WAANGLIKANA WAPATA ASKOFU MKUU MPYA...

Dk Jacob Erasto Chimeledya.
Askofu wa Kanisa la Anglikana wa Dayosisi ya Mpwapwa, Dk Jacob Erasto Chimeledya (56) amechaguliwa kuwa Askofu Mkuu mpya wa Kanisa la Anglikana nchini.
Askofu huyo anarithi nafasi ya Askofu Valentino Mokiwa ambaye amemaliza muda wake kwa mujibu wa katiba ya kanisa hilo.
Mkuu huyo mpya ataongoza kanisa hilo kwa kipindi cha miaka mitano na anakuwa askofu mkuu wa sita.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Katibu Mkuu wa kanisa hilo, Dk Dickson Chilongani alisema uchaguzi wa askofu huyo ulifanyika jana katika Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika.
Alisema mkutano uliomchagua askofu huyo ulihudhuriwa na wajumbe 129 kati ya wajumbe 140 kati yao wakiwemo maaskofu 25 kutoka dayosisi mbalimbali hapa nchini.
“Kwa kawaida katika uchaguzi askofu yeyote mwenye umri chini ya 60 huwa ni mgombea hivyo katika uchaguzi huo maaskofu 21 walikuwa na sifa za kugombea,” alisema.
Akielezea historia yake, Katibu huyo alisema Askofu Dk Chimeledya alizaliwa  mwaka 1957 na baada ya kumaliza elimu ya sekondari alichukua stashahada ya Theolojia katika Chuo cha St Philipo Kongwa.
“Baadae akaenda Kenya kuchukua shahada ya Divinity katika chuo cha St Paul kabla ya kwenda kusomea shahada ya uzamili katika theolojia nchini Marekani ambayo alimaliza mwaka 2003 na baada ya kuteuliwa kuwa askofu alipewa shahada ya falsafa ya heshima,” alisema.
Alisema mwaka 2007 Dk Chimeledya aliteuliwa kuwa askofu mwandamizi wa Jimbo la Mpwapwa chini askofu Simon Chiwanga.
Alisema baada ya Askofu Chiwanga kustaafu ndipo Dk Chimeledya alipoteuliwa kuwa askofu wa Dayosisi hiyo ya Mpwapwa mwaka 2007.
Alisema askofu huyo mpya anatarajiwa kuwekwa wakfu mwishoni mwa Mei mwaka huu mjini Dodoma.

No comments: