MAKARDINALI WANAOCHAGUA PAPA MPYA KUNYANG'ANYWA MAWASILIANO...

Papa mpya atakayeongoza Kanisa Katoliki duniani, anatarajiwa kupatikana kati ya Machi 15 na 20 mwaka huu, kabla ya Juma Takatifu kuelekea Sikukuu ya Pasaka.
Kwa utaratibu wa sheria za Kanisa na mchakato wa kumpata kiongozi huyo unaoendelea hivi sasa huko Vatican, baada ya Papa Benedict XVI kujiuzulu rasmi Februari 28 mwaka huu, Papa mpya atapatikana wakati huo.
Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Askofu wa Jimbo la Rulenge, Mhashamu Severine Niwemugizi, aameliambia gazeti hili kwamba mkutano wa makadinali unaoendelea sasa,  ni kama semina na uchambuzi wa changamoto zinazolikabili Kanisa.
“Kinachoendelea sasa ni vikao vya maandalizi, ni kama semina ya kupitia na kujadili changamoto, ili kumuomba Mungu awape mtu anayeweza kushughulikia hali ya Kanisa iliyoko na kuyaendeleza mema ya kiimani yaliyofanywa na aliyetangulia,” alisema Askofu Niwemugizi.
Akifafanua namna Papa atakavyopatikana, Askofu Niwemugizi, alisema Sheria za Kanisa zinaeleza kuwa, siku 15 baada ya Papa aliyeko kufariki au kujiuzulu rasmi, Jopo la Makardinali wenye sifa za kumchagua kiongozi huyo, litakaa na katika muda wa siku tano kumchagua Papa mpya.
Utaratibu wa Kanisa Katoliki kumpata Papa, umeelezwa kuwa unategemea zaidi nguvu za Mungu katika kufanya uamuzi.
Makardinali wote 115 wenye sifa ya kuchagua ambayo moja ya sifa ni kuwa na umri chini ya miaka 80, baada ya siku 15 za kujadili changamoto za Kanisa,  huingia katika ukumbi wenye vyumba vya kuishi vyenye mahitaji yote na kujifungia kila mmoja katika chumba chake.
Katika vyumba hivyo, makadinali hao hujifungia  kwa siku zisizozidi tano, yaani kutoka Machi 15 hadi Machi 20 bila mawasiliano na mtu yeyote, ili kuepuka ushawishi na mwingiliano wa mawazo.
“Wanakuwa kama wafungwa, wakishaingia kwenye ukumbi wa kupiga kura kila mmoja anakuwa katika chumba chake, hapo hakuna kampeni, ni kumuomba Mungu tu, kusali, kufunga na kutafakari katika hizo siku tano na kupiga kura,” alisema.
Kura mara 200
Askofu Niwemugizi alisema, wahudumu maalumu walioteuliwa, hupeleka makaratasi ya kura na kuyaingiza katika kila chumba cha kardinali kwa utaratibu uliowekwa.
Utaratibu huo kwa mujibu wa Niwemugizi, unazuia kuonana na Kadinali na baada ya kuacha karatasi, Kadinali hutakiwa kuandika jina la mtu anayempendekeza na kurudisha karatasi ambayo huchukuliwa na mhudumu ambaye huipeleka eneo zinakohesabiwa.
“Hakuna kardinali anayeruhusiwa kutoka katika chumba chake kabla tangazo maalum la kutoka linalotolewa baada ya kumpata Papa, vyumba vina kila kitu na vyakula hupelekewa baada ya kuandika anachohitaji na kumpa muhudumu asubuhi kabla ya kura, hakuna simu wala mawasiliano yoyote chumbani,” alifafanua Askofu Niwemugizi.
Kwa utaratibu wa Kanisa hilo, Papa anapaswa kuchaguliwa kwa theluthi 2 ya kura zote zilizopigwa, na ikiwa idadi hiyo haijafikiwa, kura hizo huchomwa moto na moshi mweusi hutoka kuonesha Papa hajapatikana.
Baada ya hapo awamu nyingine ya kupiga kura hufanyika na kuendelea mpaka hapo atakapopatikana, ambapo kura hizo hichanganywa na kemikali itakayowezesha moshi mweupe kutoka baada ya kuchoma moto kura, kuashiria Papa amepatiaka na ndipo makadinali hutangaziwa kutoka katika vyumba hivyo.
Askofu Niwemugiza alifafanua kuwa, ndani ya siku hizo tano za kupiga kura, lazima Papa apatikane hata ikibidi kurudia kupiga kura kwa zaidi ya mara 200. 
Aidha kwa mujibu wa sheria hizo, mwanaume yeyote ndani ya kanisa hilo, mwenye daraja la Upadri na hadhi za Uaskofu na Ukardinali, anaweza kuteuliwa kuwa Papa na makardinali hao ikiwa atatajwa katika kura na kufikia theluthi 2.
Hata hivyo hilo haliwahi kutokea katika historia ya Kanisa kwani mara zote huwa ni miongoni mwa makardinali.
Askofu Niwemugiza alisema Kiongozi wa Jopo, ama wa sheria za Kanisa, ambaye huteuliwa kabla ya makadinali kuingia vyumbani, hujitokeza adharani katika chumba cha juu ambacho kiimani, kilitumiwa na mitume katika kanisa la kwanza, akiwemo Papa wa Kwanza, Mtakatifu Petro (Mtume) baada ya moshi mweupe kufuka, kumtangaza Papa.
Hatua hiyo hufuatia na kujitokeza kwa Papa mpya katika hadhara ya waumini, ambao wengi huwa katika maeneo mbalimbali wakiomba na kufuatilia suala hilo muhimu katika Kanisa.
Akijitokeza Papa, hapo kengele za Kanisa, furaha, hoi hoi na vifijo hufuatia kwa waumini watakaokuwa katika viwanja vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro na dunia nzima.
Hivi sasa makardinali kutoka nchi mbalimbali duniani wapo Vatican katika maandalizi ya Jopo (Conclave) la uchaguzi wa  la kuanzia Machi 15, ambalo ndio makadinali huingia vyumbani.
“Kinachoendelea wakati huu ni kupitia mafanikio ya Kanisa na changamoto zake, namna zilizvyoshughulikiwa kipindi cha Papa Benedict XVI ambaye sasa ni Papa mstaafu,” alisema.
Changamoto hizo ni pamoja na kutoa mwongozo wa namna ya kuomba na wapi Kanisa linaelekea, baada ya kumpata kiongozi mpya.
Askofu Niwemugizi alibainisha wazi kuwa, maandalizi hayo yatawaongoza wapiga kura kujua ni kiongozi wa aina gani anahitajika kuliongoza kanisa hilo.
“Vikao vya maandalizi ya sasa vinafanyika katika vipindi viwili, asubuhi na mchana. Ikitokea katika  siku hizo tano Papa hajapatikana, basi ni wazi Kanisa linaweza kuwa mashakani maana haijawahi kutokea,” alisema Askofu Niwemugizi ambaye ni Mtaalamu wa Sheria za Kanisa.
Papa Benedict XVI ambaye jina lake la ubatizo ni Joseph Ratzinger (85), aliaga rasmi Februari 28 baada ya kutangaza kujiuzulu mapema mwezi huo.
Kabla ya kuaga rasmi, aliwaaga makardinali na kisha waumini wa kanisa hilo katika Ibada iliyofanyika kwenye Viwanja vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro (St Peter), Vatican.
Ingawa kujiuzulu kwake kulishtua wengi, hasa waumini wa Kanisa hilo, kutokana na historia kuonesha kuwa, jambo kama hilo liliwahi kutokea karne kadhaa zilizopita katika miaka ya 1400, kumekuwa na mtizamo chanya wa hatua hiyo kama fundisho kwa wanaong’ang’ania madaraka hata pale wanapoona hawawezi.
Papa Benedict wa XVI ni mrithi wa Papa Yohana Paulo wa II, aliyefariki mwaka 2005. Sababu za kujiuzulu kwa kiongozi huyo zimeelezwa zinatokana na umri na matatizo ya kiafya. Pia kwa kujiuzulu kwake, aliachia nafasi ya kuwa Kiongozi Mkuu wa Serikali katika nchi ya Vatican.

No comments: