KUSHOTO: Wasamaria wakifunika mwili wa trafiki huyo eneo la tukio. KULIA: Mtuhumiwa Jackson Simbo. |
Kesi inayomkabili dereva, Jackson Simbo anayetuhumiwa kumgonga na kumuua askari wa Usalama Barabarani, imeahirishwa tena mpaka Juni 3, mwaka huu, kutokana na Wakili anayeendesha kesi hiyo kuumwa.
Kesi hiyo ambayo ipo katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, iliahirishwa jana mbele ya Hakimu Mfawidhi Kwey Rusema kutokana na Wakili wa Serikali, Ladslaus Komanya kuwa mgonjwa.
Kwa mara ya kwanza, Simbo (43) alifikishwa Mahakamani hapo Machi 26, mwaka huu akikabiliwa na mashitaka ya kuingilia msafara wa kiongozi na kusababisha kifo cha askari.
Awali, Wakili Komanya alidai Machi 18, mwaka huu katika taa za kuongozea magari, eneo la Bamaga barabara ya Bagamoyo, Simbo akiwa dereva wa gari aina ya Landrover lenye namba za usajili T328 BML, aliendesha gari hilo kwa kasi na kuhatarisha maisha ya watu.
Alidai kutokana na kuendesha gari hilo kwa kasi na hali ya hatari, alimgonga askari WP 2492 Koplo Elikiza na kusababisha kifo chake.
Katika mashitaka ya pili siku hiyo, Simbo aliingilia msafara wa kiongozi na kutotii maelekezo ya ishara, yaliyotolewa na Koplo Elikiza ambaye alikuwa kazini.
Katika mashitaka mengine, Komanya alidai baada ya kumgonga askari huyo, Simbo alishindwa kuripoti tukio hilo la ajali katika kituo cha Polisi kilicho karibu na eneo hilo.
Hata hivyo, mshitakiwa alikana kutenda kosa hilo na yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili, waliotakiwa kusaini hati ya dhamana ya Sh milioni mbili.
No comments:
Post a Comment