WEZI WA MAJI DAR SASA WAFUNGA MOTA UVUNGUNI MWA KITANDA....

Mmoja wa wakazi wa Dar es Salaam akisubiria kupata huduma ya maji.
Wizi uliokithiri wa maji umegundulika katika Jiji la Dar es Salaam baada ya kiasi kikubwa cha mota za kusukumia kimiminika hicho kukutwa zimefungwa ndani ya vyumba vya ‘wezi’ hao.
Hatua hiyo imetokana na operesheni maalumu iliyoendeshwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick akishirikiana na vyombo vya Dola kutokana na kilio cha muda mrefu cha wakazi wa Jiji hilo kutokana na ukosefu wa huduma hiyo katika maeneo mengi.
Operesheni hiyo iliyofanyika jana ikimshirikisha pia Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana katika maeneo ya Kagera, Tandale, Urafiki na Mkwajuni.
Mota zaidi ya 25 zilikamatwa sambamba na pampu ambapo katika nyumba moja kulikuwa na mota hizo katika vyumba vya kulala, huku kabati likitumika kuficha mlango wa kuingia bafuni sehemu ambayo mabomba mengine yamefungwa. Watuhumiwa wawili walikamatwa.
Katika eneo hilo la Tandale mtaa wa Mkunduge, nyumba moja ikiwa na kisima cha maji nje ilibainika ikiendelea na biashara ya maji kwa wananchi wa eneo hilo, huku mota zikiwa kwenye vyumba vya kulala zikinyonya maji.
Meta chache kutoka hapo kuna kisima halali cha maji ya Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) ambacho hakina maji kutokana na mota hizo kuyafyonza na kuuzia wananchi ndoo moja Sh 200 tofauti na bei halali ya Dawasco ya Sh 20.
Katika mtaa wa Kagera, nyumba ilikutwa na mota nane huku mabomba yakiwa yametawanywa katika baadhi ya nyumba za wananchi kutoa huduma hiyo huku mabomba ya Dawasco yakiwa yamekauka kutokana na mota hizo kutumika kufyonza maji kwenye mabomba hayo.
Aidha, katika eneo la Mkwajuni, mabomba ya inchi nane mali ya Dawasco yalitobolewa kwa ustadi mkubwa huku maji yakielekezwa upande wa wananchi kuwasambazia na kuuziwa kwa bei kubwa inayofanya wananchi kulalamika kila siku kutokana na huduma ya maji.
Akizungumzia tukio hilo,  Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kagera, Juma Jangilaga, alisema  suala la mabomba ya maji ya Dawasco kukatwa na wezi ni tatizo la Kampuni hiyo kwani amekuwa akifuatilia na kuripoti hali hiyo lakini ufumbuzi haukupatikana.
Katika mtaa huo, takriban nyumba zaidi ya tano zinadaiwa kujiunganishia mabomba hayo kwa njia ya wizi huku wakiyatawanya kwa wengine kinyemela.
Akizungumzia operesheni hiyo, Sadiki alisema asilimia 30 ya maji yanayopotea kila siku kutokana na kuibwa Serikali kupoteza Sh bilioni mbili kila siku.
Kuhusu maeneo yaliyokamatwa na mota, aliiamuru Dawasco kukata huduma hiyo huku ikitafuta njia mbadala kuhakikishia wananchi wa maeneo hayo hawahangaiki kwa kukosa huduma.
Aliitaka Dawasco inunue maboza yatakayofikisha huduma ya maji kwa bei  nafuu kwa wananchi ili kuwapunguzia ukali wa maisha.
Aliitaka pia kuingia mkataba na wauza maji wa maboza na kuwatambua kisha kuwasajili ili  walipe kodi kwani ni wafanyabiashara kama wengine.
Alihimiza wafanyakazi Dawasco kujisafisha kwa kuwa kuiba maji na kuyaunganisha kwa wananchi inafanywa kwa utaalamu mkubwa, hivyo wajidhibiti.
Aligeukia wenyeviti wa serikali za mitaa akiwataka kutoa taarifa za wizi huo unaofanyika ili kwamba isijeeleweka, kuwa nao wanashiriki kuhujumu Serikali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Dawasco, John Midala alisema wako kwenye mchakato wa kununua mita za maji kama za Luku kuanzia Aprili ambazo watumiaji watakuwa wakilipia kadri wanavyotumia.

No comments: