WASHITAKIWA 54 WAMKANA SHEKHE PONDA KORTINI...

Shekhe Ponda Issa Ponda akifuatilia kesi yake mahakamani.
Washitakiwa 54 wanaokabiliwa na mashitaka ya uchochezi na kufanya maandamano bila kibali wamekana kuwa wafuasi wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Shehe Issa Ponda.
Washitakiwa hao wanadaiwa kufanya maandamano kutoka katika misikiti iliyopo maeneo mbalimbali Dar es Salaam kwa lengo la kushinikiza Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuondoa zuio la dhamana kwa Shehe Ponda.
Walikana kuwa wafuasi wa Ponda katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati wanasomewa maelezo ya awali na Wakili wa Serikali Peter Njike mbele ya Hakimu Sundi Fimbo.
Wakili Njike alidai Februari 15 mwaka huu, walikamatwa wakifanya maandamano yasiyo halali huku wakiwa na visu,vipeperushi, mawe na mabango yaliyochochea maandamano pia walikaidi amri ya polisi iliyozuia maandamano hayo.
Baadhi yao walidai walikamatwa kwa sababu ni Waislamu na walikuwa na ndevu. Walikana kufanya maandamano na kukaidi amri ya Polisi. Pia walikiri kukutwa na visu na vipeperushi ambavyo walidai havikuwa vya kuhamasisha maandamano hayo.
Upande wa Mashitaka ulidai, washitakiwa ni wafuasi wa Shehe Ponda kwa kuwa lengo la maandamano yao ni kuomba dhamana ya Shehe huyo anayekabiliwa na kesi ya uchochezi na kujimilikisha isivyo halali kiwanja cha Chang’ombe Markazi.
Washitakiwa wanadaiwa kula njama ya kutenda kosa, kukusanyika pasipo uhalali, jambo lililosababisha uvunjifu wa amani, kushiriki kufanya vurugu na kukaidi amri ya Polisi iliyowazuia kuandamana.
Katika mashitaka mengine washitakiwa Salum Makame, Said Iddi na Ally Nandumbi, wanadaiwa kuwashawishi wenzao kufanya mkusanyiko isivyo halali kwa kugawa vipeperushi na mabango, yaliyokuwa yakiwataka kufanya mikusanyiko hiyo.
Kama ilivyo kwa Shehe Ponda na Swalehe Mukadam, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) amewasilisha hati ya kuzuia dhamana dhidi ya Makame, Iddi na Nandumbi na Mahakama imezuia dhamana kwa washitakiwa wengine 51 hadi hali ya usalama itakapotulia. Kesi inaendelea kusikilizwa leo.
Katika hatua nyingine, Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepokea maelezo ya onyo ya Shehe Swalehe Mukadam aliyekiri kuhusika katika mchakato wa kuvamia kiwanja cha Chang’ombe Markazi kama sehemu ya ushahidi wa upande wa mashitaka.
Maelezo hayo yalipokewa jana wakati Mahakama ikisikiliza kesi ndogo ndani ya kesi ya  uchochezi na wizi wa mali zenye thamani a Sh milioni 59 inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Shehe Issa Ponda, Mukadam na wenzao 48.
Hakimu Victoria Nongwa alisema maelezo hayakuchukuliwa kwa utaratibu wa kisheria, kwa sababu askari alipitisha zaidi ya saa tatu ya kumhoji mtuhumiwa na hawakwenda katika Mahakama yoyote kuomba waongezewe muda wa kufanya hivyo.
Hata hivyo alisema anapokea kielelezo hicho kwa kuwa jambo hilo haliwezi kuathiri utoaji wa haki katika uamuzi wake.
Juzi Askari wa Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Sajenti Mkombozi Mhando (46) alidai kuwa Novemba mosi, mwaka jana alimhoji Shehe Mukadam katika Kituo cha Polisi Kati na kuchukua maelezo yake ya onyo.
Shehe Mukadam na wenzake 48 wanakabiliwa na  mashtaka  manne, likiwemo la wizi wa mali yenye thamani ya Sh milioni 59.6, uchochezi na kuingia kwa jinai katika ardhi inayomilikiwa na Kampuni ya AgriTanza Ltd kwa nia ya kujimilikisha  isivyo halali.

No comments: