MWISHO WA "WAUZAJI SURA" BUNGENI SASA UMEWADIA....

Wabunge wakiwa katika moja ya matukio yaliyonaswa yanayoaminika kulishushia hadhi Bunge, mjini Dodoma.
Ili kukomesha vurugu na wabunge wanaotafuta umaarufu wa bei chee maarufu kama 'wauza sura', Bunge limeanza mchakato wa kusitisha matangazo ya vikao vyake kurushwa moja kwa moja na televisheni, kama ilivyo sasa.
Badala yake linatarajia kuanzisha chaneli yake,   itakayorusha yaliyojiri kwenye vikao hivyo, baada ya kuhaririwa.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah, alisema hayo jana alipokutana  waandishi wa habari Dar es Salaam, kuzungumzia  yaliyojiri katika mkutano wa 10 wa Bunge, uliomalizika hivi karibuni.
Alisema uamuzi wa kutorusha matangazo hayo moja kwa moja, unatokana na hali halisi ya vurugu zinazotokea ndani ya Bunge.
“Bunge sasa limekuwa kama ukumbi wa siasa, kanuni hazifuatwi, kila mtu anasimama kivyake na kutaka kuzungumza ilimradi tu aonekane kwa wananchi kuwa naye yumo.
“Hali hii haileti picha nzuri hata kidogo, sasa tumependekeza kutokurushwa moja kwa moja kwa vikao hivi vya Bunge,” alisema Dk Kashililah.
Alitoa mfano: “Sote tunaona yanayojiri kila siku bungeni  … mbunge anasimama na kutamka kuhusu utaratibu, mwongozo wa Spika, hakuna kitu kama hicho huku kote ni kuvunja kanuni na kanuni hizi jamani ziko wazi kabisa, lazima Bunge liendeshwe kwa utaratibu, pale si klabuni wala sokoni.”
Alisema kupitia Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Bunge, tayari wameanza kuwasiliana na Tume ya Mawasiliano (TCRA) na Shirika la Taifa la Utangazaji (TBC), ili kuweka utaratibu mzuri wa kurusha matangazo hayo,   na kupatiwa chaneli yao.
“Tunachotaka hata kama hawa TBC wataendelea kurusha matangazo, basi kuwe na utaratibu mzuri wa udhibiti wa matukio ndani ya Bunge. Hili si jambo geni, hata nchi nyingi za wenzetu wanafanya hivi,” alisema.
Alisema katika hali halisi, mambo mengi yanayofanyika ndani ya Bunge hilo kwa upande wa habari, ni kosa, ikiwemo upigaji picha wa wabunge ambao hawazungumzi.
“Katika Sheria za Mabunge ya Jumuiya ya Madola, kumpiga picha mbunge asiyezungumza ni kosa, hata kama amelala kwani nani kawaambia kulala ni kosa?” Alihoji.
Dk Kashililah alisema Bunge linatarajia kupeleka kwa mamlaka husika, majina ya wale wote waliotuma ujumbe mfupi na kupiga simu za matusi kwa Spika Anne Makinda na Naibu wake Job Ndugai, kwa kuwa tayari majina ya wamiliki wa namba hizo yamepatikana.
“Nawahakikishieni wale wote waliotuma matusi yao kwenye simu ya mheshimiwa, majina yao tunayo, tutayawasilisha kwenye vyombo husika na lazima wataitwa kuhojiwa,” alisisitiza.
Alisema matusi hayo hayajazuia mfumo wa Bunge kuweka wazi namba za simu za viongozi, kwa kuwa ni kwa faida ya watu wengi na si wachache wenye nia mbaya.
Alisema kuhusu hoja ya Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, kuhusu masuala ya elimu, uamuzi wa kuiondoa kwenye ratiba haukufanywa kiholela kama inavyodaiwa, bali ilikubaliwa ndani ya Kamati ya Bunge ya Uongozi, ambayo wajumbe wake pia wamo viongozi kutoka vyama vya upinzani.
Hata hivyo, alibainisha kuwa hoja hiyo itawasilishwa katika Mkutano ujao wa Bunge na hoja nyingine tisa ambazo hazijawasilishwa, wabunge wenye hoja hizo wametakiwa kutoa taarifa ya kuomba ziwasilishwe.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen-Kijo Bisimba, akitoa tathimini ya mwenendo wa Mkutano uliopita wa Bunge jana, alisema  ipo  haja ya wabunge kujiangalia kwa karibu katika uwezo na utayari wao kujadili masuala ya maslahi ya taifa, bila kuingiza ushabiki na maslahi binafsi.
Pia walitaka Spika wa Bunge kutumia nafasi yake kuelekeza Bunge, ili lifanye kazi zake vizuri zaidi, huku wabunge wakitambua uwepo wao bungeni ni kwa maslahi ya Watanzania na hoja zinazogusa wananchi zipewe kipaumbele.

No comments: