MKONO ALIOKATWA MWANAMKE ALBINO WAPATIKANA...

Mkono wa mwanamke mlemavu wa ngozi, Maria Chambanenge, uliokatwa katikati ya wiki hii, umepatikana ukiwa umezikwa porini katika Kijiji cha Miangalua, wilayani Sumbawanga.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, Peter Ngusa, alionesha mkono huo jana ukiwa umeanza kuharibika kwa Mkuu wa Mkoa, Stella Manyanya.
Akisimulia kisa kilichosababisha mkono huo kukatwa, ambacho sasa ni madai dhidi ya watuhumiwa wa unyama huo, Kamanda Ngusa pia alidai kuwa wameshakamata watuhumiwa watano.
Taarifa za Polisi zinaeleza kuwa mkazi wa kijiji hicho, Linus Silukala (42), ndiye aliyekuwa wa kwanza kukamatwa na anadaiwa ndiye aliyemshawishi mume wa Maria, Gabriel Yohana ili mkono wa mkewe ukatwe wapate utajiri. 
Inadaiwa kabla ya ushawishi huo, Silukala alifika katika  kitongoji cha Mkoe katika Kijiji cha Miangalua na kufanya urafiki na Gabriel na baadae kumshawishi  wamkate Maria mkono.
Kwa mujibu wa madai ya taarifa hizo, baada ya kumkata mkono, Silukala aliahidi kuupeleka kwa mganga wa kienyeji,  Peter Kazanda ‘Kaponda’ (53), ili awasaidie wapate  utajiri kupita kiasi.
Baada ya kushawishiwa, inadaiwa Gabriel alimshirikisha mdogo wake, Gaudensi Yohana, ambaye inadaiwa  ndiye aliyemkata shemeji yake huyo mkono wake wa kushoto.
Inadaiwa Gaudensi na Silukala, ambao wote wako mbaroni, waliufikisha mkono huo kwa Kazanda na kwa pamoja walienda kuuzika  mkono  huo  porini,  wakisubiri  utakapoanza kuoza na kutoa funza, ndipo  nao waanze ‘kuogelea’ kwenye bahari ya ukwasi.
Wakati mkono huo ukipelekwa kwa mganga na kuzikwa, inadaiwa Gabriel, ndio alikuwa amempeleka mkewe hospitali kwa matibabu.
Hata hivyo, inadaiwa wakati wameuzika, Silukala alianzisha mawasiliano na mfanyabiashara wa Sokomatola jijini Mbeya, Mtogwa Suleiman (30), kwa ajili ya biashara ya kuuza mkono huo.
Wakati wakiwa katika mawasiliano hayo, inadaiwa Polisi walimkamata Silukala, ambaye baada ya kubanwa, alianika mtandao mzima wa biashara hiyo ya kinyama.
Kamanda Ngusa alikiri kuwa Silukala alimtaja mganga Kazanda na baadae alimtaja mfanyabiashara wa Sokomatola jijini Mbeya, Mtogwa Suleiman (30), aliyekuwa anunue mkono huo.
Kwa mujibu wa Kamanda Ngusa, kwa kuwa Silukala alikuwa na mawasiliano na mfanyabiashara huyo, polisi walitumia mawasiliano hayo hayo kumnasa.
Alidai Polisi waliweka mtego, kwa kumpigia mfanyabiashara huyo simu na kumuahidi kumpelekea mkono huo, ambapo bila yeye kufahamu kuwa huo ni mtego, ‘alijilengesha’ mikononi mwa Polisi.
Wake wenza wa Maria,  Honoratha Xevia maarufu Mama Daria na mwenzake Estha Pesambili maarufu  Mama Ray, pia wamedai kuwa mgeni aliyefikia nyumbani kwao na kuishi hapo, ni Silukala na kuwa amekamatwa.
“Huyu mgeni, Silukala yeye tulikuwa tukiishi naye nyumbani, akisaidia kupalilia mashamba yetu hapa. Siku hiyo ya tukio saa 10 jioni, aliondoka nyumbani hapa bila ya kutuaga na hakurudi hadi tulipopata taarifa kuwa amekamatwa akihojiwa Polisi mjini Sumbawanga,“ alisema Mama Daria.
Manyanya hakuweza  kujizuia na kujikuta  akibubujikwa   machozi hadharani, baada ya kukabidhiwa mkono huo  baada ya kufukiwa  porini.
Alijikuta akilia machozi mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama, pale Kamanda Ngusa alipouonesha  hadharani  mkono huo juzi saa tatu usiku mbele  ya majengo  ya Hospitali  ya Mkoa wa Rukwa, ambao ulikuwa  umevingirishwa na majani  ya mgomba.
Mkono huo ulikuwa tayari  umeanza kutoa harufu kali na ulipooneshwa tu, mbali na Mkuu wa Mkoa, baadhi ya wajumbe wengine walibubujikwa na  machozi ya huzuni.
Manyanya alimwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda, kuhakikisha wote watakaobainika kujihusisha unyama huo wakamatwe  na kufikishwa kwenye  vyombo vya dola.
“Kitendo hiki ni unyama uliopita ustaarabu wa kibinadamu  hivyo naagiza Polisi ihakikishe  watuhumiwa  wote wanafikishwa mahakamani kwa  kuwa  tayari  ushahidi upo  na wenyewe wameonesha  mkono huo walikoufukia.
“Tunatarajia  hakutakuwa na visingizio  vya kutaka kuharakisha  kutolewa kwa hukumu ya shauri  hilo,”  alisema
Maria  ambaye ni mama wa  watoto  wanne, kitinda mimba akiwa na umri wa miezi miwili,  bado amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Rukwa mjini kwa matibabu  huku hali yake ikielezwa kuimarika.

No comments: