Kamanda Charles Kenyela. |
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela amekanusha taarifa zilizoenezwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba alilishwa sumu au alikula sumu badala yake alidai kwamba taarifa hizo zilikuwa na lengo la kumchafua.
Akizungumza jana katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kenyela alisema ni kweli kwamba aliugua lakini hilo ni jambo la kawaida kwa binadamu yeyote na alitibiwa na kupona.
“Habari kwamba nililishwa sumu, ni za uzushi… mimi sijalishwa sumu, isipokuwa niliugua kama binadamu yeyote na nimetibiwa nimepona, hivyo habari za kwamba nilipewa sumu sijui zilikuwa na lengo gani ila mimi naona zililenga kunichafua,” alisema.
Alisema, “habari hizo ambazo hazikuwa na ukweli wowote zilileta usumbufu sana na hofu kwa wananchi wengi wakidhani kwamba ni kweli nililishwa sumu au nilitaka kujiua… nawatangazia kwamba sasa mimi ni mzima na ninaendelea na kazi na sina lengo la kumlaumu mtu”.
Alisema habari kama hizo ni fitina zilizopikwa na watu kwa malengo ya kutumia nafasi zao kumharibia. Alitaka wenye mapenzi naye wazipuuze.
No comments:
Post a Comment