PAPA MPYA KUPATIKANA MAPEMA KABLA YA MUDA ULIOPANGWA......

Baba Mtakatifu mstaafu, Papa Benedict XVI
Uchaguzi wa Papa mpya unaweza kuanza mapema kuliko tarehe iliyotarajiwa Machi 15, imebainika jana.
Chini ya sheria za Vatican, kawaida kuna siku kati ya 15-20 za kusubiri kabla Makardinali kupiga kura kwenye mkutano wa faragha baada ya nafasi ya upapa kubaki wazi.
Lakini tangazo hilo la Papa Benedict XVI kwamba atastaafu Februari 28, linamaanisha watakuwa na muda wa kutosha kwenda mjini Roma kushiriki kwenye uchaguzi huo.
Msemaji wa Vatican Mchungaji Federico Lombardi alidai kwamba taratibu za urithi wa papa zilikuwa wazi kutafsirika na kwamba "hili ni swali ambalo watu wanalijadili."
Alisema: "Inawezekana kwamba mamlaka za kanisa zinaweza kuandaa pendekezo litakalochukuliwa na makardinali katika siku ya kwanza baada ya tangazo hilo la nafasi ya papa kwenda nalo wakati wa kuanza kwa mkutano wa faragha.
Tarehe ya kuanza kwa mkutano huo wa faragha ni muhimu kwa sababu Wiki Takatifu inaanza Machi 24, kwa Misa ya Jumapili ya Matawi ikifuatiwa na Jumapili ya Pasaka Machi 31.
Ili kuweza kuwa na Papa mpya kwa wakati kwa ajili ya kipindi chote cha litrujia katika kalenda ya kanisa, atahitaji kutawaza kama Papa hadi kufikia Jumapili ya Machi 17.
Huku ukiwa umetolewa muda mfupi, minong'ono imeibuka kwamba baadhi ya maandalizi yamekuwa yakifanyika kuwezesha kuanza kwa mkutano huo wa faragha mapema kuliko maandiko ya sheria yanavyoruhusu.
Maswali kuhusu kuanza kwa mkutano huo wa faragha yameibuka tangu Benedict kutangaza Februari 11 kwamba atastaafu, Baba Mtakatifu wa kwanza katika miaka 600 kung'atuka badala ya kuendelea kuongoza hadi mauti yatakapomfika.
Lombardi pia ametoa taarifa zaidi kuhusu mkutano wa mwisho wa Benedict na mipango ya kustaafu, akisema tayari watu 35,000 wameomba tiketi kwa ajili ya kuhudhuria mkutano huo utakaofanyika St. Peter's Square, Februari 27.
Alisema Benedict atatumia mapumziko ya takribani miezi miwili katika Castel Gandolfo kusini mwa Roma mara tu baada ya kung'atuka kwake, kuruhusu muda wa kutosha ili ukarabati uweze kukamilika kwenye makazi yake ya ustaafu - jumba la utawa lililobadilishwa ndani ya uzio wa Vatican.
Hiyo inamaanisha Benedict anatarajiwa kurejea Vatican, sio tena kama Papa, nyakati za Aprili au mwanzoni mwa Mei, alisema Lombardi.

No comments: