DALADALA, MABASI YA MIKOANI, TRENI SASA NAULI JUU...

Baadhi ya mabasi yaendayo mikoani yakipakia abiria Stendi Kuu ya Mabasi Ubungo, Dar es Salaam.
Nauli kwa mabasi ya daladala jijini Dar es Salaam, yaendayo mikoani na usafiri wa treni katika Reli ya Kati, zimepanda kuanzia wiki ijayo.

Viwango vipya vya nauli vitaanza kutumika Ijumaa ijayo April 12 mwaka huu, ambapo nauli za daladala jijini Dar es Salaam, zimeongezeka na kiwango cha chini kitakuwa Sh 400 na cha juu Sh 750.
Aidha, wanafunzi wa shule mbalimbali ambao hutakiwa kuonesha kitambulisho wanaposafiri, nauli yao imepanda kutoka Sh 100 hadi Sh 200 kwa safari ya umbali wowote ndani ya jiji hilo.
Uamuzi huo ulitangazwa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra), Ahmad Kilima.
Kwa mujibu wa Kilima, hatua ya kupandisha nauli hizo, imefikiwa baada ya kupitia mapendekezo ya wadau kuhusu kupanda kwa gharama za uendeshaji, na kufanya michakato kujua uhalisia wake.
Kutokana na uamuzi huo, kwa umbali wa kilometa kati ya 0 hadi kumi, nauli itakuwa Sh 400 na mfano wa njia ya umbali huo, ni Kivukoni hadi Ubungo.
Kwa umbali wa njia ya kilometa 11 hadi 15, nauli itakuwa Sh 450 na mfano wa njia hiyo ni Mwenge hadi Temeke.
Kwa njia za kilometa 16 hadi 20, nauli itakuwa Sh 500 na mfano wa njia hiyo ni Tabata, Chang’ombe  hadi Kivukoni na kwa kilometa 21 hadi 25, nauli itakuwa Sh 600 na mfano ni kutoka Pugu Kajiungeni hadi Kariakoo.
Nauli ya juu kabisa jijini Dar es Salaam, itakuwa Sh 750 kwa njia za umbali wa kilometa 26 hadi 30 na mfano wake ni njia ya Kibamba hadi Kariakoo.
Sumatra kwa mujibu wa Kilima, itasimamia utaratibu wa kubandika nauli kwa kila njia katika daladala za njia husika.
Kilima alionya kuwa kwa usafiri wa mijini, abiria atatakiwa kuwa na tiketi na dereva atakayekatisha ruti, basi litafungiwa na dereva na kondakta, hawataruhusiwa tena kuendeha basi lenye leseni ya Sumatra.
Pia Sumatra imeagiza madereva na makondakta kuwa na sare nadhifu, ili kuboresha huduma.
Akitangaza nauli mpya za mikoani, Kilima alisema nauli zitaongezeka kwa asilimia 20.3 kwa mabasi ya kawaida, asilimia 16.9 kwa mabasi ya daraja la kati na asilimia 13.2 kwa mabasi ya daraja la juu.
Kutokana na hatua hiyo, kwa basi la kawaida kwa njia ya lami kwa kilometa moja, nauli itakuwa Sh 36.89 badala ya Sh 30.67 na kwa njia ya vumbi, nauli itakuwa Sh 46.11 kwa kilometa badala ya Sh 37.72.
Kwa basi la hadhi ya kati bila kujali katika lami au katika vumbi, nauli itakuwa Sh 53.22 kwa kilometa badala ya Sh.45.53. Kwa wanaopenda kusafiri na basi la hadhi ya juu pia bila kujali ni katika lami au katika vumbi, nauli  itakuwa Sh 58.47, kwa kilometa badala ya Sh.51.64.
Ili kubaini daraja la basi husika na kulipa nauli kuendana na gharama, Kilima alisema wanaanza na Mkoa wa Tanga ambapo mabasi yatawekewa vibao vyenye rangi kuonesha basi la daraja la juu litakalokuwa na rangi nyekundu, la kati bluu na lile la kawaida rangi nyeupe.
Kwa upande wa mabasi ya ruti ndefu, Kilima alisema ili  viwango vipya vya nauli viendane na ubora wa huduma, Sumatra imewaagiza wamiliki wa mabasi ya masafa marefu kutotumia wapigadebe kwa kuuza tiketi, bali ziuzwe kwenye ofisi au ndani ya mabasi kwa njiani.
Kuhusu usafiri wa Reli ya Kati, Mamlaka hiyo imeeleza kuwa ongezeko la nauli kabla ya hili jipya, mara ya mwisho ilikuwa 2009.
Alisema viwango vipya vya nauli za usafiri wa reli kutoka Dar es Salaam mpaka Kigoma kwa daraja la kwanza ni 75,700 badala ya 60,599.
Kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza Sh 74,800 badala ya 59,818, Dar es Salaam mpaka Tabora,  Sh 54,800 badlaa ya 43,859 na Dar es Salaa mpaka Dodoma  Sh 34,700 badala ya Sh 27,788.
Kilima alisema kwa daraja la pili, kutoka Dar es Salaam mpaka Kigoma Sh 55,400 badala ya 44,305, Dar es Salaam mpaka Mwanza Sh 54,700 badala ya 43,747, Dar es Salaa mpaka Tabora Sh.40,500 badala ya 32,364 na Dar es Salaam mpaka Dodoma ni Sh 26,400 badala ya Sh 21,092.
Kwa daraja la tatu  Dar es Salaam mpaka Kigoma ni Sh  27,500 badala ya Sh 19,084, Dar es Salaam mpaka Mwanza Sh 27,200 badala ya Sh 18,860, Dar es Salaam mpaka Tabora ni Sh 20,400 badala ya Sh 14,173 na Dar es Salaa mpaka Dodoma ni Sh 13,500 badala ya Sh  9,374.
Kutokana na ongezeko hilo, Shirika la Reli Tanzania (TRL), wameelekezwa kutumia mfumo wa utunzaji taarifa za abiria, ambapo wamepewa mwaka mmoja kukamilisha uanzishwaji wa matumizi ya mfumo huo.
Pia wametakiwa kuboresha mfumo wa kudhibiti mapato ya shirika, ili kuzuia uvujaji wa makusanyo ya fedha katika vituo ndani ya mabehewa, ambapo wametakiwa kutekeleza kwa miezi mitatu.
Pamoja na kuboresha huduma ya usafirishaji abiria, pia wametakiwa  kuhakikisha kuna mabehewa yenye huduma muhimu kama taa, maji safi, huduma za chakula na kuwa na vyoo bora na safi na abiria wakikata tiketi na kupakia, waonesha vitambulisho.
Akizungumzia ongezeko la tozo mbalimbali za kuhudumia meli katika bandari zinazomilikiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari  (TPA), Kilima alisema TPA kwa ilipendekeza kuongeza tozo kutoka asilimia saba hadi asilimia 400.
“Hata hivyo Mamlaka imeridhia ongezeko la gharama kwa wastani wa asilimia 34.3, gharama ambazo kwa mara ya mwisho zilifanyiwa mapitio mwaka 1994,”alisema.
Alitaja tozo 19 zilizoongezwa kati ya huduma 100 zinazotolewa bandalini, kuwa ni Tozo za Nahodha kuingiza meli itakayokuwa dola 150, badala ya dola 122.05.
Tozo za Bandari itakuwa dola 13.40, badala ya dola 10.00, tozo za kuongoza meli kuingia bandarini itakuwa dola 6.00 badala ya 4.50, tozo ya kuegesha meli, dola 0.50 badala ya 0.35.
Kilima alisema kabla ya kuanza kutoza viwango vipya,TPA wanapaswa kutoa taarifa ya utekelezaji wa maelekezo waliyopewa, ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma kwa wateja.
Pia TPA wametakiwa kuboresha usalama wa mizigo na shehena pamoja na kuimarisha ulinzi bandarini, na kuhakikisha hatua za ulinzi na usalama zinatekeleza kwa mujibu wa makubaliano ya kimataifa.
Kilima aliwahakikishia watumiaji wa bandari na wananchi kuwa, viwango vipya havitaathiri ushindani wa TPA na bandari nyingine, endapo wataongeza ubora wa huduma wanazotoa.

No comments: