguni Ilala,” alisema.
Pia katika msako uliofanywa Temeke, walikamata bunduki aina ya SMG namba 26081997 iliyokatwa kitako na mtutu ikiwa na magazini yake.

No comments: