WAKRISTO WAENDELEA KUPIMWA IMANI ZANZIBAR...

Watu wasiojulikana wamechoma Kanisa la waumini wa Siloam lililopo Kiyanga kilometa saba  nje kidogo ya mji wa Unguja na kusababisha uharibifu mkubwa.
Hili ni tukio la pili kwa Kanisa hilo lenye wafuasi 100 kushambuliwa,  baada ya mwaka jana kuvunjwa ukuta ujenzi ulipokamilika.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Jeshi la Polisi,  Yussuf Ilembo jana alithibitisha tukio hilo na alifika kanisani hapo kushuhudia uharibifu uliofanyika.
Ilembo akifuatana na makachero, alisema hatua za mwanzo za uchunguzi zinaonesha kuwapo hujuma dhidi ya Kanisa hilo ambalo sehemu za ndani ziliharibiwa.
“Tunafanya uchunguzi, ndiyo unaona makachero wakiwa na vifaa vyao wakipima eneo lililoharibiwa kwa moto,” alisema Ilembo na kukiri kwamba ni mara ya pili kwa Kanisa hilo kushambuliwa.
Alisema wataanza kufuatilia kumbukumbu za nyuma kuhusu taarifa za kukamatwa kwa baadhi ya watu waliohusikana na tukio la kwanza la kuvunjwa kwa Kanisa hilo.
Mchungaji Msaidizi wa Kanisa hilo, Penuel Elisha alisema alipokea simu kutoka kwa mlinzi wa Kanisa saa 11 alfajiri jana akipewa taarifa ya tukio hilo hilo.
Kwa mujibu wa Mchungaji, mlinzi alimwambia walikuwapo watu wakirusha mawe na baadaye kulichoma Kanisa.
Hata hivyo,  Mchungaji  alikiri kuwapo kwa msuguano wa muda mrefu na uongozi wa Msikiti wa Kiyanga, ambao umekuwa ukihoji sababu za kujengwa kwa Kanisa hilo na kutaka kujua aliyewapa kiwanja.
“Hapa tunakabiliwa na mgogoro wa muda mrefu na uongozi wa Msikiti wa Kiyanga, mwaka jana walituita na kutuuliza nani aliyetupa kiwanja na kama tuna hati ya kujenga Kanisa,” alisema.
Alisema katika kikao hicho walionesha hati ya kumiliki kiwanja na shughuli za ujenzi wa Kanisa hilo kihalali.
“Ndiyo maana mimi sitaki kuuita huu kuwa ni mgogoro...sisi tunamiliki kiwanja hiki kihalali, sasa tatizo wapo watu hawataki tuwe hapa kutokana na kujenga Kanisa tu,” alisema.
Kulingana na maelezo ya Mchungaji, katika tukio la kuvunjwa kwa Kanisa hilo mwaka jana, watu kadhaa walishikiliwa na Polisi na kisha kuachwa.
Mlinzi wa Kanisa hilo, Musa Jackson, alisema kwa muda wa wiki mbili wamekuwa wakipokea taarifa za vitisho na kuripoti Polisi.
Akizungumza na mwandishi, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema kilichochomwa si Kanisa ibali viti vya plastiki ndani ya Kanisa.
Alisema jengo la Kanisa halikuguswa. Kwa mujibu wa Kamishna, nyumba hiyo ya ibada imejengwa kwa matofali na haina milango wala madirisha na haikuguswa.
“Inaonesha lengo la watu waliofika, lilikuwa ni uharibifu lakini katika jengo kitu ambacho kiliweza kuharibiwa ni hivyo viti hata jengo lenyewe halikuguswa,” alisema Mussa.
Alisema hadi sasa hakuna idadi kamili ya waliokamatwa kwa kuwa wanaendelea kukamata watu wanaoshukiwa na kuwahoji.
Tukio hilo la kuchomwa Kanisa limekuja siku chache baada ya Padri Evarist Mushi (55) wa Kanisa Katoliki kuuawa Jumapili visiwani humo kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.
Nalo Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania(BAKWATA), limesema viongozi wa dini wanapaswa waenziwe, wathaminiwe na walindwe kwa kuwa ni muhimu katika jamii.
Mufti wa Tanzania, Shekhe  Issa bin Simba alisema hayo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Dar es Salaam kuhusu mauaji ya Padri Mushi.
Alisema BAKWATA katika kikao chake cha Baraza la Ulamaa limepokea kwa masikitiko makubwa kuuawa kwa Padri huyo.
“BAKWATA kwa niaba ya Waislamu wote Tanzania linalaani vikali kitendo hicho cha mauaji ya padri huyo… maisha ya binadamu yeyote lazima yathaminiwe kama Qur’an Tukufu inavyotuagiza,” alisema.
Alisema, “Waislamu wote Tanzania tunatoa pole kwa Wakatoliki wote, Wazanzibari wote na Watanzania wote kwa ujumla kwa msiba huu mkubwa”.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limesema limeanza kukamata wachochezi wa uvunjifu wa amani kupitia njia mbalimbali ikiwamo mitandao ya kijamii.
Akizungumza na waandishi wa habari jana  Dar es Salaam,  Msemaji wa Polisi, Advera Senso alisema Polisi inafahamu, kwamba wachochezi wa vurugu na uvunjifu mwingine wa amani unatokana na watu kutumwa na wafadhili au kujituma kwa sababu ya kutimiza matakwa ya kimaslahi.
 “Wawe wanasiasa, wana dini au raia wa kawaida, wakijihusisha na uchochezi unaosababisha uvunjifu wa amani, hatutawachekea kwa sababu watakuwa wanatenda makosa ya jinai. Bila kujali wanatenda uhalifu huo katika maeneo gani au kwa mtindo gani, ilimradi tuna ushahidi kuwa wanachokifanya ni kosa la jinai, tutawashughulikia kisheria,” alionya.
Senso alitaja njia zinazotumika kufanya uchochezi huo kuwa ni mitandao ya jamii hususan blogu, vyombo vya habari, wahubiri wa dini wasio na maadili na wafanyabiashara wa kanda za mahubiri ya dini na siasa. 
“Baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya jamii hususan blogu havizingatii maadili na badala yake, vinakuwa mstari wa mbele kutoa habari zinazohamasisha uchochezi wa chuki na uvunjifu wa amani.
“Ni vema ikafahamika, kuwa tunafanya ufuatiliaji wa kila andiko, chapisho na tamko kuona kama kuna jinai, ili tukamate wahusika na kuwachukulia hatua zaidi,” alisema.
Alisema hilo ni miongoni mwa maazimio waliyoyafikia katika mkutano wa wakuu wa Jeshi hilo, uliomalizika Dodoma hivi karibuni.

No comments: