HIVI NDIVYO PADRI MUSHI ALIVYOUAWA KWA RISASI ZANZIBAR...

Marehemu Padri Evaristus Mushi.

Mapema asubuhi ya leo, kisiwa cha Zanzibar kimeingia doa baada ya Padri wa Kanisa Katoliki la Minara Miwili lililopo eneo la Mji Mkongwe, Evaristus Mushi (56) kufariki dunia kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.
Tukio hilo lililotokea majira ya Saa 1 asubuhi wakati Padri huyo akiendesha gari lake kwenda kuongoza ibada katika Kanisa la Mtoni lililopo nje kidogo ya mkoa wa Mjini Unguja, ndipo ghafla aliposhambuliwa kwa risasi kichwani na watu hao waliokuwa kwenye pikipiki aina ya Vespa.
Kwa kuwa gari alilokuwamo Padri huyo lilikuwa kwenye mwendo, ndipo likaacha njia na kuparamia nyumba kadhaa za jirani ambapo madhara yake hayakuweza kufahamika mara moja.
Hadi mwili wa Padri huyo unafikishwa hospitalini majira ya Saa 2 asubuhi hakukuwa na ofisa yeyote wa polisi zaidi ya waumini kadhaa wa kanisa hilo waliokuwa wakilia kwa uchungu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Unguja, Aziz Juma alithibitisha kutokea tukio hilo na kusema kuwa Jeshi la Polisi limeanza upelelezi kujua chanzo cha tukio hilo na kuwakamata waliohusika na mauaji hayo.
Hilo ni tukio la pili kutokea kisiwani humo, baada ya lile la kupigwa risasi kwa Padri Ambros Mkenda wa Kanisa la Mpendae mwaka jana.
Padri huyo alipigwa risasi na watu wasioulikana wakati akielekea nyumbani baada ya kukamilisha ibada.

No comments: