HOSPITALI NA SHULE ZA KANISA KATOLIKI KUWABEBA MASIKINI...

Mwalimu katika moja ya shule zinazomilikiwa na Kanisa Katoliki akiwa darasani.
Tabia ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis ya kuwa ni mtu asiyetabirika kiutawala, na aliyejitambulisha kuwa mtumishi kwa masikini, inatarajiwa kuleta neema kwa watoto wa masikini katika shule za Kanisa.
Mbali na watoto wa masikini katika shule za Kanisa, muonekano huo wa Papa, umesababisha pia Kanisa kuanza kufikiria namna ya kuwasaidia zaidi masikini, katika hospitali za Kanisa.
Akizungumza na mwandishi jana, Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Askofu wa Jimbo la Rulenge, Mhashamu Severine Niwemugizi, alisema anachokiona, Papa analenga kuwaweka karibu wahitaji waone thamani yao.
"Ametoka katika nchi iliyokuwa na tawala za kikomunisti, ukandamizaji wa watu ulikuwa mkubwa, anaelewa nini maana ya unyonge na umasikini.
"Ataweza kuwaleta wanyonge karibu zaidi na Kanisa na hili linadhihirika hata kutokana na jina alilochagua, Francis, Mtakatifu aliyetoka nyumbani kwao, kwenda kuishi na masikini," alisema Askofu Niwemugizi.
Alisema mwelekeo wa Papa Francis ni kuwawezesha masikini, ili waone thamani ya utu wao zaidi ya kupewa kitu kama fedha.
"Kuthaminiwa ni zaidi ya kupewa kitu, bila shaka analenga kuwaweka karibu wahitaji waone thamani yao," alisema Askofu Niwemugizi.
Papa Francis hakuwemo katika Utawala (Curia) ya Vatican, jambo linalowafanya wachambuzi waamini, anatarajiwa kuleta mabadiliko ya utawala yatakayohitaji watu wenye kuwajali masikini zaidi.
Hata hivyo, mabadiliko hayo yanaelezwa hayatakuwa makubwa, kwa kuwa tayari kupitia mitandao mbalimbali alishawataka watendaji wa Vatican, kila mmoja kutulia na kuendelea na kazi yake.
Kwa mujibu wa Askofu Niwemuzi, Papa Francis analenga kuzifanya jumuiya za kimataifa kutazama uumbaji wa Mungu, kulinda maisha na kupunguza ubinafsi.
Pia atarajiwa kuhamasisha mfumo wa huduma za jamii, wa kuondoa tofauti kwa kuweka namna ya matajiri kutumia utajiri wao, ili kuwezesha huduma kwa masikini na wahitaji.
Kwa upande wake, Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Method Kilaini, alisema Papa Francis ni mchungaji zaidi ya mtawala, muelekeo wake haupishani na Papa Yohana Paulo II, katika kuwarejesha walio mbali na Kanisa, kufanyia kazi changamoto kiutume zaidi ya utawala.
Alipoulizwa kuhusu shule za kanisa, ambazo zimekuwa ghali kuliko za Serikali na watu binafsi wengine, kama zitapungua ada, Niwemugizi alisema, "Ukipunguza sana, utasababisha huduma mbovu."
Alifafanua kwamba kikubwa ni kuwezesha walio nacho, kutoa zaidi kwa ajili ya wahitaji, ili wote wapate huduma sawa na bora, si katika shule tu, hata afya.
Papa Yohana Paulo II ndiye kiongozi wa juu wa kanisa hilo aliyetawala kwa muda mrefu katika kipindi cha karne za karibuni.
Yeye alitekeleza maazimio ya Mkutano Mkuu wa II wa Vatican ulioitishwa na Yohana wa XXIII mwaka 1962 hadi 1966. Mkutano huo, uliamua kujenga uhusiano na dini mbalimbali na kutafsiri Ibada katika lugha za mataifa mbalimbali kutoka Kilatini pekee.
Askofu Niwemuzi alifafanua, "Kanisa lilitaka kujitazama upya, Yohana Paulo II alitazama upya teolojia (mafundisho ya kanisa) na namna ya litrujia (uendeshaji wa ibada), alifanyia kazi pengo baina ya makanisa yaliyojitenga na Katoliki, huduma za jamii kama shule, afya na miradi."
Pia alitazama uhusiano baina ya kanisa na watu wasio Wakristo, alipitisha dhana ya Kanisa kuwatazama watu hao kama ndugu, maana watu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, aliwaleta pamoja viongozi wa dini mbalimbali katika mji wa Assisi, kusali kuomba amani katika dunia.
Kwa mujibu wa Askofu Niwemugizi, utekelezaji huu ulileta Katekisimu mpya ya Kanisa, iliyokuwa na ufupisho na tafsiri ya lugha za mataifa mbalimbali, ilitolewa mwaka 1992. Kutolewa kwa Katekisimu hiyo, ni mabadiliko makubwa kwa Kanisa.
Aidha Kanisa katika utawala wa Yohana Paulo II, iliweka Biblia katika matendo zaidi, huduma za jamii ziliimarishwa na kuwafikia wengi, kila alipokwenda katika ziara za misionari, alihamaisha Kanisa kutoa huduma za jamii, kuhudumia watu kiroho na kimwili bila kujali dini na imani zao.
Anaelezwa alichukua tahadhari ya kutenda zaidi ya umri wake wa miaka 78 aliokuwa nao. Alipunguza kasi ya mabadiliko ya kilitrujia, akarejesha mambo yaliyosahaulika, ikiwemo ibada ya misa la Kilatini kwa maeneo yaliokuwa yakitaka kuzitumia na alikazia uhusiano na dini nyingine.
Kuwepo kwa matukio ya kashfa kwa makasisi wa Kanisa, kulimuumiza kichwa Papa Benedict XVI na alitumia muda mrefu kushughulikia nidhamu ndani ya Kanisa na kuomba msamaha kwa makosa yote ya Kanisa kwa dunia.
"Alitazama uhusiano wa Kanisa Katoliki na Anglikana, wakati wa misukosuko ya ushoga ndani ya kanisa hilo lililojitenga na Katoliki, aliweka utaratibu wa namna ya kuwapokea Waanglikana waliogoma kukubali ushoga katika nchi zao, na walibaki kuwa Waanglikana," alifafanua Niwemugizi.
Hivi sasa Kanisa Katoliki limeweka mabadiliko katika litrujia ya Misa kwenye viitikio kote duniani, haya yalifanywa na Benedict. Misale ya Kirumi ilitafsiriwa upya ili kuleta ukaribu wa tafsiri inayowiana kabisa na Kilatini cha kwanza.

No comments: